Prime
Ninja: Kucheza nje ilikuwa suala la muda
MAISHA ya soka yanapanda na kushuka kama anavyosimulia aliyekuwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anavyojitoa kurejesha makali, ili atakapoanza majukumu asianze upya.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Ninja anasema kabala hajasaini kuichezea Lubumbashi Sport ya DR Congo, hakuwahi kuacha programu za mazoezi kama inavyotakiwa kwa mchezaji anayelenga kufika mbali.
Anasema Jumatatu na Jumanne alikuwa anafanya mazoezi ya ufukweni, Jumatano ufukweni kidogo kisha anaingia uwanjani. Alhamisi na Ijumaa anafanya gym asubuhi na jioni anatafuta mechi za kucheza. “Mchezaji lazima ujitunze, kwani soka ni kazi yangu na nina watu wanaonitegemea, hivyo siwezi kufanya mchezo kujituma na kuhakikisha nakuwa fiti,” anasema beki huyo.
KAJIUNGA NA TIMU
Ninja tayari amejiunga kambini katika timu yake mpya ya Lubumbashi na mambo yakikaa sawa anaweza akaanza kuichezea. “Nipo kambini na Ligi Kuu ya Congo (DRC) ilishaanza, hivyo kuna baadhi ya mambo yakikaa sawa mtaanza kuniona nacheza,” anasema.
Aliipataje timu hiyo? “Kuna mtu yupo Congo alinitafuta na kunipa dili hilo, wakati huo nilikuwa nimepata nyingine kama tatu za nje, vivyo hivyo za nyumbani zilikuwa tatu, kikubwa nimefurahi najiandaa na majukumu mapya,” anasema Ninja.
Anasema bado ana ndoto kubwa ya kuacha alama kwenye soka akiamini kuna wakati mchezaji kiwango kinapanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali.
“Mwaka 2021 nikiwa Yanga nilifanyiwa upasuaji wa goti nje ya nchi. Nikapitia kipindi cha kuuguza majeraha kisha nikakaa sawa. Wakati huohuo kwenye nafasi yangu kina Bakari Mwamnyeto na Dickson Job walikuwa wamewaka, hivyo ingekuwa ngumu kwa kocha kutowapanga nikapewa nafasi kubwa mimi,” anasema.
“Kwa msimu ulioisha baada ya kuona nipo fiti kabisa niliomba kwenda kucheza kwa mkopo Dodoma Jiji, ambako nilicheza mechi kadhaa baadaye nikarejea tena Yanga chini ya kocha Nabi ambaye alijaribu kumpa nafasi kila mchezaji nisingeshindwa kucheza, kilichofanya nisiambulie mechi hata moja ni kuchelewa kuchukua ITC kutoka Dodoma Jiji.”
KUONDOKA YANGA
Ninja anasema ni kawaida mchezaji kuondoka au kuachwa na timu, hivyo hashangazwi baada ya kumaliza mkataba klabu hiyo kutohitaji kuendelea naye.
Kwa mara ya kwanza Ninja alijiunga na Yanga 2017-2019 kisha akapata dili kwenda MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech ambayo ilimpeleka kwa mkopo LA Galaxy ya Marekani 2019 alikocheza miezi sita kisha akarejea Yanga ambako alidumu 2019-2023.
“Maisha ya mchezaji hayana makazi ya kudumu, unapotoka timu moja kwenda nyingine unajifunza na umakini unaongezeka. Bado nacheza natakiwa kupambana zaidi, kwani kinachohitajika kwenye timu ni kiwango kulingana na timu husika,” anasema na kuongeza:
“Yanga ni timu iliyo na malengo makubwa ndio maana kuna ushindani kwa kila nafasi na siyo kila mchezaji anayeondoka kiwango chake kimekufa. Pia mchezaji anapopata nafasi kwenye timu ya namna hiyo lazima ajue kutumia fursa akijua walikuwepo wengine na wataendelea kuja.”
USHAURI WA CANNAVARO
Hadi sasa Ninja anawasiliana na aliyekuwa nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye anamshauri kutokata tamaa ili kuhakikisha anapigania ndoto zake bila kujali mazingira yanayomzunguka.
Ikumbukwe wakati Cannavaro anastaafu 2018 jezi yake namba 23 alimkabidhi Ninja na hiyo ni kati ya sababu zinazofanya ukaribu wao uendelee kuwapo.
“Ingawa kwa sasa tunaweza tukawasiliana kwa wiki mara tatu kutokana na kupisha muda. Cannavaro anaishi Marekani kwa sasa pamoja na hayo yote hajaacha kuniambia nina muda wa kuonyesha nilicho nacho kwenye soka,” anasema.
Anapoulizwa angependa nani avae jezi namba 23 Yanga? Ninja anajibu: “Sitamani avae mtu ingekuwa amri yangu ingepumzishwa kwanza. Pia nitakapokuwepo siwezi kusema nitavaa namba hiyo au la kwani nikimkuta anaitumia mtu siwezi kumvua, ingawa nikiipata ipo huru nitafurahi zaidi.”
JASHO LA SOKA
Ninja anasema kwa asilimia kubwa maendeleo aliyofanya yametokana na kucheza Yanga akimjengea nyumba mama, kajenga yake na pia amewasomesha wadogo zake watano.
“Marekani sikupata pesa nyingi. Asilimia kubwa ya vitu nimefanya nikiwa Yanga ambapo nina miradi midogomidogo pia namiliki gari. Bado soka halijanilipa kihivyo, ndio maana naendelea kucheza hadi sasa.”
Kuhusu maisha ya Marekani, jambo kubwa alilojifunza ni namna wachezaji wenye ndoto kubwa wanavyotakiwa kuishi bila makocha kutumia nguvu kubwa ya kuwasukuma.
MAKOCHA WAKE
Beki huyo anasema hawezi kumsahau kocha George Lwandamina kwani ndiye aliyependekeza asajiliwe Yanga, hivyo alisaidia kipaji chake kuonekana kwa ukubwa zaidi tofauti na alivyokuwa Jang’ombe ya Zanzibar ambako pia alikuwa maarufu mtaani kwao hadi wakampa jina la Ninja.
“Baada ya kusajiliwa sikuanza moja kwa moja kucheza, nilikuwa naumia. Kuna muda alinipa nafasi nikawa najiona sifiti majukumu wakati huo, kisha akaniita akaniambia umeonaje na unajua kwa nini nilikuacha ujifunze kwanza. Baadaye nikapata uzoefu na nikawa naisaidia timu,” anasema
“Baada ya kuondoka Lwandamina alikuja Mwinyi Zahera ambaye alinipa nafasi sana hadi nikaonekana nje, hivyo makocha hao ni kama wazazi wangu. Kwa upande wa wachezaji ambao ni washikaji hadi tumekuwa kama ndugu sasa ni Mudathir Yahya, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Pius Buswita, Juma Makapu wapo wengine wengi.”
HADITHI YA MAPENZI
Akisimulia namna alivyompa mkewe Shemsa Mussa Alawi utacheka. Haikuwa safari rahisi hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa Machi 28, 2022.
“Nilianza kumfukuzia tangu 2010 akanikubali mwishoni mwa 2011. Kwanza tulikuwa tunamgombania mimi na kaka zangu wa tumbo moja. Alikuwa na msimamo sana. Kaka zangu wakakata tamaa, nikawaambia nitaendelea kupamba hadi kieleweke, nikafanikiwa.
“Mara ya kwanza mimi na kaka zangu tulimuona akienda kumpelekea chakula ndugu yake alikuwa rumande nyumba yetu ilikuwa ya mwisho kisha unafika gerezani, tulikuwa tunaishi kwenye kota kwa sababu baba alikuwa askari. Alikuwa binti mkali sana na mwenye misimamo ya hofu ya Mungu,” anasema mchezaji huyo.
“Chanzo cha kunikubali, siku moja nilikuwa nimetoka kukamua jipu lililonishika mkononi, hivyo nilifungwa bendeji si akaniona na kuniuliza nini kimetokea, nikamjibu nimepigwa na kaka zake baada ya kwenda kumuulizia kwao. Akaanzia kunionea huruma, kisha akaniambia ananipenda kwa mara ya kwanza. Nilihisi kama sijasikia vizuri, lakini aliponiambia nimsindikize ila nisifike kwao nikaamini kaingia laini.”