Namna Man Utd inavyomuaibisha Sir Alex Ferguson
Muktasari:
- Mechi aliyokuwa akiitazama ilipigwa Oktoba 22, 2022 ambayo United ilipoteza 6-3, huku Erling Haaland akifunga mabao matatu peke yake.
KILA inapokuja mechi ya Manchester United na Manchester City kipande fulani cha video huzunguka mitandaoni kikimuonyesha kocha wa zamani wa United, Sir Alex Ferguson akiwa jukwaani akitazama moja ya mechi za watani hao wa Jiji la Manchester.
Mechi aliyokuwa akiitazama ilipigwa Oktoba 22, 2022 ambayo United ilipoteza 6-3, huku Erling Haaland akifunga mabao matatu peke yake.
City ilitangulia kuongoza kwa mabao 4-0 kipindi cha kwanza na ghafla ikaonyeshwa video ya Sir Ferguson akihuzunika jukwaani. Mtangazaji wa mechi hiyo wa kituo cha BBC, Guy Mowbray akaitendea haki kwa kusema maneno yafuatayo: "Sir Alex Ferguson was asked in 2009 if Man City could ever go into a derby as favourites, he said 'not in my lifetime' now it's every time." Hapo alimaanisha "Sir Alex Ferguson aliulizwa mwaka 2009 endapo Man City wanaweza kuingia kwenye dabi kama wababe, akasema 'sio katika uhai wangu' sasa ni kila wakati."
Mowbray alimpiga kijembe Sir Alex Ferguson kwa kauli yake ya Septemba 13, 2009 wakati wa maandalizi ya mechi ya dabi akiwa kocha.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa siku iliyokuwa ikifuata yaani Septemba 14, 2009, Sir Ferguson aliulizwa na mwandishi wa The Independent, Ian Herbert endapo kuna siku itafika Manchester City itaitisha Man United kuelekea mechi yao.
Hapo alijibu kwa kicheko cha dharau, "sio katika uhai wangu" halafu akasema "nadhani niondoke tu", na akaondoka.
Hicho kilikuwa kipindi ambacho Sheikh Mansour ametoka kuinunua Manchester City na anahangaika kuijenga.
Hadi hapo City haikuwahi kuwa kitisho kwa United ya Sir Alex Ferguson kwani iliwahi kushinda mara moja tu kwenye Uwanja wa Old Trafford katika muda wake kama kocha mkuu wa Man United.
United waliingia kwenye mchezo huo wakipigania ubingwa huku City wakipigania 'Top Four". Na mchezo ulipofika, United wakashinda 4-3, Michael Owen akifunga bao la jioooooni.
Sir Ferguson hakuona kama City wanaweza kuwa wababe siku moja mbele ya United. Aliwachukulia kama City walewale waliokuwa na kawaida ya kupanda daraja na kushuka. Hali ilianza kubadilika msimu wa 2011/12 pale Man United walipofungwa 6-1 Old Trafford na Manchester City kuwa mabingwa mwisho wa msimu.
Siku ya kusherehekea ubingwa, Carlos Tevez, nyota wa City aliyetokea United alibeba bango lililosomeka RIP Fergie akiwa na maana PUMZIKA KWA AMANI FERGIE.
Tevez alikuwa akimrushia kijembe Ferguson kwa ile kauli yake ya SIO KATIKA UHAI WANGU, akisema Man City hawatakuja kuwa wababe mbele ya United katika uhai wake. Na sasa wamekuwa, basi labda hayupo hai.
Bango hilo la Tevez lilisababisha klabu yake kuomba radhi kwa Sir Ferguson na Manchester United kwa ujumla, lakini Tevez mwenyewe alikataa kuomba radhi. Kauli ilihusu mechi ya Septemba 14, 2009 na miaka 16 baadaye yaani Septemba 14, 2025 timu hizo zinakutana, huku City wakiingia kama wababe na kuwachanachana United 3-0. NOW IT'S EVERY TIME.
Tangu mara ya mwisho United wawe mabingwa 2012/13, City wameshakuwa mabingwa mara saba. NOW IT'S EVERY TIME. Ama kwa hakika Sir Alex Ferguson hatamani kuiona mechi ya Manchester Derb kwa sababu inamuabisha.