Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namba 866 kwa Sowah na kasi ya kutupia

Muktasari:

  • Katika mechi tatu ambazo timu yake imebakisha ili kumaliza msimu, mshambuliaji huyu ana kazi kubwa kuhakikisha anafanya ambalo halikutarajiwa na yeyote la kumaliza mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara. licha ya kusajiliwa katikati ya msimu.

NI Azam FC na KMC tu ambazo hajazifunga kati ya timu 11 alizocheza nazo tangu amejiunga na Singida Black Stars katika dirisha dogo la usajili msimu. Huyu ni mdunguaji hatari kabisa kutoka Ghana, Jonathan Sowah.

Katika mechi tatu ambazo timu yake imebakisha ili kumaliza msimu, mshambuliaji huyu ana kazi kubwa kuhakikisha anafanya ambalo halikutarajiwa na yeyote la kumaliza mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara. licha ya kusajiliwa katikati ya msimu.

Ili kufikia malengo hayo  mbele yake amesimama mnyama Simba, kuna Dodoma Jiji zote ugenini na mchezo wa kumaliza msimu nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.

Kabla ya mtihani huo, Sowah tayari amethibitisha kuwa ni mwamba kabisa mbele ya lango kwani amehitaji chini ya nusu ya mechi walizocheza vinara wa ufungaji wa Ligi Kuu kuwakaribia.

Kwa kiwango alichokionyesha akiwa na dakika chache ukilinganisha na nyota ambao wanafanya vizuri kwenye eneo hilo kama Clement Mzize na Prince Dube wa Yanga na Charles Ahoua anayekipiga Simba, ni wazi kuwa Sowah ndiye mshambuliaji tishio Ligi Kuu kwani hajahitaji muda mrefu kuizoea ligi.

Nyota huyo amezifunga Kagera Sugar, JKT Tanzania, Yanga, Pamba Jiji, Mashujaa (mawili), Namungo, Fountain Gate, Coastal Union na Tabora United ambayo pia ameifunga mabao mawili.


866

Katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara, vita ya ufungaji imekuwa kali zaidi kuliko misimu uliopita kwani wachezaji wengi wanaonyesha kukitaka Kiatu cha Dhahabu.

Takwimu zinaonyesha kuwa mshambuliaji huyu ndiye mwenye ufanisi mkubwa zaidi katika kufumania nyavu, akiwa amefunga mabao mengi ndani ya muda mfupi ukilinganisha na washambuliaji wote wa ligi.

Sowah amefunga mabao 11 katika mechi 11 tu alizocheza, akitumia jumla ya dakika 866 uwanjani. Hii ina maana kuwa anafunga bao kila baada ya dakika 83, kiwango cha juu zaidi kwa msimu huu hadi sasa.

Wakati Mzize wa Yanga akiwa kinara wa mabao kwa sasa akifikisha 13, Dube na Ahoua wanafuatia wakiwa na 12 kila mmoja na wote wamecheza dakika nyingi zaidi ya Sowah.

Hata hivyo, mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala, mwenye mabao 10 ndani ya dakika 736 (sawa na bao moja katika kila dakika 73), ndiye mwenye takwimu bora zaidi ya wote wanaowania tuzo ya ufungaji pale juu. Mukwala licha ya kucheza mechi 20, amekuwa uwanjani kwa dakika chache zaidi.

Elvis Rupia, ambaye ni mwenzake Sowah katika safu ya ushambuliaji ya Singida BS, ana mabao 10 ndani ya dakika 1,500, akiwa na uwiano wa bao kila baada ya dakika 150. Mwingine wa Yanga, kiungo Pacome Zouzoua, ana mabao 9 kwa dakika 1,364, sawa na bao kila dakika 151.

Katika mazingira hayo, ni wazi kuwa Sowah ameingia kwa kishindo katika vita ya wafungaji, huku akiweka presha kubwa kwa wale waliomtangulia. Ni vigumu kuamini kuwa mshambuliaji aliyeanza kucheza katikati ya msimu sasa yuko hatua chache tu kufikia waliocheza mechi kati ya 20 hadi 26.


KUHUSU KUTUA YANGA

Mwamba huyu anayehusishwa na mipango ya kujiunga na Yanga mwisho wa msimu huu, kwa kasi yake haishangazi anapohusishwa na timu ya wananchi.

“Yanga ni nyumbani kwangu. Singida walipokuja niliwaambia Yanga ndio nyumbani kwangu. Rais wa Yanga (Injinia Hersi Said) ni kama baba kwangu. Huyu mtu ni kama malaika katika maisha yangu kwa mambo aliyonifanyia. Ndio (ni suala la muda tu kabla sijajiunga na Yanga). Natumai hivyo,” alisema Sowah katika mahojiano na mtandao mmoja.

Kauli ya Sowah haitofautiani na ya Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, ambaye ametamba kwamba atafurahi kama yeyote kati ya washambuliaji wao watatu  atamaliza mfungaji bora.

“Iwe yule mwenye mabao 13 (Clement Mzize), au mwenye mabao 12 (Prince Dube) au mwenye mabao 11,” alisema bila ya kumtaja huyo mwenye mabao 11, licha ya kwamba mwenye mabao 11 ni Sowah pekee katika chati ya vinara wa mbio za ufungaji Ligi Kuu Bara hadi sasa.


ANACHOSEMA

Akizungumza na Mwanaspoti, Sowah anasema: “Kazi yangu ni kufunga na ndio kilichonileta hapa, kila nafasi nitakayoipata nitaifanyia kazi, nina malengo na kuhusu kuwa mfungaji bora ndio kitu nakifikiria. Rupia alikuwa kinara, nilifikiria kumpita nimefanikisha, sasa vita ni walio mbele yangu.

“Nilipofika Tanzania kitu cha kwanza niliangalia chati ya wafungaji nikaona Rupia ndiye ambaye amefunga mabao mengi, nikajiwekea malengo ya kuhakikisha nafunga mabao mengi, nashukuru Mungu kasi yangu imeendana na malengo,” anasema.

“Chati ya ufungaji ilinipa nguvu na kuamini kuwa nipo katika nafasi ya kutoa ushindani hilo limeonekana sasa vita iliyobaki ni kupambana kuwafikia walio mbele yangu na ikiwezekana niwapite.”

Anasema ana furaha kucheza ndani ya kikosi cha Singida Black Stars na anamfurahia kila mchezaji lakini ikitokea mchezaji mwenzake akamnyima nafasi ya wazi ya kufunga atamchukia kwasababu kiu yake ni kufunga.

Akizungumzia kasi yake ya ufungaji, Sowah anasema; “Hii ni kazi yangu na nina furaha kwa sasa na kiwango changu naamini naweza kufanya zaidi na kuisaidia timu yangu kumaliza katika nafasi ya tatu au ya pili kwenye msimamo wa ligi.”

Mbali na kuwa hatari langoni, Sowah anaonesha utulivu, uwezo wa kukaa eneo sahihi na kufunga kwa nafasi ndogo.