Msisimko wa namba, siku, wafungaji Dabi
MASHABIKI wa soka hasa wale wapenzi wa Simba na Yanga kwa sasa mioyo inawadunda kwa pupa, huku wakihesabu siku tu, kabla ya kuzishuhudia timu hizo zikishuka uwanjani katika pambano la kwanza la Dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026.
Timu hizo ambazo ni watani wa jadi zinatarajiwa kuvaana Machi Mosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika pambano la Ligi Kuu Bara baada ya mechi hiyo kuahirishwa kutoka Desemba 13 mwaka jana.
Tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya marudiano ya msimu uliopita iliyoahirishwa mara mbili kwa sababu zilizotokana na kutunishiana misuli kwa klabu hizo na kuyumba kwa Bodi ya Ligi (TPLB) iliyoahirisha kienyeji pambano la Machi 8 kisha kurudia tena Juni 15, safari hii ni kutokana na kuingiliana kwa ratiba za timu hizo katika mechi za kimataifa na kupigwa kwa AFCON 2025.
Fainali za AFCON 2025 zilizofanyika Morocco kati ya Desemba 21, 2025 na kumalizika Januari 18, mwaka huu Tanzania ilikuwa ni moja ya timu 24 zilizoshiriki na klabu hizo zilitoa wachezaji wengi waliotakiwa kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, lakini zote zimefuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Azam FC na Singida Black Stars.
Hili litakuwa ni pambano la 115 kwa timu hizo katika Ligi tangu mwaka 1965, huku likiwa ni la 11 ndani ya Machi , yakiwamo 10 ya Ligi Kuu na moja la michuano ya Kombe la Tusker (haipo kwa sasa).
Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo katika pambano la Machi, Yanga ndio wababe mbele ya Simba, kwani imeshinda michezo minne kati ya 10 ya Ligi Kuu tangu zilipoanza kukutana mwezi huo kuanzia mwaka 1968.
Simba yenyewe imeshinda mara moja tu katika mechi za Ligi Kuu, lakini ina ushindi mwingine wa fainali ya Kombe la Tusker, ambapo Yanga ililala kwa mabao 4-1 na kuibuka vurugu kubwa mbele ya aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia mwaka juzi.
Mechi nyingine tano baina ya timu hizo zilipokutana Machi, zimeisha kwa sare tofauti huku, Yanga ikivuna mabao mengi zaidi na watani wao, kwani katika mechi 10 za Ligi za mwezi huo imevuna mabao tisa, wakati Simba imefunga matano tu.
Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza Machi 30, 1968 na Yanga kushinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na Kitwana Manara 'Popat' kabla ya kuja kukutana tena Machi 3, 1969 likiwa ni pambano la pili katika mwezi huo.
Mchezo huo haukumalizika baada ya Simba kuugomea na Yanga kupewa ushindi wa mezani wa pointi mbili na mabao mawili na timu hizo zilikaa hadi mwaka 1984 zilipokutana kwa mara ya tatu ndani ya Machi.
Pambano hilo la Ligi, lilichezwa Machi 10 na liliisha kwa sare ya bao 1-1, Simba ikitangulia kwa bao la penalti iliyopigwa na kipa, Idd Pazi 'Father' aliyekuwa kipa wa kwanza kufunga katika Dabi ya Kariakoo kabla ya Juma Kaseja kuja kuilipa Mei 6, 2012 wakati Simba ikiizima Yanga kwa mabao 5-0. Bao la kusawazisha la Yanga katika mechi hiyo ya Machi 10, 1984 liliwekwa wavuni na Omar Hussein 'Keegan' dakika ya 72 na kuiepushia Yanga kipigo ndani ya Machi.
Miaka miwili baadae timu hizo zilikutana tena ndani ya Machi, mechi ilipigwa Machi 15, 1986 na kuisha pia kwa sare ya 1-1, Simba ikitangulia kwa bao la John Hassan Douglas dakika ya 20 na Abeid Mziba 'Tekero' akaichomolea Yanga dakika ya 44.
Mwaka 1993, ikiwa ni miaka saba tangu zilipokutana kwa mara ya mwisho, Yanga iliibuka tena kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Machi 27, mabao yote mawili ya Yanga yakifungwa na Said Mwamba 'Kizota' dakika ta 47 na 57 kabla ya Edward Chumila 'Eddo Boy' kufunga la kufutia macho la Simba dk ya 75.
Simba na Yanga zilikutana tena Machi 18, 1995 na Machi 26, 2006 na mara zote zilishindwa kutoa mshindi kwa kutoka suluhu mara zote, kisha Machi 5, 2011 timu hizi zilikutana tena katika mchezo wa Ligi Kuu na kutoka sare ya 1-1.
Hii ndio mechi ndio iliyotajwa kuzindua mfumo wa VAR, kwani Yanga ilitangulia kwa bao la dakika ya 59 kupitia beki wa kushoto, Stephano Mwasyika kisha Mussa Hassan Mgosi aliichomolea Simba dakika ya 73 kwa kichwa mpira uliogonga besela na kudondokea ndani, lakini bado lilikataliwa na mwamuzi, Oden Mbaga.
Wachezaji wa Simba na mashabiki walilalamikia uamuzi wa Mbaga na kumtaka aangalie marejeo kupitia televisheni iliyopo uwanjani na kubaini ni kweli mpira uligongea ndani kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga na kulikubali bao hilo la Mgosi na kufanya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.
Mechi ya tisa kwa timu hizo kukutana Machi, ilikuwa Siku ya Wanawake Duniani, yaani Machi 8 2015 likiwa la kwanza kwao kukutana katika siku kama hiyo na Emmanuel Okwi alifunga bao kali la mbali, kabla ya Yanga kujibu Machi 8, 2020 kwa bao la friikikii ya Bernard Morrison'BM3'.
Pambano pekee la Machi lililo la Ligi Kuu ni lile la fainali ya Kombe la Tusker iliyopigwa Machi 31, 2002 na Yanga kulala kwa mabao 4-1, yaliyofungwa na Mkenya Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emmanuel Gabriel dk. 83., huku Sekilojo Chambua akifunga bao la kufutia machozi la Yanga dk 16.
Mechi hii nusura ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao la tatu likitokana na kuutengeza kwa mkono kabla ua kumtungia kipa Peter Manyika (sasa marehemu).
Kwa ujumla katika mechi zote 11 za mashindano tofauti ndani ya Machi ikiwamo ile ya Kombe la Tusker, bado Yanga ina mabao mengi ikiwa na 10 dhidi ya tisa ya Simba, kuonyesha Vijana wa Jangwani ina kismati na mwezi huo wa Machi.
Hata hivyo, kwa aina ya vikosi na makocha wapya ilizonazo timu hizo ni wazi safari hii kutakuwa na kazi kubwa katika vita ya kuwania pointi tatu za mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ya kwanza kwa msimu huu. Simba ina kocha mpya, Steve Barker kutoka Afrika Kusini na Yanga ina Pedro Goncalves raia wa Ureno ambao hawajawahi kukutana kabisa, kwani mechi ya Ngao ya Jamii ambapo Simba ilipasuka kwa bao 1-0 la Pacome Zouzoua, Simba ilikuwa na Fadlu Davids aliyerejea Raja Casablanca ya Morocco na Yanga ikiwa na Romain Folz aliyetiumuliwa Jangwani.
Kocha Barker na Simba ina kazi ya kuzima mzimu wa vipigo mfululizo kwa timu hiyo mbele ya Yanga, kwani tangu mwaka 2023 haijawahi kupata ushindi iwe katika Ligi Kuu au Ngao ya Jamii.
Simba imepoteza mechi sita mfululizo ikiwa ni rekodi kwa sasa kwa timu hizo zenye upinzani wa jadi, kwani imefungwa mara nne katika Ligi Kuu na nyingine mbili za Ngao ya Jamii, kiasi cha kuwapa unyonge mashabiki na wapenzi wa Wekundu wa Msimbazi hao mbele ya wenzao wa Yanga.
Utamu ni kwamba klabu zote zina mashine mpya vikosini, Yanga ikiongeza majembe kama Allan Okello, Aurelio Laurindo 'Depu', Emmanuel Mwanengo, Mohammed Camara na Buba Jammeh, huku Simba ikiwa na kipa Gibrilla Kassalli, Libasse Gueye, Clatous Chama, Ismael Toure, Nickson Kibabage, Anicet Oura na Inno Jopsin Loemba.
Nani atakayeibuka na ushindi katika mechi hii ya 115 za watani katika Ligi Kuu Bara na nani atakayemaliza ubishi wa mwezi huu Machi ? Ngoja tuone!
MECHI ZA MACHI
1) Mar 30, 1968 (Jumamosi)
Yanga 1-0 Sunderland
MFUNGAJI: Kitwana Manara dk. 28.
2) Mar 3, 1969 (Jumatatu)
Yanga v Sunderland
(Yanga ilipewa pointi za chee na ushindi wa mabao 2-0, baada ya Sunderland kugoma kuingia uwanjani).
3) Mar 10, 1984 (Jumamosi)
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 72.
Simba: Idd Pazi kwa penalti dk 20.
4) Mar 15, 1986 (Jumamosi)
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 44
Simba: John Hassan Douglas dk. 20.
5) Mar 27, 1993 (Jumamosi)
Yanga 2-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Said Mwamba Kizota dk. 47 na 57
Simba: Edward Chumila dk. 75.
6) Mar 18, 1995 (Jumamosi)
Simba 0-0 Yanga
7) Mar 26, 2006 (Jumapili)
Simba 0-0 Yanga.
8) Mar 5, 2011 (Jumamosi)
Simba 1-1 Yanga
WAFUNGAJI:
YANGA: Stefano Mwasyika (penalti) dk 59.
SIMBA: Mussa Mgosi dk 73.
(Refa Oden Mbaga alizua tafrani uwanjani, kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidia wake namba moja).
9) Mar 8, 2015 (Jumapili)
Simba 1-0 Yanga
MFUNGAJI: Emmanuel Okwi Dk 52
10) Mar 08, 2020 (Jumamosi)
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Bernard Morrison 44'
11) Mar 31, 2002 (Jumapili)
Simba 4-1 Yanga
WAFUNGAJI:
SIMBA: Mark Sirengo dk 3 na 76, Madaraka Selemani dk 32 na Emmanuel Gabriel dk. 83.
YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.
Msimamo mechi za watani tangu 1965-2025
P W D L F A PTS
YANGA 114 42 40 32 123 105 166
SIMBA 114 32 40 42 105 123 136