Prime
MO BANKA: Tatizo lililonitesa lilianzia kwenye soksi
JANA Ijumaa tulianza makala iliyotokana na mahojiano maalumu na kiungo wa zamani wa Yanga, Namungo na Taifa Stars, Mohammed Issa ‘MO Banka’ aliyekiri bangi alizokuwa akizitumia zilikaribia kumvurugia kipaji alichonacho cha soka.
Pia alifunguka kuhusu tatizo la maradhi yaliyompata ghafla na kumfanya aweweseke na leo tunaendelea na kiungo huyo fundi wa boli akifichua shida nzima ilianzia wapi hadi kufikia kuhangaika kabla ya kupata matibabu ya kumrejesha katika hali nzuri. Endelea naye...!
SOKSI CHANZO CHA YOTE
Pamoja na kwamba Banka amekana kuthibitisha sababu ya shida zake katika maswali mengi aliyoulizwa na Mwanaspoti, kiungo huyo amejikuta akifunguka kuwa akiwa kwenye mihangaiko ya kusaka matibabu shida iliyokuwa ikimtesa, soksi zilitajwa.
“Nikiwa huko natibiwa, mtaalam alinikumbusha kitu ambacho nilishakisahau kuhusu upotevu wa kipande changu cha soksi ndipo nilipovuta picha na kukumbuka mambo ya nyuma, ni kweli nilishawahi kuibiwa soksi,” anasema na kuongeza:
“Nakumbuka alinitajia siku hadi niliyoumia na akaniambia namna ambavyo nilikuwa natafuta soksi yangu ambayo sikuwahi kuipata hadi sasa nikamwambia kweli akasema tena ni kipande nikamjibu sahihi kwa sababu mimi napenda kuzikata zinakera ukivaa nzima ndani ya kiatu zinateleza.”
Banka anasema anakumbuka aliyechukua soksi, lakini hakuwahi kudhani kama angepatwa na lolote baya.
PACHA NA TSHISHIMBI
“Kipindi hicho nacheza Yanga ilikuwa na viungo wengi kama Balama Mapinduzi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Papy Tshishimbi, Abdulaziz Makame akaja na Haruna Niyonzima mwishoni mwishoni nilikuwa nawapenda wachezaji wote na kipindi hicho ndio Yanga ya bakuli maisha yalikuwa yanasonga,” anasema na kuongeza;
“Kwa wachezaji hao wote nilikuwa navutiwa zaidi nikipangwa na Tshishimbi nilikuwa nafurahi sana kama unakumbuka kulikuwa na kampa kampa tena hiyo ilikuwa bora sana kwangu.” anasema kiungo huyo ambaye alizungumzia namna wanawake walivyokuwa wanamtongoza.
Banka anasema Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji bora aliowahi kucheza nao alikuwa anajisikia huru zaidi na walikuwa wametengeneza pacha nzuri sana.
AMTAJA KOCHA JANZA
Imezoeleka sana na umefanywa kama utaratibu ni nadra sana wachezaji kutoka timu nje ya Simba, Yanga na Azam FC kuitwa timu ya taifa ata wawe na ubora kama anavyothibitisha Banka baada ya kupata nafasi ya kuitwa akiwa na Namungo.
“Nakumbuka siku ya kwanza kufanya mazoezi nikiwa na Namungo baada ya kutoka majeruhi ilikuwa chini ya kocha mpya baada ya Hemed Morocco kutoka kumalizana na uongozi na timu kuachiwa Hanoor Janza raia wa Zambia nilikwa nimetoka Zanzibar kujiuguza kocha huyo aliponiona alisimamisha mazoezi,” anasema na kuongeza:
“Aliuliza kwa aliyekuwa msaidizi Jamhuri Kihwelo kipindi hicho mimi ni nani akamjibu ni mchezaji wa timu hiyo nilikuwa majeruhi nimerudi akahoji nimetoka nchi gani akaambiwa mimi ni mtanzania ni mzariwa wa Zanzibar alivutiwa na uwezo wangu na kunipanga kuwa sehemu ya timu ambayo itacheza mechi inayofuata huku akimuondoa Lucas Kikoti.”
Anasema hakutarajia hilo kwani aliamini ametoka kujiuguza atapata muda wa kupumzika usiku daktari wa timu alimuhakikishia kuwa atakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya siku nne na ametoka majeruhi kwa miezi minne bila kucheza.
“Kocha anasema hakuna mchezaji kama mimi ligi kuu ameona kipaji kikubwa sistahili kucheza ligi ya ndani anatamani kuona nacheza ulaya hivyo tangu apo alikuwa ananikubaki sana nakumbuka kuna muda alipewa timu ya taifa kwa muda na Stars tulikuwa tunaenda kucheza Burundi aliniita nikiwa Namungo,” anasema.
YANGA IMENIPA NYUMBA
Licha ya kupita Yanga ambayo ilikuwa na changamoto ya fedha wakipitisha mabakuli kwa mashabiki zao Banka ameweka wazi kuwa timu hiyo imembadilishia maisha ameweza kumiliki nyumba.
“Yanga imenifanya najulikana, Yanga imenipa jina kubwa Mtibwa Sugar pia ilinifanya niwe hivyo lakini Yanga ni timu kubwa tungekuwa Hispania tunge ifananisha na Barcelona hivyo najivunia kupita timu hiyo,” anasema na kuongeza;
“Yanga ni timu ambayo kila mchezaji anandoto ya kupita hapo kucheza ili aweze kutengeneza maisha yake hivyo siwezi kuisahau kuna kitu nimekitengeneza kwenye maisha yangu.”
NIYONZIMA, CHAMA
Wachezaji wengi wa kigeni wanaocheza eneo la kiungo mshambuliaji wamepita Tanzania na kucheza ligi kuu lakini Banka humwambii kitu kuhusu Haruna Niyonzima na Clatous Chama kama anavyofunguka.
“Ni kweli wachezaji wengi bora wamecheza ligi kuu kutoka mataifa mbali mbali lakini mimi kipindi nacheza nilikuwa namkubali sana Haruna Niyonzima ni kuongo fundi sana anaeufanya mpira kuwa rahisi,” anasema na kuongeza;
“Kwa sasa kuna mtu anaitwa Chama anaujua sana mpira namkubali sana anajua kucheza sijui nimuelezee vipi ila kauli yangu ni kwamba anajua sana kucheza mpira.” Anasema Banka ambaye ameweka wazi kuwa ameacha starehe zote alizokuwa anatumia hapo awali saizi ni swala, TV na kupumzika sana.
PACOME, AZIK KI
Ukiondoa kiungo huyo kubainisha kuwa na mapenzi makubwa ya kiuchezaji na Niyonzima na Chama amewataja wachezaji wengine bora kwenye eneo hilo kuwa ni Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.
“Kwenye eneo ninalocheza kwa sasa nimesema navutiwa na Chama lakini kikosini nikiwa ma Pacome na Aziz Ki ntaanza na Pacome kwa sababu ni mchezaji mwenye kasi na mtu wa maamuzi ya haraka.” anasema na kuongeza;
“Aziz Ki ni mchezaji mzuri pia lakini hana kasi licha ya kuwa vizuri kwenye kufumania nyavu akiwa nje ya 18 anauwezo kwa Pacome anaweza kuniofa vitu vingi uwanjani ni mchezaji ambaye anatumika pembeni na kati.” anasema.
AKATAA SOKA, ACHAGUA KUFUGA
Kutokana na soka la Zanzibar kushindwa kuendelea Banka anasema aliamua kuachana na mpira na kuamua kuwekeza nguvu kwenye ufugaji wa ng’ombe hadi kufikia mahala alikuwa anaitwa mmasai.
“Sola la Zanzibar halikui kwa sababu ya kukosa uwekezaji na wadhamini hivyo unajikuta unacheza kwa mapenzi tu hakuna unachoingiza hivyo baada ya kuona hivyo niliamua kuachana na mpira na kuwekeza nguvu kwenye ufugaji,” anasema na kuongeza;
“Nilikuwa nafuga ng’ombe nilikuza nao wanee kwa Zanzibar kufikia idadi hiyo miaka hiyo ilikuwa ni utajiri nikabatizwa na jina la mmasai na ng’ombe hao walikuwa wananiingizia fedha kwani pia walikuwa wanatumika kama usafiri kwa kubeba mizigo kama guta.”
Banka anasema alikuwa akitoka na ng’ombe wake anauwezo wa kurudi ntumbani na fedha nyingi tofauti na akienda kwenye mpira lakini mzazi wake alikuwa hapendezwi na ufugaji kwani alikuwa anaamini katika kipaji alichokuwa nacho.
“Baba alikuwa hapendi lakini hawezi kunishawishi na wadau wengi wa mpira walikuwa wanavutiwa na uwezo wangu nikijito mara moja moja kucheza na kuja nyumbani kumshawishi baba aniruhusu nirudi kucheza mpira.”
MILION MOJA ILIMRUDISHA UWANJANI
“Kuna tajiri mmoja alikuwa shirika la umeme alikuwa na timu yake daraja la pili alinishawishi nirudi uwanjani sikumuelewa akaniomba nimpeleke nyumbani nikaenda naye nilivyofika baba akaniuliza nimefanya kesi gani akaambiwa hamna;
“Nikamwambia baba msikilize amekuja kwa ajili yako ndio akaanza kujieleza kuwa yeye anatimu ya daraja la pili hivyo ananitaka nikaichezee timu hiyo baba alisema huyo hataki mpira nimeshindwa mshawishi sasa naomba tulubaliane mimi huyo nataka aje kwenye timu yangu kila akija mazoezini tu namlipa elf kumi na hapa namsainisha mkataba wa milion moja;
“Baba akasema haya unataka nini sasa utacheza akamtuma huyo mtu akachukue fomu kwa ajili ya kunisainisha baada ya kutoka tu kufuata nilipewa maneno aliporudi ikanibidi nisaini mkataba baada ya mechi sita tu timu zote za ligi kuu zilionyesha nia ya kunihitaji.” anasema Banka ambaye amebainisha kuwa baada ya kukubali kucheza baba yake alipika pilau kwa furaha.
Banka anasema baada ya kufanya vizuri alipata timu ya ligi kuu kwa kusaini mkataba wa miezi sita timi ya Chuoni ambaya hata hivyo hakuhudumu nayo kwani alirudi kwenye shida ya kulipwa elfu mbili baada ya mazoezi na kuamua kurudi kwenye ufugaji tena.
“Niligundua kuwa yule jamaa alikuwa ananishawishi kurudi kwenye mpira kwa kunipa fedha nyingi ambazo mtu mwingine hawezi kupata kwani nilishangaa ligi kuu nalipwa elfu mbili bila ya mshahara wakati daraja la pili nilikuwa napata fedha nyingi,” anasema na kuongeza:
“Chuoni kipindi hicho nilikuwa na marehemu Ibrahim Rajab ‘Jeba’ Mungu aendelee kuilaza roho yake mahala pema peponi alikuwa mchezaji mzuri sana na alikuwa na moyo wa kipekee.”
JEBA ALIVYOMPELEKA BARA
“Nakumbuka tulikuwa tunacheza mechi ya kirafiki kwa timu za mtaani Jeba alikuwa timu pinzani nilimsumbua sana kwenye hiyo mechi baada ya mechi aliniuliza unacheza timu gani nikamwambia nilikuwa nacheza Chuoni lakini sijaenda nina mwaka hadi sasa,” anasema na kuongeza;
“Akasema wewe unakipaji sana na sio cha kucheza Zanzibar mimi nacheza Mtibwa Sugar nilikupa nafasi ya kufanya majaribio utakuja sokutaka kukataa nikakubali akasema chukua namba yangu nikachukua baada ya mwezi mmoja nipigiwa simu na namba ngeni akajitambulisha na kuniambia boss wake kakubali.”
Banka anasema akamwambia anatakiwa kusafiri kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio akaanza kutafuta sababu mara hana viatu, bukta alishaacha mpira hivyo sio mchezaji tena Jeba akamuuliza anavaa viatu size ngapi akamjibu tisa akamjubu ana viatu pea nane size hiyo.
“Kwa iyo kesho boti ya saa tisa unatakiwa uanze safari nakutumia tiketi ya boti akatuma na laki moja hivyo mimi nikasafiri kama nilivyo nimefika Itumbi kina Shaban Nditi ndio mastaa kocha Salum Mayanga na Zuberi Katwila tulifanya mazoezi tulikuwa wengi .” anasema na kuongeza:
“Kipindi hicho Mtibwa imewauza Mzamiru Yasin, Mohammed Ibrahim na Shiza Kichuya hivyo wanatafuta wa kuziba nafasi zao tayari alikuwa amepatikana mmoja Rashid Mandawa mshambuliaji hivyo tukapita mimi na Stamil Mbonde tukasajiliwa.”
Banka anasema baada ya hapo walirudi Manungu alikutana na changamoto kocha hamkubali mechi sita anakalia mbao muda mwingine anakaa jukwaani huku eneo hilo akicheza Ally Makalani mechi ya Saba walikuwa wanacheza na Simba.
“Siku hiyo nikasema sikubali nikaanza mazoezi kutoka Manungu hadi tuliani nakimbia asubuhi nimefunga machupa nakimbia siku ya mechi nilikuwa sehemu ya kikosi ila nilianzia benchi nakumbuka kipindi cha kwanza tulikuwa tumefungwa bao moja kocha akageuka nyuma benchi akaniona akaniita nipashe,” anasema na kuongeza;
“Nilicheza kwenye huo mchezo kwa haisa na kiwango kikubwa sana sitakaa nikasahau bosi Jamal Baysar baada ya mpira kuusha alikuja vyumbani na kuhoji kwa nini situmiki akanipa laki moja kama zawadi akinitaja kuwa mchezaji bora wachezo.”
KAZIMOTO ALIMHAKIISHIA NAMBA
“Nakumbuka Mwinyi Kazimoto baada ya mechi alimfuata Henry Joseph Shindika akamuuliza kwanini sianzi kwenye kikosi chetu na nina kipaji kikubwa naweza kuisaidia timu hakuishia hapo,” anasema na kuongeza;
“Alinihoji kwa kuniuliza kama ni mzanzibar nikamjibu ndio akasema ndio maana una kipaji kikubwa timu inatakiwa ikuchezeshe sana kama wanataka matokeo hapo ndio ukawa mwanzo wangu wa kucheza mpaka kuna muda naumia naambiwa ntacheza wananitegemea.”
Banka anasema ilifika muda alikuwa anaamua kuwajaribu na kuwaambia hawezi kucheza mechi wanampeleka hadi kwa waganga ili tu aweze kucheza huku lengo lake likiwa ni kutaka kuona umuhimu wake kikosini.
“Kuna muda mazoezini nakaa na muambia kocha nina henka anaanza washakuroga hao hakuna anaekubali wewe uende timu ya taifa ucheze urudi uingie moja kwa moja kikosini twende kwa mganga naenda kweli mganga ananichanja anaweka dawa siku ya pili naenda mazoezi nafanya vizuri anabaini kuwa kweli nimerogwa,”
“Anasema bila Jeba muda huu sijui angekuwa wapi kwani saizi ufugaji wa ng’ombe umekatazwa na tayari kumeshakuwa mjini kuna toyo tofauti na mwanzo tulikuwa tunatumia ng’ombe.”
TOFAUTI BARA, ZANZIBAR
“Kuna utofauti mkubwa sana wa ligi ya bara na Zanzibar kuanzia uwekezaji hadi ugumu wa ligi Bara ligi yao ni ngumu na inatoa changamoto ya ushindani tofauti na Zanzibar.”
“Tanzania Bara kuna mchanganyiko wa wachezaji wengi kutoka mataifa mbali mbali na ushindani wake ni mkubwa tofauti na Zanzibar ambapo utimamu wa mwili kwa wachezaji upo chini sana lakini kwenye suala la kuchezea mpira mtu ata aamshwe usiku wa manane hakuna mtu wa kupora mpira.”
Banka anafunguka sababu ya kukosa utimamu kwa wachezaji kuwa ni kutokana na mazingira ya ligi ya Zanzibar kuachia wachezaji kurudi majumbani tofauti na bara ambapo wanakaa kambi.
“Zanzibar hakuna muendelezo kwanichezaji anatoka mazoezi anarudi nyumbani anakutana na kazi nyingine ambayo inamfanya atoe alichokiingiza katika mazoezi wakati bara mtu akitoka mazoezi anakaa kambini kujiweka tayari na mecho lazima awe fiti.” anasema Banka ambaye ameweka wazi kuwa mbali na kufuga ng’ombe amefanya biashara ya kuuza vyombo na kuuza machuma akitoka mazoezi anakutana na tajiri wa biashara ya vyombo anampa kazi ya kuzungusha mitaani kwa ajili ya kuuza.
Anasema Zanzibar vipaji ni vingi sana kwa sababu kule watoto wengi wanakua wakijifunza mpira kutokana na kuzungukwa na viwanja vingi mtaani na wachezaji wengi wanakuzwa katika mazingira ya mpira wakiwa na umri mdogo.
ATAMANI TIMU KAMA SINGIDA
Licha ya kuto kucheza kwa miaka miwili na nusu kiungo huyo amesema amekuwa akifuatilia mpira na kubaini kuwa umekuwa ukikua siku hadi siku kutokana na mabadiliko makubwa yaliyopo kuanzia uwekezaji hadi sajili bora zinazofanyika.
“Ligi inakua msimu hadi msimu kuna ushindani unaongezeka mfano uwepo wa Singida Black Stars unaleta changamoto ya ushindani kwa timu kama Simba na Yanga ambazo ilizoeleka kila msimu asipokuwa bingwa huyu basi yule hivyo kama kutakuwa na ongezeko la timu bora kama Singida basi ubora wa ligi utaendekea kupaa,” anasema na kuongeza;
“Ukiondoa hilo pia uwekezaji kwenye klabu na sajili bora zimeongeza chachu ya ukuaji na ushindani kwa wachezaji wa ndani na kimataifa sasa hivi sio rahisi mgeni kumng’oa mzawa bila ushindani.” anasema Banka.
Anasema zikipatikana timu tano kama Singida ambazo zitatoa ushindani basi nchi itakuwa na timu bora ya taifa ‘Taifa Stars’ kutokana na ushindani utakaokuwepo.
MUDATHIR, FEI TOTO
Ukiondoa nyota wa kigeni aliowataja kwa ubora Banka hakusita kutaja nyota wa ndani ambao anawakubali kutokana na ubora wao huku akizungumzia namba sahihi ambazo wanafaa kuzicheza.
“Wazawa wapo wengi bora na wanafanya vizuri nakubaliana na uwezo wao kuna Mudathir Yahya na Feisal Salum ni wachezaji wazuri sana wana uwezo mkubwa hawa kwenye timu yangu wote nawapanga siachi mtu benchi,” anasema na kuongeza;
“Mudathir anacheza nane au sita kwa sababu ni namba zote ambazo anauwezo mkubwa wa kucheza vizuri alafu fei toto namchezesha nane au kumi najua atanipa vitu sahihi.”
Banka anasema nafasi hizo kwa nyota hao walikuwa wanazicheza hata timu ya taifa ya Zanzinar ‘Zanzibar Heroes’ kama Muda akianza sita basi fei toto anacheza nane hivyo anaamini wakicheza pamoja wanafanya kitu kizuri zaidi.
AMKINGIA KIFUA BACCA
Imeripotiwa kuwa Ibrahim Hamad ‘Bacca’ amefungiwa mechi tano kuto kucheza ligi kuu baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Mbeya City kwenye mchezo wa ligi timu yake ikiambulia suluhu uwanja wa Sokoine Mbeya hilo limemuibua Banka ambaye amesema beki huyo hajatendewa haki.
“Bacca ni beki bora anatakiwa kuendeleza ubora wake lakini kwa kilichofanyika hivi karibuni kwa kumfungia mechi tano sijui nisemeje sijui niseme kaonewa ila acha niwaachie wenyewe lakini kwa mchezaji sio kitu kizuri hasa kwa Yanga ya sasa,” anasema na kuongeza;
“Sio kizuri kwa sababu kuna mtu anaitamani namba yake anamuachia kwa mechi tano labda ashindwe mwenyewe yani uniachie mimi mechi tano urudi utegemee kuchukua namba sio kweli labda niwe sina kiwango.”
Banka anasema ni wakati wa mchezaji ambaye hana namba kumshawishi kocha kuchukukua namba ya Bacca ambaye ni mchezaji bora wa timu ya Yanga lakini pia timu ya taifa adhabu ni kubwa sana waangalie namna nyingine.
UFAFANUZI KUHUSU TATUU
Nyota huyo wa zamani wa Yanga amechora tatuu tatu mkononi moja begani amechora namba nane, mkononi amechora nyavu na mkono mwingine amechora mawingu na nyota ameelezea maana yake.
“Unajua vitu vingine vinatokea tu na unajikuta unaingia mtego wa ibirisi ndio kama hivi licha ya kuwa muislam na kupita madrasa nafahamu hii haitakiwi lakini nimechora na naenda msikitini kwa kujificha zisionekane uzu natia nyumbani,” anasema na kuongeza;
“Tatu mbili zote nimetumia laki nne moja mbili na hamsini nyingine laki na nusu hii ya nyavu kwa sababu mimi ni mtu wa kufunga hivyo nikaamua kuchura hivi lakini hii nyingine ya mawingi na nyota inamaana ya ustaa mimi ni bland.” anasema.
TUKIO GUMU LA SOKA
Kwenye soka kuna wakati wa raha na huzuni kama anavyothibitisha Banka kwa kutaja tukio lake gumu alilowahi kukutana nalo ukiondoa kuugua ugonjwa usio julikana.
“Kuna siku tulienda Pemba kwenye bonanza kunaitwa Bungi kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa kumi na huko haina kupumzika unatoka baada ya dakika unaingia kucheza,” amasema na kuongeza;
“Baada ya kumaliza huochezo tulipewa elfu tano nilichoka sana nilikuwa hui na tulienda tulikuwa hatufahamu tunapewa bei gani na matarajio yalikuwa elfu 20.” amasema.
Banka anasema katika tulio lingine alialikwa kucheza mechi bingwa alipewa kiloba cha kilo 20 za mchele hili tukio pia hata kaa akasahau licha ya kuambulia sh elfu 30.
“Siku hiyo pia tulipewaaembe na mafenesi kama zawadi tukirudi nyumbani ni sawa na mtu aende Lindi lazima atarudi na korosho.” anasema Banka ambaye ameweka wazi kuwa usajili wake mkubwa mbali na milion moja alishawahi kusajiliwa timu ya vijana kwa kupewa baiskeli na viatu vya mpira na ndio ulikuwa usajili mkubwa kikosi cha Alizona ndio ilikuwa timu yenye fedha.