MJUAJI: Rekodi za mabao mengi Simba na Yanga

HISTORIA inaendelea kuandikwa. Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika mchezo wa ‘Dabi ya Kariakoo’. Katika hali isiyotarajiwa na wengi, Yanga iliandika historia nyingine baada ya miaka 55.
Inaweza kuchukua muda mrefu kwa kitendo kama hiki kujitokeza tena kutokana na historia za timu hizo zenye utani wa jadi.
Mechi hii imewachanganya sana mashabiki na wanachama wa Simba kwa kuwa hawakutarajia kufungwa idadi hiyo ya mabao. Wengi wanaaamini kuna mkono wa mtu na haitoshi tu kwa uongozi kumfukuza Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Simba wanaamini hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa kutokana na kipigo hicho ambacho kimechafua rekodi ya kuwafunga watani wao idadi kubwa ya mabao.
Mabao ya Yanga Jumapili iliyopita yalifungwa na Maxi Nzengeli (mawili), Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua waliofunga moja kila mmoja.
RAGE ALIITISHA KIKAO
Aprili 16, 1983 Simba ilifungwa mabao 3-1 na Yanga na kumfanya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Simba wakati huo, Ismail Aden Rage kuitisha mkutano wa dharula kesho yake kujadili kipigo hicho. Simba ilifungwa ikiwa na Kocha Mbrazili, Nader Silva. Ilikuwa ni baada ya mechi ya kwanza ya Februari 10, 1983 ambayo Simba ikiwa inatoka Brazil kuisha kwa sare tasa.
Historia inaonyesha, Yanga ilikuwa timu ya kwanza kuifunga Simba mabao mengi Juni Mosi 1968. Katika mchezo huo Yanga ilifunga Sunderland (Simba) mabao 5-0.
Yalikuwa ni mabao yaliyofungwa na Maulid Dilunga (mawili) dakika 18 kwa penalti na dakika 43. Mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika 54 na 89, Kitwana Manara alifunga dakika 86.
SIMBA YALIPA KISASI
Yanga iliingia kwenye mgogoro mkubwa sana uliofukuta klabuni hapo na kusababisha timu hiyo kugawanyika pande mbili mwaka 1976. Msimu uliofuata Julai 19, 1977, Simba ililipa kisasi kwa kuifunga mabao 6-0. Hapa ndipo ilipozaliwa ‘hat trick’ ya kwanza katika Dabi ya Kariakoo iliyofungwa na Abdallah Seif ‘ Kibadeni’ King Mputa. Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masumenti’ na lingine la kujifunga la beki wa Yanga, Suleiman Jongo.
Simba iliendeleza ubabe wa kupachika mabao mengi baada ya Julai 2, 1994 kuifunga Yanga mabao 4-1. Mabao ya Simba yalifungwa na beki George Magere Masatu, lile la Yanga lilifungwa na Constantine Kimanda. Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Athumani Abdallah ‘China’, Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’ na Dua Said.
UBABE WA SIMBA
Bado Simba iliendeleza ubabe mbele ya Yanga baada ya kushinda katika mchezo wa fainali za Kombe la Tusker mwaka Machi 31, 2022 kwa mabao 4-1.
Mabao ya Simba yalifungwa na Mark Sirengo dakika 3 na 76, huku mengine yakifungwa na Madaraka Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio dakika 32 na Emmanuel Gabriel ‘Batgoal’ dakika 83, huku bao la Yanga lililokuwa la kusawazisha kabla ya Simba kuongeza hayo mengine, lilifungwa na kiungo Sekelojo Chambua.
Mechi hii nusura ivunjike baada ya Madaraka kutuhumiwa kufunga bao alilotengeneza kwa mkono na kuzua ghasia uwanjani, kiasi cha aliyekuwa Rais wa Yanga, Tarimba Abbas kuinuka jukwaani na kuwaonyesha ishara wachezaji wa timu hiyo kutoka uwanjani. Hata hivyo Mwamuzi Omar Abdulkadir alisubiri ghasia zitulie kwa msaada ya FFU na kuendelea na mchezo, japo Tarimba aliondoka uwanjani na kujikuta akifungiwa na Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF).
MECHI YA NCHUNGA
Kama haitoshi, Simba iliifunga tena Yanga mabao mengi kwenye mchezo mmoja Mei 6, 2012 baada ya kuitandika mabao 5-0. Mechi hii ilikuwa na maneno mengi nyuma yake, ikidaiwa wachezaji wa Yanga walicheza kwa maelekezo maalumu baada ya mwenyekiti wa Yanga wakati huo, Llody Nchunga kugoma kuachia ngazi.
Mara baada ya kichapo hicho baadhi ya mashabiki na wanachama wa Yanga waliandamana hadi nyumbani kwa mwenyekiti huyo na kutishia kuichoma nyumba yake moto.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Emmnanuel Okwi dakika 1 na 62. Mengine yalifungwa na Felix Sunzu dakika 56 (penalti), Juma Kaseja (dakika 67, penalti) na Patrick Mafisango (dakika 72, penalti).
MECHI YA MABAO SABA
Hii hapa mechi nyingine ya Kariakoo Dabi iliyokuwa na mabao mengi kwenye mchezo mmoja. Ilikuwa Aprili 18, 2010 baada ya Simba kushinda kwa mabao 4-3. Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Selemani dakika 3, Mussa Hassan Mgosi dakika 53 na 74 na la ushindi likifungwa na Hilary Echesa dakika 90+
Mabao ya Yanga yalifungwa na Athuman Idd ‘Chuji’ dakika 30 na Jerry Tegete dakika 69 na 89. Mechi ilikuwa na upinzani mkali kwelikweli.
MARA YA MWISHO
Kipigo kingine kikubwa ambacho Yanga ilikipokea kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ilikuwa ni Julai 13, 2020 katika nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation. Yanga ilikubali kuchapwa mabao 4-1.
Mabao ya Simba yalifungwa na Fraga Viera katika dakika 20, Clatous Chama dakika 49, Luis Miquisson dakika 52 na bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ dakika 70 na Mzamiru Yassin dakika 87 alifunga la nne .
MABAO MANANE
Katika historia ya Simba na Yanga, hii ndiyo mechi iliyozalisha mabao mengi zaidi kwenye mechi moja. Jumla la mabao manane yalifungwa kwenye mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Timu hizo zilifungana 4-4. Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Edibilly Lunyamila, Mustafa Hoza ( beki wa Simba alijifunga), Said Mwamba ‘Kizota’ na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’. Mabao ya Simba yalifungwa na Thomas Kipese, Ahmed Mwinyimkuu, Dua Said alifunga mabao mawili.
Oktoba 20, 2013 ilishuhudiwa Dabi ya Kariakoo ya ajabu Simba ilitoa sare ya kishujaa ya 3-3 katika Uwanja wa Taifa (Benjamin Mkapa). Mabao ya Yanga yaliyofungwa na Mrisho Ngassa dakika 14, Hamis Kiiza dakika 35 na 45. Kipindi cha pili kilikuwa cha Simba ilipoanza kusawazisha mabao yaliyofungwa na Betram Mombeki dakika 55, Joseph Owino dakika 57 na Girbert Kaze dakika 83.