Mbuna atoa siri ya benchi Yanga

FRED Mbuna ni miongoni mwa majina yaliyotamba ndani ya Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ni katika mastaa ambao wamekaa ndani ya kikosi hicho kwa muda mrefu na hata kuondoka waliondoka kwa heshima.
Kuna muda alikuwa hana namba kwenye kikosi cha kwanza kwa muda mrefu. Namba yake ilikuwa pale kwenye benchi pembeni kidogo ya makocha wa wakati huo.
Kiraka huyo mwenye miaka 44 ambaye sasa yupo kwenye benchi la ufundi la timu ya vijana ya Yanga amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam.
Lakini alianza na ishu ya kukaa benchi.
NAHODHA KUANZIA BENCHI
Mbuna anaeleza kwa mara ya kwanza sababu ya kuanzia benchi, ilitokana ni aina ya majukumu maalumu aliyokuwa anakabidhiwa na makocha, kuhakikisha timu inamaliza dakika 90 salama.
Jambo kubwa alilokuwa analifanya ni kusoma kila anachofanya mchezaji wa Yanga uwanjani na mapungufu ya wapinzani wao, ili akiingia mabadiliko yazae matunda.
Anashangazwa na baadhi ya wachezaji na wadau kudhani wanaoanzia benchi viwango vyao vimeshuka, jambo analopingana nalo, akiwapa elimu ya umuhimu wa ‘sub’ ni kubadilisha matokeo na kuondoa udhaifu.
“Mchezaji anayeingia kipindi cha pili anakuwa anaibeba timu mabegani mwake, kama timu imeshinda kazi yake inakuwa ni kulinda ushindi, ikihitaji matokeo ahakikishe inapata na siyo fikra potofu kuona wanaingia ili mradi, hakuna maisha ya soka ya namna hiyo,” anasema Mbuna akimaanisha kuwa anayetokea benchi ndiyo staa zaidi ya aliyeanza.
“Mchezaji anapokuwa benchi anakuwa na kazi kubwa ya kuangalia wenzake wanapatia wapi na kukosea wapi, akili zao zinapaswa kuwa mchezoni na siyo kupiga stori, sasa waanze na kubadilisha mitazamo yao ndipo watakapofanikiwa,” anasema na kuongeza kuwa wakati anatua Yanga mwishoni mwa mwaka 1998, alisajiliwa kama straika, aliamua kujiongeza na kucheza nafasi zote.
“Yanga nimecheza namba zote kwa maana ya kipa, beki ya kati na pembeni, kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, kifupi nilifiti kila eneo, sikufanya hivyo kwa bahati mbaya, nilijituma kweli kweli, nikiheshimu kazi na mwili wangu ulikuwa tayari kufanya kila kitu.” anasema Mbuna na kuongeza;
“Nilikuwa naanzia benchi kwasababu ya kuondoa madhaifu yaliyokuwa yanafanywa na wengine, kocha alikuwa anaweza akanipanga nafasi yoyote na nilifanya nilichotakiwa, nikiri kwamba kocha Boniface Mkwasa alinijenga kufikiri tofauti,”anasema.
Anatolea mfano alivyodaka mechi ya Ligi kuu Bara dhidi ya Toto Africans, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Yanga ikishinda mabao 2-0, mwaka 2006.
“Niliingia kipindi cha pili, Benedict Haule alipewa kadi nyekundu na makipa wenzake walikuwa wanaumwa, hivyo hawakuwa sehemu ya mchezo siku hiyo, nikatoka kucheza beki ya pembeni nikaenda kudaka, niliushangaza umati uliyoshuhudia mechi ile baada ya kuokoa mashuti hatari,” anasema Mbuna na kuongeza.
“Kama haitoshi, Yanga tulicheza na Tusker ya Kenya ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0, nikaingia dakika 15 za mwisho zilitosha kutoa asisti mbili za mabao yaliyofungwa na Boniface Ambani.”
Anaulizwa siri ya kudumu na unahodha? Anajibu “Siyo kazi rahisi unaongoza vichwa vyenye uelewa tofauti, nilizimgatia kujiheshimu mwenyewe, kujua saikolojia zao, nilifanya majukumu yangu kwa unyoofu.”
FUNDI KURUSHA MPIRA
Mbuna alikuwa bora kurusha mipira, iliyokuwa inazaa mabao wakati mwingine, anaeleza hilo kwamba lilitokana na mazoezi maalumu ya urushwaji wa mpira, akisisitiza hakuna vitu vinavyotakiwa kufanyika kwa bahati mbaya uwanjani.
“Tulifanya mazoezi ya kutosha, ili ukiingia kwenye mechi kila kitu kinafanyika kwa urahisi, inashangaza kuona mchezaji anafanya makosa yaleyale, ama kipa anafungwa mabao yaleyele hilo linathibitisha uvivu wao wa mazoezi ya ziada.” anasema Mbuna na kuongeza;
“Hivi umewahi kujiuliza kwa nini kona nyingi hazizalishi mabao, wakati huohuo timu za nje zikipata kona zinafunga, au unakuta mchezaji anakosa penalti mara kwa mara, inatokana na kushindwa kuyafanyia kazi makosa yao wakiwa mazoezi, wanachukulia vitu kawaida sana kwa kurizika na ukubwa wa majina yao mtaani.”
HAMSAHAU KAPUYA
Anasema ilikuwa kati ya mwaka 2003 na 2004 aliitwa timu ya taifa ya Ngorongoro Heroes (U-20), lakini akajikuta anatimuliwa kambini kwasababu ya kugombana na mwandishi wa Habari aliyemshitaki TFF.
Anasema kipindi hicho, Waziri wa Michezo alikuwa, Profesa Juma Othman Kapuya, aliyemsaidia kuondolewa adhabu yake baada ya kuzungumza na uongozi wa TFF, akitaka huduma yake inufaishe taifa.
“Kisa cha ugomvi Yanga ilifungwa na Simba mabao 4-0 Kombe la Tusker, mwandishi akawa ananing’ang’aniza kuniuliza wakati sipo tayari kuzungumza na sikuwa nahodha, nikamjibu vibaya na kumnasa kibao, akanishitaki TFF ambao wakanifukuza kambini, ikanibidi nirejee Yanga” anasema na kuongeza;
“Kapuya akanitetea, nikarejeshwa siku ya mechi tulicheza dhidi ya Burundi kufuzu Afcon, pamoja na kutofanya mazoezi na timu, nilianza kikosi cha kwanza na nilifunga mabao mawili kati ya 3-1 lingine likifungwa Waziri Mahadhi.” anasema.
Kesho Mbuna atafunguka zaidi kuhusu maisha yake ndani ya soka la Bongo.