Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City inavyopambana na kivuli chake!

MBEYA Pict

Muktasari:

  • Kutokana na matokeo waliyonayo msimu huu, imeweka wasiwasi na hofu kwa baadhi ya wadau na mashabiki kuanza kuitabiria kurudi Championship, huku wakishauri nini kifanyike.

REKODI za Mbeya City zinaendelea kupotea kwenye Ligi Kuu kufuatia matokeo yasiyoridhisha, huku presha ikipanda na kushuka kwa mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya.

Kutokana na matokeo waliyonayo msimu huu, imeweka wasiwasi na hofu kwa baadhi ya wadau na mashabiki kuanza kuitabiria kurudi Championship, huku wakishauri nini kifanyike.

Pamoja na mashabiki hao, benchi la ufundi na mastaa wa timu hiyo wameendelea kutuliza presha wakiahidi Mbeya City kuweza kuamka na kufanya vizuri na kubaki salama Ligi Kuu.

MBE 04

REKODI YA MIAKA 10

Timu hiyo yenye mashabiki wengi jijini Mbeya na nje ya mkoa, iliweka heshima yake ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2012/13 kwa kumaliza katika nafasi ya tatu ikiwa chini ya aliyekuwa kocha mkuu, Juma Mwambusi.

Kama haitoshi, msimu uliofuata ilionyesha kuwa haijabahatisha kupanda Ligi Kuu ilipomaliza katika nafasi ya nne na kuvutia wadau wengi waliotamani kuwekeza fedha zao kutokana na matokeo mazuri.

Mbali na kuwa na matokeo hayo, City iliendelea kufanya vizuri ikimaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambako ilidumu kwa miaka 10 mfululizo katika mashindano hayo.

Ikiwa chini ya mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe, Mbeya City ilionyesha ushindani kwenye ligi na kuzipa wakati mgumu timu kubwa nchini, Yanga, Simba na Azam FC.

Mara kadhaa timu hiyo ilikuwa ikizipa ugumu Yanga, Simba na Azam bila kujali nyumbani wala ugenini na kuzifanya timu za Ligi Kuu kuitazama kwa jicho la tatu Mbeya City.

Msimu wa 2022/23 ilijikuta ikishuka daraja kupitia play offs ilipofungwa na Mashujaa FC kwa jumla ya mabao 3-2 na kucheza Championship kwa misimu miwili.

Baada ya kuaga Ligi Kuu, Kimbe aliondoka madarakani na kijiti chake kushikwa na aliyekuwa Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ally Nnunduma aliyehuduma kwa takribani miaka mitatu.

Kwa kipindi hicho, Nnunduma alifanya vizuri kwa kuipandisha timu tena Ligi Kuu na kuisimamia katika mechi nne na matokeo ya mwisho ilikuwa dhidi ya KMC iliposhinda mabao 3-0 ugenini.

Mechi iliyokuwa na mvuto zaidi ilikuwa dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, ambapo City ilionyesha ubora na ushindani na kufanya dakika 90 kuisha kwa suluhu.

Baada ya muda huo, Nnunduma alipata uhamisho kwa kupelekwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu akishika nafasi ya Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia, sera, ubunifu na mipango.

Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya mtendaji mkuu, John Kilua ambaye pia ni Afisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ambaye ameanza kibarua hicho kuiongoza Mbeya City.

MBE 02

ILIVYOREJEA LIGI KUU

Msimu huu wa 2025/26 timu hiyo imerejea upya lakini imeonekana kuchoka ikihaha kutafuta matokeo mazuri na kuweka presha kwa mashabiki katika vita ya kukwepa kushuka daraja.

Matokeo iliyovuna kwenye mechi 12 kwa pointi tisa ni kama inapiga hatua 100 nyuma ikilinganishwa na kile ilichowahi kufanya kwa miaka 10 nyuma licha ya matumaini wanayotoa.

Tangu ushindi wake dhidi ya KMC Oktoba 18, 2025 haijaonja tena ladha hiyo ikiwa chini ya aliyekuwa kocha mkuu, Malale Hamsini aliyepanda nayo Ligi Kuu akichukua mikoba ya Salum Mayanga aliyetimkia Mashujaa FC.

Kwa sasa kikosi hicho kinanolewa na kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na KMC, Mecky Maxime ambaye amesimamia michezo miwili akipoteza mmoja na sare moja.

Katika mechi 12 ilizocheza imeruhusu mabao 17, huku ikifunga sita tu na kuwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu yenye timu 16, hali ambayo inawapa wakati mgumu kujikwamua kutoka katika nafasi hizo za mkiani.

MBE 01

USAJILI WENYE WAKONGWE

Katika dirisha dogo lililofungwa Januari 30, Mbeya City imeongeza wachezaji wanane ikiamiani wanaweza kufanya kazi na kuleta mabadiliko na tayari baadhi wameshaanza kutumika.

Orodha hiyo, iliwajumuisha mastaa wa zamani waliowahi kutamba katika timu za Simba na Yanga akiwamo ni Yacouba Songne, Hassan Dilunga na Kelvin Kijili, huku wengine wakipita katika timu nyingine zenye ushindani.

Mastaa hao ni Omary Omary, Hijja Shamte, Mohamed Ally, Said Naushad na Abdalah Kulandana, ambao matumaini ya wengi ni kuona wanakuja na kitu cha utofauti.


WASIKIE WACHEZAJI

Kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya amesema pamoja na kuanza kwa unyonge ligi, lakini bado wanao uwezo wa kubadili matokeo kwa kuwa wachezaji wote wanao uwezo.

Anasema mashabiki na wadau wanaoikatia tamaa timu hiyo bado ni mapema kwa kuwa lolote linawezekana kutokana na ligi kuwa kwenye mwendelezo akiahidi kuwa, City itarudi vizuri.

“Ni mapema sana kuitabiria mabaya timu, wachezaji tunao uwezo kupambana na kuweza kuiondoa nafasi za chini, huu ni upepo umetuanzia vibaya ila tutaamka upya,” anasema Kakolanya.

Naye kipa wa timu hiyo, Soud Dondola anasema wamekutana na mwanzo mgumu, lakini watakapoanza kushinda hakuna atakayewasimamisha akiahidi Mbeya City kubaki salama Ligi Kuu.

“Hata maji baharini huchafuka, tunaendelea kupambana kuhakikisha mechi zinazofuata tunafanya vizuri, tunao muda wa kusahihisha makosa na kusimama imara,” amesema Dondola.

MBE 05

MAXIME AWATULIZA

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime anasema licha ya kutoanza vyema, anaridhishwa na uimara wa timu kwa namna wachezaji walivyoonyesha kuingia kwenye mfumo wake.

Anasema kwa sasa timu imekuwa na muunganiko na wachezaji wameonekana kutengeneza nafasi tofauti na ilivyokuwa awali, akiahidi kuwa wanachopambania kwa sasa ni ushindi.

“Timu inacheza, inamiliki mpira na inatengeneza nafasi tatizo lililobaki ni kufunga na kushinda mechi, naendelea kuwaandaa kiakili na kisaikolojia ili kusahau matokeo yaliyopita.

“Naendelea kuisuka safu ya ushambuliaji na ukizingatia usajili tuliofanya wakiwamo wachezaji wenye uzoefu wameanza vizuri, matarajio yangu ni kuona mabadiliko zaidi katika mechi zijazo,” amesema Maxime.

MBE 03

WADAU, MASHABIKI WANASEMAJE?

William Michael anasema matokeo waliyonayo timu hiyo hairidhishi na kama uongozi hautashtuka, huenda City ikarejea tena Championship kutokana na hali ilivyo Ligi Kuu.

Anasema usajili walioufanya bado ni mapema kuutabiria, lakini hali si nzuri kikosini na inahitaji nguvu ya ziada kwa mechi zilizobaki kuhakikisha wanaondokana na aibu.

“Uongozi kama ni pesa itumike waangalie uwezekano wa kutangaza hata bonasi kwa kila mechi ili kurejesha morali kwa wachezaji, mwendelezo wa matokeo ya kupoteza imewaharibu kiakili,” anasema Michael.

Naye Charles Nsemwa anasema pamoja na uongozi kutoa sapoti kubwa kwa timu, lakini kuna baadhi ya wachezaji uwezo wao uwanjani ni mdogo na hali hii inaweza kuathiri matokeo ya jumla.

“Presha inatukuta sisi mashabiki ambao kila mechi tunaacha kazi zetu kuja kushangilia, baadhi ya wachezaji uwezo ni mdogo, tunaweza kupoteza hii timu Ligi Kuu kama hatutashtuka mapema,” amesema Nsemwa.