Maswali magumu ratiba Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Ratiiba hiyo inaonyesha msimu rasmi wa ligi utafungwa Julai 4,2026 utakapochezwa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB na kila klabu, wadau mashabiki watapumzia kusubiri msimu ujao wa 2026/27.
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa ratiba mpya ya kumalizia msimu wa 2025/26 na mechi za mwisho za mzunguko wa 30 ambazo ni za kufunga msimu, zitapigwa Juni 30,2026.
Ratiiba hiyo inaonyesha msimu rasmi wa ligi utafungwa Julai 4,2026 utakapochezwa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB na kila klabu, wadau mashabiki watapumzia kusubiri msimu ujao wa 2026/27.
Kuna uwezekano mkubwa hii ikawa ndiyo ratiba ndefu zaidi kuwahi kutokea duniani. Inaizidi hata ile iliyokuwa imekumwa na janga la Corona (Uviko 19) na ulimwengu ulitikiswa na kusababisha michezo kusimama ikiwamo soka na ligi mbalimbali duniani zilisimama au kuchezwa bila ya mashabiki kuhudhuria ili kuepuka migusano ambayo ndiyo ilikuwa hasa inayoeneza ugonjwa huo wa mlipuko.
Katika Ligi Kuu Bara, kumekuwa na mvurugiko wa ratiba kwa miaka mingi jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na wadau wa soka na hata klabu na zimekuwa zikilazimika kucheza ili tu msimu kumalizika lakini zinaona wazi hazijatendewa haki katika mambo hayo.
Ni wazi ukitazama kwa undani msimu huu kwa nini umekuwa mrefu kiasi hiki. Utajiuliza kilichochangia kuwa ndefu ni nini kwani hata yale mashindano ambayo Tanzania ilishiriki ikiwamo Fainali za Mataifa Afrika (Afcon), zilizofanyika Morocco ratiba yake ilikuwa inajulikana.
Yapo matukio ikiwamo ya klabu nne za Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa ya Caf na Yanga na Simba zilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na Singida Black Stars zikishiriki Kombe la Shirikisho.
Ni wazi ratiba za mechi zao zilikuwa zinajulikana lakini baada ya timu hizo kuondolewa katika michuano hiyo hadi sasa ratiba haijatulia.
Ni wazi ratiba ya ligi imeendelea kuwa kidonda sugu kwa TPLB na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ipo siku tunaweza kwenda mbali zaidi kama hatutaamua kutafuta tiba ya hili kwa haraka kama ilivyoonekana katika mambo haya.
MECHI KILA SIKU
Hili limewashangaza wengi na kujiuliza vipi hali za wachezaji zitakuje kwani hawapumziki kutokana na kucheza mechi mfululizo na kila siku inabidi wawe safarini kuwahi vituo vya mechi.
Ukiamka leo utasikia Pamba inacheza na timu fulani na kesho yake utasikia Simba inacheza na timu nyingine, ukiamka kesho yake utaambiwa Azam ipo ugenini leo.
Hakuna siku maalum za kucheza ligi hatua ambayo itatoa mapumziko sahihi na kutoa hamu ya kufuatilia hizo mechi ili kuongeza mvuto zaidi.
Katika ratiba ya msimu huu zimetokea mechi kuchezwa chini ya saa 72 hatua ambayo ni ya hatari kwa afya za wachezaji kwani inaweza kuzalisha majeruhi wengi.
TIMU NDOGO ZINAUMIZWA
Zipo timu kwenye ligi zina matarajio makubwa na mechi dhidi ya klabu kubwa kama Simba, Yanga, Azam, hata hivyo, unakuta ratiba ya mechi zao dhidi ya wakubwa hao zinapagwa katikati ya wiki, hii inapunguza uwezekano wa kupata mapato ya kutosha.
Mechi hizo kama zingefanyika wikiendi zingeweza kuwa sehemu ya kuingiza fedha za kutosha klabu hizo ili zipate mapato ambayo wanayatarajia lakini haipo hivyo hapa kwetu.
Hebu fikiria juzi Aprili Mosi Singida ilikuwa nyumbani dhidi ya Azam FC kule Singida, kulikuwa na shida gani Simba isicheze saa moja usiku siku hiyohiyo hali ya kuwa mechi hizo zimechezwa mikoa tofauti?
Azam na Simba zote zilikuwa na wachezaji waliokuwa na timu ya taifa kule Rwanda ambao walirejea pamoja na wale wa Azam wamewahi Singida wakisafiri umbali mrefu na wakacheza na kuamua matokeo wakiwemo Idd Seleman ‘Nado’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wakati wale wa Simba wakiwahi kujiunga na timu yao na bado wakashindwa kucheza mchezo ambao ulitakiwa kucheza hapohapo waliposhukia wakitokea Rwanda.
Mechi za ligi wakati mwingine zinapelekwa mbali bila kuwa na sababu nzito wakati zingeweza kuchezwa kwa wakati mwafaka na ushindani ukionekana, hili linaondoa afya ya ligi na hapo baadaye unakuja kuona mechi za karibu zinakuja hali ya kuwa kulikuwa na muda wa kutosha maeneo mengine.
FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA
Ni wazi hadi fainali za Kombe la Dunia zinakaribia kumalizika ligi yetu itakuwa inaendelea. Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 19 huku ligi ikitarajiwa kumalizika Julai 4 kama hakutatokea mabadiliko mengine ya ratiba na kupanguliwa.
Kombe la Dunia ni moja ya michuano inayofuatiliwa kwa wengi na hata wachezaji, viongozi na wadau wengi wanafuatilia. Hivyo, ligi kuchezwa wakati fainali hizi zinachezwa ni kulazimisha tu iishe lakini ni wazi itapoteza mvuto na wengi watahamia katika michuano hiyo ya kwanza kwa ukubwa duniani inayokutanisha nyota wakubwa.
Wengi watatamani kwenda kuitazama moja kwa moja inakoandaliwa Marekani, Canada na Mexico na baadhi yao watakuwa ni wahusika wa ligi yetu. Kwa maana hiyo itawapa wakati mgumu kushika moja na ndiyo hapo itawabidi kuchagua wakaanzie mechi za katikati wakisubiri ligi iishe au waende waiache ikiendelea huku wao wakipata burudani kubwa zaidi inayofuatiliwa na maelfu ya watazamaji duniani.
IDRISA MFUPA MGUMU
Novemba 29,2025 TPLB ilipata mwenyekiti mpya ambaye ni Nassoro Idrisa ‘Father’ ambaye hadi leo anamaliza zaidi ya siku 122 akiwa kwenye nafasi hiyo, hili litamhusu na moja ya vitu ambavyo anatakiwa kukaa pamoja na wenzake wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiongozwa na Rais Wallace Karia na Oscar Mirambo ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa TFF ni kutafuta tiba ya hii ratiba.
Father sio mtu mgeni pale TPLB kwani hapo kabla alikuwa makamu mwenyekiti, anaijua vyema ligi yetu na hakuna shaka anajua shida ilipo, hakuna sababu ya kuwa na ratiba ndefu ya ligi kama hii endapo wataamua kulimaliza hili.
Endapo tutaendelea kulifumbia macho hili, itafika wakati ligi zitaungana kwa maana msimu unamalizika na mwingine unaanza kabla hata wachezaji hawajapumzika na klabu kujiandaa na msimu mpya. Tushtuke mapema.