Prime
Mastaa hawa Simba washtuke mapema

Muktasari:
- Hilo kwa upande mwingine limewafanya baadhi kusugua benchi au wakipata nafasi kiduchu ya kucheza. Ni wazi wana wakati mgumu kwenye kikosi hiho kinachopambana kubeba taji la Ligi Kuu Bara linalowaniwa pia na mabingwa watetezi, Yanga inayoongoza msimamo na pointi 61, huku wanamsimbazi ikiwa ya pili na pointi 57.
MWANZONI mwa msimu huu 2024-2025, Kocha wa Simba, Fadlu Davids alionekana kumpa nafasi ya kucheza kila mchezaji na kuna waliomshawishi kwa kuonyesha viwango vya kuisaidia timu. Hawa tayari wana utawala wao kikosi cha kwanza.
Hilo kwa upande mwingine limewafanya baadhi kusugua benchi au wakipata nafasi kiduchu ya kucheza.
Ni wazi wana wakati mgumu kwenye kikosi hiho kinachopambana kubeba taji la Ligi Kuu Bara linalowaniwa pia na mabingwa watetezi, Yanga inayoongoza msimamo na pointi 61, huku wanamsimbazi ikiwa ya pili na pointi 57.
Ni wazi pia kutokutumika kwao mara kwa mara ni ili klabu kufikia malengo yake msimu huu ikiwa pia ndiyo pekee inayoliwakilisha Taifa kwenye michuano ya kimataifa ikiwa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo wa kwanza ilipoteza dhidi ya Al Masry kwa kuchapwa mabao 2-0, jijini Suez, Misri na zitarudiana Aprili 10 Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam huku Simba ikipewa nafasi kubwa kusonga mbele.
Hapa Mwanaspoti linakuchambulia mastaa walio na wakati mgumu zaidi wa kupata nafasi ya kucheza mbele ya wanaoanza kikosi cha kwanza Simba, kutokana na kuzidiana viwango na ubora wao uwanjani. Pia hali hiyo ina hatarisha ajira zao na mwisho wa msimu lolote linaweza kutokea ikiwa si kutolewa kwa mkopo wanaweza wakaondolewa kikosini kama mambo hayatabadilika.
Hii ni tathmini ya wachezaji wanaopitia wakati mgumu zaidi kwenye kikosi hicho katika maeneo tofauti.

Hussein Kazi – Beki wa Kati
Amepata nafasi ya kucheza dakika 10 pekee msimu huu katika ligi, jambo linaloonyesha ugumu wa kupata nafasi mbele ya mabeki waliopo. Kwa sasa, safu ya ulinzi ya Simba inaongozwa na Che Fondoh Malone (mechi 19, dakika 1260, mabao 2), Abdulrazack Hamza (mechi 17, dakika 1160, bao 1), na Chamou Karabou (mechi 14, dakika 912).
Mabeki hawa wanaonekana kuwa chaguo la kwanza la benchi la ufundi, jambo linalompa Kazi kibarua kigumu. Ili kurejea kwenye ushindani, atahitaji kuonyesha uimara katika mazoezi, kuboresha uwezo wake wa kupambana na washambuliaji wa timu pinzani na kuwa tayari kuchangamkia fursa chache anazopata. Pia, kutumia mechi za kirafiki na mazoezi kuonyesha ubora wake kunaweza kumsaidia kupata nafasi zaidi.
Kazi aliwahi kumzungumzia Hamza kwamba ana umakini mkubwa wa kuziona hatari, akili yake ina maamuzi ya haraka kutegua mitego ya wapinzani pindi timu inapokuwa inashambuliwa, kitu alichokisisitiza anakipenda kutoka kwa staa huyo.

Edwin Balua – Winga
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri mwishoni mwa msimu uliopita, Balua alitarajiwa kuwa na msimu mzuri zaidi. Hata hivyo, kwa sasa anaonekana kuwa nyuma ya Elie Mpanzu (mechi 10, dakika 785, mabao 2, asisti 2).
Balua amepata mechi nane pekee, akicheza kwa dakika 317 na kufunga mabao mawili. Mpanzu ameonyesha kiwango kizuri katika eneo la ushambuliaji, akichangia mabao ya Simba kwa usahihi mkubwa licha ya kuingia dirisha dogo.
Hali hii inamlazimu Balua kuongeza ubunifu, kasi na uwezo wa kutumia nafasi chache anazopata uwanjani ili kumshawishi kocha kumpa nafasi zaidi.
Anayemfundisha mazoezi binafsi Mpanzu, Mohammed Mrishona Mohammed 'Xavi' aliwahi kusema staa huyo ni fundi wa kukaa na mpira mguuni na ana jicho la kutoa pasi sahihi, jambo ambalo wanaoshindana nao namba wanapaswa kujipanga.

Mzamiru Yassin – Kiungo wa chini
Amekuwa na wakati mgumu tangu aliporejea kutoka kwenye majeraha. Kwa sasa, eneo la kiungo kimekuwa chini ya Yusuph Kagoma (mechi 12, dakika 580), Augustine Okejepha (mechi 10, dakika 510) na Fabrice Ngoma (mechi 16, dakika 1117, mabao 3).
Mzamiru amecheza mechi 7 pekee za ligi msimu huu, akipata dakika 279 bila kufunga bao wala asisti.
Atahitaji kuongeza kasi ya kurejesha kiwango chake ili kushindana na wenzake walioko kwenye ubora wa juu. Pia, ni muhimu kwake kuboresha uwezo wa kupiga pasi sahihi na kusaidia safu ya ulinzi, kwani ushindani kwenye nafasi yake ni mkubwa. Kiungo huyo yupo Simba tangu Julai 2016.

Joshua Mutale – Winga
Alikuwa mmoja wa wachezaji waliotegemewa mwanzoni mwa msimu, lakini sasa anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Kibu Denis (mechi 16, dakika 1041, mabao 2, asisti 1) na Ladack Chasambi (mechi 10, dakika 638, bao 1, asisti 2).
Mutale amepata dakika 451 katika mechi 11 alizocheza lakini hana bao wala asisti. Ili kurejea kwenye kikosi cha kwanza, atahitaji kuongeza kasi, uimara wa kushambulia na uwezo wa kutoa pasi za mwisho. Pia, atahitaji kuongeza utulivu wake katika nafasi za kufunga mabao, jambo ambalo linaweza kumsaidia kushawishi benchi la ufundi kumpa nafasi zaidi.

Omary Omary – Kiungo wa kati
Miongoni mwa wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kutosha msimu huu, akicheza mechi mbili pekee za ligi kwa dakika 55.
Ushindani kwenye nafasi yake umekuwa mkali zaidi kutoka kwa Jean Charles Ahoua (mechi 20, dakika 1457, mabao 12, asisti 6) na Awesu Awesu (mechi 16, dakika 656, mabao 2, asisti 1).
Kwa kiwango anachoonyesha Ahoua, Omary anahitaji kufanya kazi kubwa zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza mara kwa mara. Moja ya mambo ambayo anaweza kufanya ni kuboresha uchezaji wake wa kushambulia, kuongeza kasi yake ya maamuzi na kuwa na utulivu zaidi anapokuwa na mpira.
HAKUNA NAMNA
Ili wachezaji hawa warudi kwenye ushindani wa namba, wanapaswa kufanya kazi zaidi ya wachezaji walioko mbele yao kwa sasa. Mazoezi ya ziada, kuongeza uimara wa mwili na kuwa na mtazamo chanya kunaweza kuwasaidia kupata nafasi ya kucheza.
Kwa upande mwingine, mfumo wa timu na falsafa ya kocha inaweza kuwa changamoto kwa wachezaji hawa. Ikiwa kocha anataka viungo wa kati wenye nguvu na kasi, basi Mzamiru atahitaji kuongeza nguvu na mbinu za kuzuia. Ikiwa kocha anapendelea mabeki wenye uwezo wa kujenga mashambulizi kutoka nyuma, Kazi atahitaji kuonyesha ubunifu wake zaidi kwenye eneo hilo.
MSIKIE FADLU
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amezungumzia ushindani wa namba ndani ya kikosi chake na kusisitiza kila mchezaji anapaswa kupambana ili kupata nafasi ya kucheza.
"Tuna wachezaji wenye vipaji vikubwa, lakini nafasi za kucheza ni chache. Kila mmoja anapaswa kuthibitisha thamani yake mazoezini na kwenye mechi chache wanazopata. Ushindani huu ni mzuri kwa timu, kwani unaleta msukumo wa kuongeza kiwango kwa kila mchezaji," amesema Fadlu.
Hussein Kazi
MECHI: 1
DAKIKA: 10
MABAO: 0
ASISTI: 0
Che Fondoh Malone
MECHI: 19
DAKIKA: 1260
MABAO: 2
ASISTI: 0
Abdulrazack Hamza
MECHI: 17
DAKIKA: 1160
MABAO: 1
ASISTI: 0
Chamou Karabou
MECHI: 14
DAKIKA: 912
MABAO: 0
ASISTI: 0
Edwin Balua
MECHI: 8
DAKIKA: 317
MABAO: 2
ASISTI: 0
Elie Mpanzu
MECHI: 10
DAKIKA: 785
MABAO: 2
ASISTI: 2
Mzamiru Yassin
MECHI: 7
DAKIKA: 279
MABAO: 0
ASISTI: 0
Yusuph Kagoma
MECHI: 12
DAKIKA: 580
MABAO: 0
ASISTI: 0
Augustine OKejepha
MECHI: 10
DAKIKA: 510
MABAO: 0
ASISTI: 0
Fabrice Ngoma
MECHI: 16
DAKIKA: 1117
MABAO: 3
ASISTI: 0
Joshua Mutale
MECHI: 11
DAKIKA: 451
MABAO: 0
ASISTI: 0
Kibu Denis
MECHI: 16
DAKIKA: 1041
MABAO: 2
ASISTI: 1
Ladack Chasambi
MECHI: 10
DAKIKA: 638
MABAO: 1
ASISTI: 2
Omary Omary
MECHI: 2
DAKIKA: 55
MABAO: 0
ASISTI: 0
Awesu Awesu
MECHI: 16
DAKIKA: 656
MABAO: 2
ASISTI: 1
Jean Charles Ahoua
MECHI: 20
DAKIKA: 1457
MABAO: 12
ASISTI: 6