Maneno ya Haji Manara yanachangia ushindi Simba

KIPIGO cha bao 1-0 cha Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika juzi, hakikuchangiwa tu na ubora wa kikosi hicho, bali ujanja mwingine nje ya uwanja.

Maujanja yenyewe ni pamoja na maneno ya mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Simba, Haji Manara ambaye mashabiki wa Simba na wachezaji wanapoyasikia tu - basi huwapa bonge la hamasa na ari ya ushindi.

Msemaji huyu ni mjanja anayejua kucheza na saikolojia za watu, ndiyo maana hata mikutano yake huwa inajaza wanahabari ili wamsikie atasema nini na wakiandika anachosema huwa ni shida kwa wapinzani wake.

Mtindo ambao ameubuni hivi sasa wa kuita mechi hizi kama vile War in Dar (Vita Ndani ya Dar) na huku wakitengeneza picha wakiwa na mavazi ya kijeshi inaongeza ladha na kuvutia kuiona mechi.

Hata wapinzani wao wanaposoma vichwa vya habari na kutazama kuta za mitandao ya kijamii ya Simba na ya msemaji huyo lazima tu kuna hofu itawaingia

Kucheza na hisia za binadamu katika soka haikuanzia tu kwa klabu ya Simba hata England kocha maarufu anayefundisha hivi sasa Klabu ya Tottenham Hotspur, Jose Morinho ametumia sana mbinu hizi kuwabamiza wapinzani kipindi akiifunfisha Chelsea.

Al Ahly ni moja ya klabu kubwa Afrika yenye mafanikio, hivyo matokeo kama yanaumiza washabiki na wachezaji wenyewe kiasi cha kuwapa mpasuka wa kihisia na kuongeza hofu ya kufungwa mechi ijayo.

Timu hiyo ya Misri ipo juu kimafanikio kimataifa ukilinganisha na Simba, hali hii ya matokeo kama haya lazima yatatikisa hisia zao.

Ni ukweli kuwa mpasuko wa hisia kwa wachezaji unaongeza hatari ya kufanya vibaya mchezoni, hivyo ni muhimu kwa Simba kukomalia hapohapo na kutumia mbinu za Manara ili kuongeza hamasa na ari ya ushindi kwa wachezaji wa Simba na kuwachoma wachezaji pinzani kihisia.

Ahadi za kumwaga pesa toka kwa mdhamini wa klabu hiyo, Mohammed Dewji nazo ndizo zimeongeza chachu zaidi kwa wachezaji na kucheza kwa ari ili kupata ushindi.

Mambo kama anayofanya Manara kuwapasua hisia wapinzani wao ndiyo yanazifanya klabu kubwa kimataifa kuwaajiri wanasaikolojia kwa ajili ya kuwatuliza wachezaji kabla na baada ya mechi.

Wachezaji ni binadamu kama wengine wanapokutana na nyomi ya watu ndani ya uwanja kama wa Benjamin Mkapa wakishangilia kwa hamasa kubwa huzidi kuwaongezea hofu hata kama wamezoea matukio kama hayo.


Lakini kwa nini mchezaji anahitaji utulivu wa kiakili? Wachezaji wa Simba watarajie pia matukio mbalimbali ya kuvurugwa kihisia au mambo ya kukera katika mchezo unaofuata kule nchini Misri kwani Waarabu nao ni wazuri kucheza na akili za watu.

Ikumbukwe kuwa mchezaji kucheza katika kiwango bora na kufanya vizuri zaidi atahitaji kuwa na utulivu wa kiakili kuweza kuupiga kwa kujiamini wakati wote wa mchezo. Hivyo kipaji cha Manara cha maneno ya hamasa kinaweza kuwa tiba nzuri ya hisia za wachezaji na kuwafanya katika mchezo wa marudiano kucheza kwa kujiamini na huku wakiwa na utulivu wa kiakili.

Mchezaji anaweza kuvurugwa kisaikolojia kabla, wakati na baada ya mechi na ndiyo maana ndani ya timu kuna wachezaji ambao huwa ni viongozi wa kuwatuliza wenzao wenye mihemko hasi uwanjani.

Nahodha wa timu, msaidizi wake na makipa ni watu ambao mara kwa mara wanatumika kuwatuliza wenzao waliovurugwa kihisia ndani ya uwanja.

Kukabiliana na hali kama hizi wachezaji hupewa msaada wa kisaikolojia toka kwa wataalamu wa tiba, wanasaikolojia, benchi la ufundi, kocha, wachezaji wa akiba, mashabiki na viongozi wa timu.

Mara baada ya kupata kipigo hicho toka kwa Simba hapo juzi ni dhahiri Waarabu hao watatulizwa na kuwajengea kujiamini wachezaji wao kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Kutengenezewa ari ya ushindi na kushinda ni moja ya jambo la msingi kwa kocha na viongozi wa timu kwa ajili ya kuiandaa timu kupata ushindi hata kabla timu haiingia katika uwanja.

Mtu kama Manara kumpitisha tu katika vyumba vya wachezaji kabla ya mechi akaongea mawili matatu tayari anakuwa ameishawapa hamasa na ari wachezaji, hivyo kuwapa utulivu wa kiakili.

Maneo yake yanaweza kuondoa mtego dhaifu wa kisaikolojia katika kupata ushindi na kunyanyua ari ya ushindi dakika za mwisho kabla ya mchezo.

Mchezaji akishapata hitilafu ya kihisia anashindwa kucheza kwa umakini uwanjani ikiwamo kucheza fyongo kama vile kutoa pasi za ovyo au kushindwa kumalizia mabao ya wazi.

Ni dhahiri hiki kimewapata mastaa wa Al-Ahly kutokana na maneno na mwonekano wa Klabu ya Simba na ndiyo maana wameshindwa kuonyesha makali yao kwani wamekosa utulivu wa kiakili.

Utulivu wa akili unajengwa kwa kuweka mawazo chanya na inawezekana tu endapo kuna mfumo uliowekwa ili kuwajengea

wachezaji hisia nzuri zinazochochea ari ya ushindi.

Licha ya matayarisho ya nguvu ya mazoezi ya kila siku na kuwahi kufika kuzowea mazingira ya mpinzani kama walivyofanya Al-Ahly, lakini bado wachezaji wanahitaji kujengewa hisia chanya ili wajione kuwa wao ni washindi zaidi ya wapinzani wao.

Hisia hasi kwa wachezaji ina athari kubwa katika kufanya uamuzi, hivyo kushindwa kucheza kwa ufanisi na kupata ushindi.

Ikumbukwe pia mchezaji ni mtu anayehitaji kufanya uamuzi sahihi kila agusapo mpira, akiwa na hisia mbaya hushindwa hata kufuata maelekezo ya mbinu alizoagizwa kuzifanya na kocha.

Wataalamu wa saikolojia ya wanamichezo wanakubali kuwa hisia nzuri huleta matokeo mazuri, ni kweli wachezaji wa Simba mapema sana walikuwa timamu kihisia ndiyo maana wakapata matokeo jijini Dar es Salaam.

Unapokuwa na hisia chanya inakupa nguvu ya kucheza vizuri, lakini wakati unapopoteza hamasa hukufanya uchoke na kupata hasira kila mara, hivyo kuhatarisha hisia na afya yako kiujumla.

Tafiti zinaonyesha kuwa hisia hasi haziwezi kumsaidia mchezaji kucheza kwa hamasa kwani hali hiyo haimpi furaha mchezoni.

Hisia ni kama msumeno unavyokata pande mbili, unapokuwa na hisia chanya hukupa matokeo mazuri na ikiwa hasi huleta matokeo mabaya.

Maneno ya Manara yamewapiga wapinzani wao toka Misri na kupasua hisia za wachezaji wa Al- Ahly kwa kuwafanya wawe na hisia hasi za ndani kwa ndani, hivyo kukosa utulivu wa kiakili.

Wachezaji wa Simba wanahitaji utulivu wa kiakili zaidi ili waweze kuwa timamu kimwili na kiakili na hatimaye kuwa na ari ya ushindi katika mchezo unaofuata.


Imeandiwa na SpotiDokta: Dokta Shita Samweli