Prime
Mambo matano yaliyobeba hatma ya Simba, Yanga
DAKIKA tisini zijazo za michuano ya kimataifa zimebeba maana kubwa kwa wawakilishi wa Tanzania kuandika rekodi mpya katika soka la nchi hii kupitia michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kuna rekodi tano zinasakwa kupitia wawakilishi hao ambapo Yanga na Simba zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Singida Black Stars zikiwa Kombe la Shirikisho Afrika.
Wawakilishi hao katika mechi za mkondo wa kwanza zilizochezwa wikiendi iliyopita zote zikiwa ugenini, zilipambana kusaka matokeo mazuri, kwa bahati mbaya, Yanga pekee ndiyo iliyopoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Silvers Strikers ya Malawi.
Simba imeichapa Nsingizini Hotspurs ya Eswatini kwa mabao 3-0, Azam ikiifunga KMKM pale Zanzibar mabao 2-0, huku Singida Black Stars iliyoanza kufunga bao kabla ya kusawazishiwa, ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Flambeau du Centre kule Burundi.
Wikiendi hii, kuna dakika nyingine tisini kwa wawakilishi hao wa Tanzania zilizobeba rekodi mpya.
UBABE WA SIMBA
Ushindi wa mabao 3-0 ilioupata Simba katika mechi ya kwanza ugenini wikiendi iliyopita, umeiweka timu hiyo mguu mmoja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini inapaswa kuweka angalizo.
Simba ambayo imekuwa na rekodi nzuri ya michuano ya kimataifa tangu msimu wa 2018–2019, inarudiana na Nsingizini Hotspurs ikihitaji kuendeleza ubabe wake mechi ikipangwa kuchezwa Jumapili ijayo Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kikosi hicho kinachonolewa na meneja Dimitar Pantev akishirikiana na Seleman Matola, kinahitaji kuepuka tu kipigo cha zaidi ya mabao mawili ili kufuzu hatua ya makundi ambapo itakuwa ni mara ya saba ndani ya misimu minane kufika hapo.
Rekodi zinaonyesha katika misimu saba iliyopita ya ushiriki wa Simba kwenye michuano ya CAF, imecheza makundi mara sita na zote hizo ikafanikiwa kuvuka hapo. Haijawahi kuishia makundi. Msimu uliopita 2024-2025, Simba iliweka rekodi mpya ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya awali kukwamia robo fainali.
Safari ya Simba katika kuweka ubabe wake ndani ya michuano ya CAF, ilikuwa msimu wa 2018–19 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuishia robo fainali. Ikaja kuteleza msimu wa 2019–2020 ilipotolewa hatua ya awali na UD Songo kwa sheria ya bao la ugenini baada ya sare ya 1-1 jijini Dar, awali Msumbiji matokeo yalikuwa 0-0. Baada ya hapo, Simba imekuwa na makali huku ikifika robo fainali mfululizo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Robo fainali hizo ilikuwa ni 2020–2021 (Ligi ya Mabingwa), 2021–2022 (Kombe la Shirikisho), 2022–2023 (Ligi ya Mabingwa) na 2023–24 (Ligi ya Mabingwa). Kisha ikaandika rekodi mpya 2024-2025 ilipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza ikapoteza mbele ya RS Berkane.
Kuelekea mechi ya wikiendi hii, Simba haipaswi kuamini moja kwa moja kazi imeisha kwani inaweza kukutana na kitu kizoto kama ilivyokuwa msimu wa 2021–2022 ambapo baada ya ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy katika mechi ya kuwania kufuzu makundi, ikajikuta ikifungwa 3-1 nyumbani na kuondoshwa mashindanoni kwa faida ya bao la ugenini, matokeo ya jumla yakiwa sare ya 3-3. Hiyo ilikuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa bahati nzuri, wakati huo kabla ya sheria kubadilika kuanzia msimu wa 2023–2024, Simba ikapita mlango wa uwani kwa kwenda kucheza mtoano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Red Arrows na kuichapa jumla ya mabao 4-2, ikafuzu makundi, ikaenda kukwamia robo fainali. Wakati huo kabla ya sheria kubadilika, timu za Ligi ya Mabingwa Afrika zilizokuwa zikitolewa katika hatua ya pili kuwania kufuzu makundi, ziliangukia mchujo kwenda kucheza na washindi wa hatua kama hiyo upande wa Kombe la Shirikisho Afrika na mshindi wa jumla, alifuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Kanuni hiyo pia iliibeba Yanga msimu wa 2022-2023 ambapo ilipopoteza Ligi ya Mabingwa Afrika, ikaangukia Shirikisho na kuitoa Club Africain kwa bao 1-0. Kutoka hapo, breki ni fainali, ikapoteza kwa USM Alger kwa faida ya bao la ugenini, mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 1-2, ugenini ikashinda 0-1. Baada ya msimu huo, ndipo sheria ikabadilika, sasa ukipoteza katika Ligi ya Mabingwa, safari yako inaishia hapo.
Meneja Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev, amezungumzia ushindi wa ugenini na mikakati ya mechi ya marudiano akisema: “Ushindi wa 3-0 ni matokeo mazuri sana, lakini namaanisha tunapaswa kuwa na ujasiri zaidi tunapokuwa na mpira na pia kuwa na nidhamu ya kiufundi na kufuata mpango wetu wa mchezo.
“Katika baadhi ya nyakati tulipoteza utulivu wetu. Tulianza kucheza kama wao, tukaanza kutuma mipira mirefu sana na tukawapa faida kwenye mipambano ya moja kwa moja. Unajua wana wachezaji wenye nguvu, si wazuri sana katika kumiliki mpira, pia wana ukali mkubwa kwenye mapambano.
“Kwa hiyo tulihitaji kucheza kwa mtindo tofauti kidogo. Lakini kipindi cha pili, nafikiri tulipofanikiwa kufungua nafasi nyuma ya mabeki wao wa mwisho na kutumia nafasi zile kati ya mabeki wa kati na mabeki wa pembeni, mara nyingi tulipata mafanikio.
“Wachezaji wote walioingia walionyesha juhudi kubwa, nawapongeza kwa hilo. Wote walikuwa na motisha ya kutosha na walitaka kupata alama tatu. Sasa matokeo haya yatatupa kujiamini zaidi, na bila shaka tunapaswa kuonyesha heshima kwa timu hii kwenye mechi inayofuata kwa sababu hii ni kama nusu ya kwanza tu.”
AZAM YA IBENGE
Kuna mstari mwembamba sana unaitenganisha Azam na rekodi mpya ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF iliyoshiriki mara 10 bila ya mafanikio.
Huu ukiwa ni msimu wake wa 11 kushiriki tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 2004, tayari imetengeneza mazingira mazuri kwa kushinda ugenini mabao 2-0 dhidi ya KMKM.
Kwa kiwango ilichoonesha Azam ikiwa ugenini huku rekodi yake nzuri inapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani Azam Complex - Dar, kwa asilimia kubwa timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge inakwenda kuvunja mwiko.
Azam iliyoanza kushiriki michuano ya CAF mwaka 2013, haijawahi kucheza makundi ambapo mara mbili imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na 2024-2025 ambapo zote imeishia hatua ya awali.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, angalau imewahi kufika hatua ya pili, lakini makundi, imekuwa hadithi isiyoisha simulizi kutokana na kutofika huko.
Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2013 na kuishia hatua ya kwanza, kisha 2014 (hatua ya awali), 2016 (hatua ya pili), 2017 (hatua ya kwanza), 2019–2020 (hatua ya kwanza), 2021–2022 (hatua ya pili), 2022-2023 (hatua ya pili), 2023-2024 (hatua ya kwanza).
"Malengo yetu ni kuvuka hatua ijayo lakini niseme wazi bado tuna mechi nyingine ya marudiano ambayo ndiyo itakayoamua kile ambacho kwa umoja wetu tumedhamiria kukifanya msimu huu.
"Ushindi wa mabao mawili ni mkubwa na unatupa matumaini ya mechi yetu ya marudio, ila tunapaswa kutambua hizi ni dakika 45 za kwanza na tuna nyingine pia za mwisho za kufikie kile tunachokikusudia kwa umoja wetu," amesema Ibenge.
SINGIDA KAMA NAMUNGO?
Ukiitoa Simba na Yanga zenye rekodi nzuri ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF, hakuna klabu nyingine ya Tanzania tangu mwaka 2004 ilipoanzishwa Kombe la Shirikisho Afrika iliyowahi kucheza hatua hiyo zaidi ya Namungo.
Kumbuka Kombe la Shirikisho Afrika, ni michuano iliyoanzishwa mwaka 2004 baada ya CAF kuyaunganisha mashindano mawili, African Cup Winners' Cup yaliyoanzishwa mwaka 1975 na CAF Cup ya mwaka 1992, ndipo ikazaliwa yenyewe.
Sasa basi, rekodi ambayo Singida Black Stars inaifukuzia ni kama ile iliyowekwa na Namungo msimu wa 2020–2021 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi licha ya kwamba haikuendelea zaidi ya hapo.
Timu ambazo zimeshiriki michuano hiyo mbali na Simba na Yanga ni KMC (2019–2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021–2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025), na Azam iliyowahi kushiriki mara nane.
Sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Flambeau du Centre, kwa namna moja ama nyingine imekuwa na faida kwa Singida Black Stars inayonolewa na Miguel Gamondi, kocha ambaye katika misimu miwili aliyoifundisha Yanga, aliifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara zote, huku moja akienda nayo hadi robo fainali.
Flambeau du Centre nao sio wanyonge, kwani hii ikiwa ni mara ya pili wanashiriki mashindano ya kimataifa baada ya mwaka 2022 kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, walifanya vizuri hatua ya awali kwa kuiondosha Al Akhdar ya Libya kwa mabao 4-3. Singida Black Stars iliitoa Rayon Sports kwa mabao 3-1 ambapo ilianzia pia ugenini kama hivi ikashinda 1-0, nyumbani ikashinda 2-1.
"Uwekezaji na utayari ndio siri kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hii ya kimataifa, naona Singida Black Stars ikifanya vizuri hasa tukifanikiwa kutinga hatua ya makundi mchezo wetu wa nyumbani, wachezaji wangu wana utayari na nina bahati kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wazoefu," amesema Gamondi.
Clatous Chama na Khalid Aucho ambao walikuwa na kikosi cha Yanga kilichocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024 ikinolewa na Gamondi, wanaonekana kuibeba zaidi Singida Black Stars kwa sasa.
Chama ameendelea kuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho, akifunga bao katika sare ya ugenini, huku pia mechi ya ugenini hatua ya awali dhidi ya Rayon, alitoa asisti ya bao lililofungwa na Marouf Tchakei.
HESABU KALI ZA YANGA
Kipigo cha bao 1-0 ilichopokea Yanga ugenini, kilihitimisha mambo mawili ndani ya kikosi hicho. Kwanza ni kuvunja rekodi yao ya kupoteza kwa mara ya kwanza mechi ya mashindano baada ya kupita siku 315 sawa na miezi 10 na siku 11. Pili ikawa ndiyo mwisho wa kibarua cha kocha Romain Folz.
Kabla ya mechi hiyo, Yanga ilishuka dimbani mara 37 bila ya kupoteza katika mashindano yote. Mara ya mwisho ilipoteza Desemba 7, 2024 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipofungwa mabao 2-0 na MC Alger ikiwa ugenini. Kisha ikapoteza tena Oktoba 18, 2025 ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers, mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga inakwenda kurudiana na Silver Strikers ikiwa inanolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Patrick Mabedi ambaye amekabidhiwa kikosi hicho kufuatia kuondolewa kwa Folz. Mabedi ndiye alikuwa msaidizi wa Folz katika mechi hiyo ya kwanza na alitambulishwa Oktoba 13, 2025, siku tano kabla ya mechi hiyo akichukua nafasi ya Manu Rodriguez, aliyewasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba wake kufuatia kupata changamoto ya kiafya.
Hesabu za Yanga ni kuona inapindua meza na kufuzu makundi ya michuano ya CAF kwa msimu wa nne mfululizo baada ya 2022-2023 (Kombe la Shirikisho), 2023-2024 (Ligi ya Mabingwa) na 2024-2025 (Ligi ya Mabingwa).
Ikifanikiwa katika hilo, Yanga itakuwa imeandika rekodi mpya ya kucheza makundi ya CAF misimu minne mfululizo kwani haijawahi kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1935.
SURA MPYA SOKA LA TANZANIA
Tangu Tanzania ianze kuingiza timu nne katika michuano ya CAF ngazi ya klabu msimu wa 2019–20, haijawahi kutokea timu zote za Bara zikafuzu hatua ya makundi, safari hii kuna asilimia kubwa likatokea hilo.
Tayari tumeshuhudia mara tatu mfululizo wawakilishi wetu wakicheza makundi ndani ya msimu mmoja. Ilikuwa 2022-2023, Simba ikicheza makundi Ligi ya Mabingwa na kuishia robo fainali, Yanga ikawa upande wa Kombe la Shirikisho ikaenda hadi fainali, kisha 2023-2024 zote zilikuwa makundi Ligi ya Mabingwa na kuishia robo fainali, ndipo 2024-2025 Simba ikacheza makundi Kombe la Shirikisho na Yanga Ligi ya Mabingwa. Msimu huo Yanga iliishia makundi na Simba ikacheza fainali Kombe la Shirikisho.