Makambo: Fei Toto ni kama anatudanganya!
Muktasari:
- Heritier Makambo amesema kwa kiwango anachokijua cha Fei Toto, kiungo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania bado hajakitumia kipaji chake chote na siku akiamua kucheza katika ubora wake anaamini mashabiki wataamini anachokisema kwa sasa.
FEISAL Salum ‘Fei Toto’ na kikosi kizima za Azam FC kipo ugenini jioni ya leo katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kuna straika mmoja aliyewahi kucheza naye wakati wakiwa Yanga, amefichua jambo moja, akisema jamaa ni kama anatudanganya vile!
Heritier Makambo amesema kwa kiwango anachokijua cha Fei Toto, kiungo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania bado hajakitumia kipaji chake chote na siku akiamua kucheza katika ubora wake anaamini mashabiki wataamini anachokisema kwa sasa.
Makambo, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, aliyejiunga na Namungo msimu huu akitokea Tabora United ambako msimu uliopita alifunga mabao sita na kutoa asisti nne, amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.
Amefunguka mambo mengi ikiwamo kiwango cha Fei Toto pamoja na mipango na matarajio aliyonayo kwa sasa akiwa na Namungo iliyouanza msimu mpya kwa kulazimishwa sate ya 1-1 nyumbani na Pamba Jiji.
“Ni mchezaji wa kitofauti sana, ukiwa uwanjani unainjoi kumtazama, anafanya kila kitu, lakini naamini atakuwa bora zaidi kwa sababu Fei Toto ninayemfahamu huyu bado kabisa,” anasema Makambo aliyecheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza 2018/19 akiwa na Yanga akifunga mabao 17, kisha akatimkia Horoya AC ya Guinea kabla ya kurejea Jangwani na kisha kutua Tabora United.
KILICHOMVUTIA NAMUNGO
Makambo anaeleza alichovutiwa kujiunga na Namungo ni pamoja na rekodi yao kimataifa na anatamani aandike historia nyingine akiwa na timu hiyo.
Anaongeza kuwa, ukiachana na ofa nzuri aliyowekewa, rekodi ya Namungo kufika makundi Kombe la Shirikisho Afrika ilimshawishi ajiunge na timu hiyo.
Aliongeza kuwa uzoefu alionao akishirikiana na wenzake atajaribu kuipambania timu hiyo imalize ndani ya nafasi tano za juu na kurejea kwenye michuano ya kimataifa.
“Kabla sijasaini Namungo niliuliza malengo ya timu ni nini. Waliponieleza nikaona wako vizuri, nikajiunga nao. Ukiangalia wana rekodi nzuri CAF, hilo limenishawishi kwa kiasi kikubwa,” alisema Makambo na kuongeza:
“Kwa kweli kambi iko vizuri na nimeifurahia. Kikubwa zaidi ni namna viongozi wanavyoelewana, wapo karibu na timu, na pia wanahakikisha wachezaji wanakula kwa wakati. Siwezi kulinganisha na nilikotoka, ila nainjoi nikiwa hapa.”
Aliongeza kuwa msimu uliopita hakuwa na msimu mzuri akikosa muendelezo wa upachikaji mabao.
“Sikuwa na muendelezo mzuri msimu uliopita nilipoichezea Tabora United, hivyo msimu huu nataka kufanya zaidi. Kila ninapopata nafasi ya kufunga basi nifunge ili tutimize lengo la Namungo.”
Namungo msimu uliopita iliachana na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere, ambaye aliitumikia kwa misimu miwili lakini akashindwa kuonyesha kiwango bora. Nafasi yake anachukua Makambo msimu huu.
TABORA UNITED
Anasema hapendi kuzungumzia zaidi timu aliyotoka, lakini alimaliza mkataba na Tabora United hivyo hakutaka kuongeza mkataba mwingine baada ya ule wa awali kutamatika.
“Nilipomaliza mkataba wangu niliamua kuondoka Tabora. Nilitaka kupata changamoto sehemu nyingine, ndipo nikatafutwa na viongozi wa Namungo kwamba wananihitaji. Nikaangalia ofa yao nzuri, ndio nimejiunga nao.”
LIGI KUU vs DRC CONGO
Makambo anasema kuna tofauti kubwa kati ya Ligi Kuu Bara na DRC Congo, akitolea mfano uwepo wa mashabiki kujaza viwanja na namna wanavyowashabikia wachezaji wao.
“Tanzania kuzuri sana, ndio maana wachezaji wengi tunaondoka tunarudi. Huku ukifanya vizuri mashabiki watakupongeza, ukiharibu pia watakurekebisha. Congo mpira hauna vaibu, hata mashabiki uwanjani sio wengi,” anasema na kuongeza:
“Ligi Kuu Bara kuwa namba nne Afrika sio kwa bahati mbaya. Soka la Bongo limeendelea hivi karibuni, mechi zinaonyeshwa zote na wachezaji wanapata fursa ya kuonekana. Zamani kulikuwa na changamoto kubwa hasa kwenye viwanja.
“Yaani mchezaji huwezi kuinjoi kucheza sababu viwanja sio vizuri, ila sasa mambo yamebadilika na hata majeraha ya wachezaji naamini yatapungua kama maboresho yakiendelea kufanyika kwenye viwanja mbalimbali.”
SABABU YA KUVAA JEZI 19
Anasema kuna changamoto aliwahi kuipitia wakati anajiunga na Yanga msimu wa kwanza, ingawa hakutaka kukiweka wazi, ndicho kilichomfanya aichague namba 19.
“Ni kitu ambacho kwa sasa sitaki kukitaja, lakini changamoto hiyo ndio sababu ya kuivaa jezi namba 19 hadi leo. Na nilipojiunga na Yanga kulinirejesha katika mstari wa kuzipigania ndoto zangu,” anasema.
MAYELE MPAMBANAJI
Anamtaja nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, kuwa mmoja wa wachezaji wapambanaji na anachoendelea kukifanya ni sababu ya juhudi zake binafsi.
“Sikushangaa alichokifanya Misri, ni ligi ngumu sana tofauti na Tanzania na DRC Congo, lakini bado alifanya vizuri ndani na kimataifa. Hata siku ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika nilitamani afunge.
“Nimecheza naye Yanga, ni mpambanaji, anapenda kujituma na sio mchezaji ambaye anaridhika. Anajua kufunga na anafanya juhudi nyingi binafsi.”
WACONGO KUCHEZA BONGO
Kuna nyota kibao waliotoka DRC Congo na wakafanya vizuri Ligi Kuu Bara kiasi cha kuaminiwa na vigogo Simba, Yanga na timu nyingine za Tanzania.
Ukimtoa Mayele na Makambo, kuna wachezaji kama Ducapel Moloko, Joyce Lomalisa, Djuma Shaban, Max Nzengeli, Shadrack Boka (Yanga), Elie Mpanzu, Fabrice Ngoma, Henock Inonga (Simba), Andy Bukoko (Dodoma Jiji) na wengineo.
“Sio Simba na Yanga pekee, karibu Ligi Kuu ina wachezaji wengi kutoka huko. Hii ni ishara nzuri kwamba nchi tunayotoka inaaminika na kuwa na vipaji vikubwa.
“Sisi ambao tulikuja kucheza mwanzoni nafikiri ilifanya hata wengine wavutiwe. Mazingira ya Tanzania, namna mashabiki wanavyotupenda na hata ushirikiano, hilo limefanya hata wachezaji wenyewe kushawishika kuja.”
FEI TOTO BADO
Makambo anasema anachokionyesha kiungo wa Azam, Fei Toto, anaamini bado hajaonyesha kiwango anachokijua kwani ni mchezaji mwenye kipaji ambacho Tanzania inapaswa kukilinda.
“Tulikuwa na ukaribu sana tukiwa Yanga. Hata alipokuwa anapitia mgogoro tulikuwa tunaongea sana. Kukaa nje muda mrefu kisha akaja kuonyesha kiwango hiki sio rahisi hata kidogo. Tanzania inapaswa kujivunia naye.
“Fei Toto ni mchezaji ambaye sidhani kama kuna kocha anaweza kumuweka benchi, kwani anakupa vitu vingi uwanjani. Nimefurahi kumuona na kiwango hicho, ila naamini bado hajaonyesha yale makali yake.”
INONGA ALIMSUMBUA
Anasema tangu aanze kucheza Ligi Kuu kwa msimu wa 2018/19, amekutana na mabeki wengi, ila hatamsahau Henock Inonga ambaye anamsifu kuwa alimkaba na kumdhibiti vizuri kwenye mechi zote walizokutana.
“Inonga alinisumbua sana na sijawahi kumsoma vizuri hadi naondoka Yanga. Nakumbuka nilicheza mara mbili naye kwenye FA kule Mwanza.”
BACCA, JOB
Anawataja mabeki wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca na Dickson Job, kuwa miongoni mwa pacha bora kwenye Ligi Kuu Bara.
“Ni mabeki wazuri na mimi nilibahatika kucheza nao kwenye mechi na Tabora tuliyoshinda 3-1. Unajua mimi kabla sijaingia uwanjani huwa nakaa na video, nawasoma ubora na udhaifu wa mabeki wa wapinzani tunaokutana nao,” anasema na kuongeza:
“Ndio maana kwenye mechi na Tabora sikupata tabu sana kuwasoma. Kwa sababu kwanza Job nilicheza naye wakati ule, nilikuwa najua ubora na udhaifu wa mabeki wote. Mmoja anatumia akili na mwingine nguvu zaidi.”
HAPENDI UMAARUFU
Makambo anaeleza kuwa moja ya vitu ambavyo hakipendi kabisa kwenye maisha yake ni kuwa maarufu, akitaja kuna faida na hasara zake.
“Unaweza kuwa maarufu siku moja na ukapotea kwa siku hiyo hiyo. Mimi si mtu wa kutoka sana na sipendi starehe za aina yeyote: ulevi, kukesha usiku, sio vitu vyangu.”
NJE YA SOKA
Anasema nje ya soka yeye ni mume wa mtu na baba wa familia. Anapendelea pia kusoma na kujifunza mambo ya michezo hasa soka kwenye vitabu na mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Sina shughuli nyingine zaidi ya soka. Hilo limenifanya hadi leo familia yangu inaishi vizuri kwa maana nahudumia mke na watoto na mimi mwenyewe sababu ya mpira, hivyo naliheshimu sana.
“Soka limeniheshimisha. Ndani ya miaka saba nimefanya vitu vingi ila sipendi kuviweka wazi. Kuna sehemu nimesaidiwa kirahisi sababu ya soka, nimeingia sehemu ambazo ingekuwa kawaida ingechukua muda mrefu kidogo.”
CHIKUPE, BOXER WAMFUNZA KISWAHILI
Mshambuliaji huyo anasema ingawa baadhi ya sehemu nchini DRC Congo zinaongea Kiswahili, lakini hakuwa anajua kuzungumza lugha hiyo.
“Mimi nimetokea Kinshasa, kule hatuongei Kiswahili. Sikuenda darasa kabisa, ila wakati nipo Yanga nilipata bahati ya kufundishwa na Andrew Vincent Chikupe na Paul Godfrey ‘Boxer’ kwa wakati ule.”
STAILI YA KUWAJAZA
“Nakumbuka kwenye mechi ya kimataifa tulicheza pale Mkapa. Nilipofunga bao, na lilikuwa la kwanza tangu nijiunge, nilishangilia kama napiga makofi hivi kuwahamasisha mashabiki waendelee kushangilia, lakini sikuipanga,” anasema.
“Lakini baadaye niliona kama inapendeza, nikasema kwa nini nisiitumie. Tangu pale nikawa natumia staili ile hadi leo.”