LWASA: Kagera hadi Pamba haikuwa rahisi
Muktasari:
- Mshambuliaji huyu raia wa Uganda mwenye kasi na nidhamu ameanza kuvutia mashabiki kwa kiwango chake, mtazamo chanya na malengo makubwa anayojiwekea.
Katika soka la Tanzania, jina la Peter Lwasa limeanza kuwika upya ndani ya kikosi cha Pamba FC, akiwa amesajiliwa msimu huu akitokea Kagera Sugar.
Mshambuliaji huyu raia wa Uganda mwenye kasi na nidhamu ameanza kuvutia mashabiki kwa kiwango chake, mtazamo chanya na malengo makubwa anayojiwekea.
Ni hadithi ya mchezaji anayepigania nafasi yake, akiweka mbele juhudi, nidhamu, na ndoto ya kuacha alama ya kudumu katika historia ya soka la Tanzania.
TARATIBU HADI KUNG’ARA
Lwasa anaanza msimu huu akiwa na hamasa kubwa, lakini safari yake haikuwa rahisi. Alikosa michezo miwili ya mwanzo wa ligi dhidi ya Namungo FC na Yanga SC, jambo lililowafanya mashabiki wake kujiuliza kinachoendelea.
Anaeleza kwamba changamoto hizo zilikuwa sehemu ya mchakato wa kuzoea mazingira mapya ndani ya kikosi cha Pamba.
“Nilianza msimu nikiwa bado nipo kwenye mabadiliko ya timu na maandalizi binafsi, Nilikosa michezo miwili ya mwanzo kwa sababu nilihitaji muda wa kujiandaa kimwili na kisaikolojia, Timu mpya inahitaji uelewano mpya, na sasa nashukuru nimeanza kuingia vizuri na nahisi niko kwenye kiwango kizuri zaidi.”
KUKOSA MECHI MUHIMU
Lwasa anaeleza kwa uwazi kwamba changamoto hiyo haikutokana na jeraha, bali masuala ya mpito kati ya timu mbili.
“Ni kweli nilikuwa na changamoto kidogo za mpito kutoka Kagera Sugar kuja Pamba. Hayo ni mambo ya kawaida kwenye mpira, hasa unapobadilisha timu. Lakini sikuwa na wasiwasi, nilijua muda ukifika nitarejea uwanjani kwa nguvu mpya. Sasa akili yangu yote ipo Pamba FC.
“Kipindi hicho kimenifundisha uvumilivu na kumtia nguvu zaidi kupambana kuhakikisha nafanya tofauti msimu huu.”
KWA NINI PAMBA
Wakati baadhi ya timu zilionyesha nia ya kumsajili, Lwasa anasema aliona Pamba kama sehemu sahihi ya kuendeleza taaluma yake,
Anasisitiza kuwa, uamuzi wake haukuongozwa na fedha, bali maono na utulivu wa klabu.
“Nilichagua Pamba kwa sababu niliona kuna kitu tofauti, Ni klabu yenye historia, lakini pia yenye mipango mizuri ya kujijenga upya.
“Mazingira ya ndani ni mazuri, kuna mshikamano mkubwa, na kila mtu anafanya kazi kwa malengo ya pamoja, Nilihitaji sehemu yenye umoja na dira, na nilipata yote hayo hapa Pamba.”
OFA
Ingawa hakuwa na uhaba wa ofa, Lwasa anaeleza kwamba moyo wake ulivutwa zaidi na falsafa ya Pamba FC.
Anasema aliona klabu hiyo itampa nafasi ya kujenga upya jina lake na kufikia malengo binafsi.
“Nilikuwa na ofa kadhaa, lakini nilijua wazi nataka kwenda sehemu nitakayopewa nafasi ya kujionyesha kwa uhuru. Nilipoongea na viongozi wa Pamba, nilipata imani kubwa.
“Walinieleza malengo yao waziwazi, na niliona wana dhamira ya kweli ya kufanya timu hii iwe bora. Hapo ndipo nilijua niende Mwanza.”
USHINDANI NOMA
Kama ilivyo kwa timu kubwa yoyote, Pamba FC inajivunia wachezaji wengi wenye ubora, Lwasa anaeleza kuwa ushindani huo unamfanya awe bora zaidi kila siku.
“Ushindani ndani ya timu ni mzuri sana, Kila mchezaji anapigania nafasi yake, na hiyo inanifanya nifanye kazi kwa bidii zaidi, Unapokuwa na wachezaji bora pembeni yako, unajikuta unalazimika kupanda kiwango kila siku. Huo ndio ushindani ninaoupenda wa heshima na kazi.”
MALENGO
Lwasa hachoki kuzungumzia ndoto zake. Anasema msimu huu amejipanga kuweka alama ya kweli kwenye ligi.
“Nimeweka malengo binafsi, lakini zaidi ni kuhakikisha timu inafanya vizuri. Kwa upande wangu, nataka kuwa miongoni mwa wafungaji bora watatu wa ligi.
“Najua ni kazi ngumu, lakini ninaamini nina uwezo wa kufika huko kwa msaada wa wachezaji wenzangu na kocha wetu.”
URITHI ANAOUTAKA
Wakati wengine wakifikiria mafanikio ya sasa, Lwasa anafikiria zaidi kuhusu urithi wake baada ya miaka kadhaa.
“Nataka kuacha historia nzuri kwenye soka la Tanzania. Wachezaji kama Okwi (Emmanuel) na Hamis Kiza ‘Diego’ wamekuwa mfano wa wachezaji wanaocheza kwa juhudi na heshima, nidhamu, kazi na namna ninavyoheshimu mchezo.”€
Kwa Lwasa, tofauti kati ya timu hizo mbili ni wazi, hasa upande wa usimamizi na umoja wa ndani ya kikosi.
“Kagera ilikuwa shule nzuri sana kwangu, lakini Pamba ina mazingira ya kipekee. Hapa viongozi wapo karibu sana na wachezaji wanakujali na kukusikiliza. Pia kuna umoja mkubwa ndani ya timu watu wanasaidiana. Hicho ndicho kitu nilichokosa kwa muda na sasa nakifurahia sana.”
KUMBUKUMBU ZA KAGERA
Lwasa hawezi kuzungumzia mafanikio yake bila kuitaja Kagera Sugar timu iliyomlea na kumpa jukwaa la kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Kagera ndiyo ilinifanya niwe Lwasa ninayejulikana leo. Walinipa nafasi, walinifundisha nidhamu ya kazi, na walinionyesha namna ya kuheshimu mchezo, Nitaendelea kuwa na heshima kubwa kwao, Bila Kagera, Sugar nisingefika hapa.”€
MTAZAMO LIGI KUU
Kwa mtazamo wa Lwasa, Ligi ya Tanzania imepiga hatua kubwa kitaaluma na kiushindani, na sasa imekuwa jukwaa muhimu kwa wachezaji wanaotaka kujijenga.
“Ligi yetu inakua kila mwaka. Kila timu imejipanga, viwango vya wachezaji vimepanda, na ushindani ni mkubwa.
“Kwa kweli, Ligi Kuu Bara ni jukwaa ambalo linaweza kukupeleka mbali kama utachukulia kazi kwa umakini. Mimi naiona kama chuo cha wachezaji wenye ndoto.”
ULINZI MGUMU
Akiwa mshambuliaji, Lwasa anakutana na changamoto nyingi kutoka kwa mabeki wagumu, lakini anasema hayo ndiyo mambo yanayomjenga zaidi.
“Kuna mechi nyingine mabeki wanakuwa wagumu kweli, lakini hiyo ndiyo ladha ya soka. Ukikutana na beki anayekupa wakati mgumu inakulazimisha ubuni njia mpya za kucheza. Inakufanya kuwa mchezaji bora zaidi. Sijawahi kuogopa ulinzi wowote, bali nauchukulia kama somo.”
Lwasa anasema tangu alipojiunga na Pamba, amejenga uhusiano mzuri na benchi la ufundi, jambo ambalo linamfanya ajisikie kuaminiwa.
“Kocha aliniambia wazi: ‘Nataka uwe sehemu ya mabadiliko ya timu hii.’ Maneno hayo yamenigusa sana, Kila siku ninapokuwa mazoezini au kwenye mechi, nakumbuka kwamba nina jukumu la kufanya kitu cha tofauti kwa ajili ya timu, Hiyo imani inanipa nguvu kubwa.”
UGANDA NA TANZANIA
Akiwa amecheza pia katika soka la Uganda kabla ya kuja Tanzania, Lwasa anaona tofauti kubwa ya kiutawala na kiushindani. Soka la Tanzania limepiga hatua kubwa. Ligi inaendeshwa kwa weledi, mashabiki wana mapenzi ya kweli, na miundombinu inazidi kuboreshwa, Ukiwa hapa, unajua unacheza kwenye ligi yenye hadhi. Hiyo inanijenga kisaikolojia na kunipa motisha ya kuwa bora zaidi.”