Ladack nyota mpya Mtibwa anayemzimia Maxi Nzengeli

MIONGONI mwa wachezaji waliopandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana ni Ladack Chasambi ambaye amekuwa maarufu baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Vijana U-20.

Chasambi katika mashindano hayo ambayo Mtibwa Sugar ilibeba ubingwa mara tano mfululizo na kukomba karibu kila tuzo ilizowania ikiwemo  ya mchezaji bora mara mbili mfululizo, alipandishwa timu ya wakubwa msimu huu, ingawa alipewa nafasi tangu mechi za msimu uliopita chini ya Kocha Salum Mayanga na kuonyesha uwezo mkubwa.

Mchezaji huyo anasema mbali na kuonyesha kiwango bora, lakini anaendelea kujifunza mambo mbalimbali ya soka na kuwatazama waliomtangulia.


ALIPOANZIA SOKA

Winga huyo aliyezaliwa 2004, Kisaki mkoani Morogoro anasema alianza kucheza mpira wa miguu katika akademi ya Moro Kids iliyopo mjini humo.

Chasambi alianza katika akademi hiyo akiwa na umri wa miaka 15 ambapo baadaye alihamia Alliance Boys ya Mwanza, na baada ya kufanya vizuri ambacho kimekuwa kikifanya vizuri kwa kukuza vipaji vya vijana kupita Alliance Boys ndipo akachaguliwa kujiunga na Serengeti Boys akiwa na wenzake kina Kelvin John.

Anasema baada ya kufanya vizuri na kupewa kijiti cha unahodha, alijiunga na Mtibwa Sugar ambako aliisaidia kubeba ubingwa akifanya hivyo mara mbili mfululizo.


MAXI BALAA

Unaambiwa kinda huyo anapenda kujifunza vitu mbalimbali kupitia kwa mastaa ambao wamemtangulia, lakini winga mpya wa Yanga, Maxi Nzengeli ambaye pia hucheza nafasi moja na yeye humwambii kitu kwake.

Anasema anafurahi akimuona Max ambaye pia hujifunza vitu vingi kutoka kwa Mkongomani huyo aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Maniema ya DR Congo.

Mbali na Max, wengine ambao anafurahi kuwaona wakicheza uwanjani ni kiungo Feisal Salum wa Azam FC na Saido Ntibazonkiza wa Simba.

“Wachezaji wengi sana Ligi Kuu najifunza kupitia kaka zangu walionitangulia, lakini Maxi Nzengeli namfurahia zaidi nikimuona kwa sababu hucheza nafasi yangu. Kina Saido Ntibanzonkiza na Feisal Salum nafurahi sana nikiwaona wanacheza.”


SIMBA KIPIMO KIZURI

Wahenga wanasema kosa sio kosa, bali kurudia kosa ndio kosa. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Chasambi ambaye katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara amejifunza mambo mengi.

Licha ya kuchapwa mabao 4-2 na Simba, lakini anasema ilikuwa mechi yenye kipimo kizuri kwake kwani tangu aanze soka hakuwahi kucheza na timu kubwa kama Simba.

Anasema mechi ile aliingia kwa kujiamini ili kufanya vizuri, lakini kosa moja ndilo liliwaangusha na kupokea kichapo.

“Mechi na Simba ilikuwa kipimo kizuri kwangu na kuna vitu vingi nimejifunza, kubwa zaidi ni kujiamini na kuondoa hofu ya mechi. Naamini siku nyingine tutafanya vizuri,” anasema.


SIRI YA UBINGWA U-20

Akizungumzia ubingwa U-20, anasema Mtibwa Sugar imekuwa chuo ambacho kinakuza vipaji vya wachezaji ambao hufanya vizuri Ligi Kuu na hata nje na hiyo ndiyo siri ya kufanya vizuri kwenye ligi ya vijana kwani hufanya maandalizi mazuri na kuwa na malengo makubwa kama timu.

Hata hivyo, anasema kama timu inaweka malengo ya kufanya vizuri, lakini mwenyewe huweka malengo binafsi.

“Siri kubwa ya kufanya vizuri kwa vijana ni maandalizi yetu. Tulikuwa na maandalizi mazuri na tuliweka malengo kama timu na mimi kama mchezaji nilikuwa na malengo binafsi, ndio hiyo ndio siri kubwa.”


MTIBWA SASA HATARI

Mchezaji huyo aliyebeba tuzo ya mchezaji bora mara mfululizo, anasema msimu huu kuna vijana wengi ambao hawana uzoefu wa ligi wamepandishwa timu kubwa.

Lakini, anakiona kikosi cha sasa cha timu hiyo kuwa hatari kwa sababu kila mchezaji aliyepandishwa ana uwezo mkubwa, akisema kikubwa makocha na viongozi wa timu wawape muda zaidi ili kuonyesha viwango.

“Mtibwa ya sasa ni hatari kwani tuna kikosi kizuri japo kina wachezaji wengi wazoefu nafikiri tukipata muda zaidi tutafika mbali,” anasema winga huyo.


MATTEO, MUVI FRESH

Chasambi anamtaja mshambuliaji mpya wa Mtibwa Sugar, Matteo Antony kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa hasa akiwa mazoezini.

“Matteo ni mchezaji mzuri na ana mengi ambayo kama sisi wapya tuna cha kujifunza kutoka kwake na amekuwa na mchango mkubwa klabuni,” anasema mchezaji huyo.

Akizungumzia anachopenda nje ya soka, Chasambi anasema muda mwingi anapokuwa kambini hupendelea kuangalia muvi mbalimbali ili kuiweka akili yake sawa.

“Maisha yangu yamekuwa mpira na mimi - mimi na mpira, hivyo muda mwingi napokuwa kambini napenda kuangalia muvi mbalimbali ili kuiweka akili yangu sawa isiwe na mambo mengi.”


MALENGO YAKE

Chipukizi huyo anasema kila mchezaji ana malengo, lakini kwake ni kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara kama alivyofanikiwa kwa vijana. “Nimepandishwa msimu huu rasmi timu ya wakubwa na kama mchezaji nina malengo yangu nataka kufanya vizuri zaidi kama ilivyokuwa kwa vijana japo huku ni tofauti kwa kuwa ni ligi yenye ushindani mkubwa,” anasema mchezaji huyo.