Kane atajwa tuzo Ballon d’Or
Muktasari:
- Kane ndiye mchezaji ambaye hawezi kubadilishwa kirahisi katika kikosi cha England, jambo lililodhihirika wazi wakati timu ya Thomas Tuchel iliposhindwa kutumia nafasi nyingi katika mechi za kirafiki za Machi, ilipotoka sare dhidi ya Uruguay na baadaye kufungwa na Japan kwenye Uwanja wa Wembley.
LONDON, ENGLAND: Kazi ya mwisho ya mshambuliaji Harry Kane katika msimu bora zaidi wa maisha yake ya soka ni kuingoza timu ya taifa ya England kwenye Kombe la Dunia iwapo atafanikiwa kutwaa taji hilo hakuna shaka atanyakuwa tuzo ya Ballon d’Or.
Kane ndiye mchezaji ambaye hawezi kubadilishwa kirahisi katika kikosi cha England, jambo lililodhihirika wazi wakati timu ya Thomas Tuchel iliposhindwa kutumia nafasi nyingi katika mechi za kirafiki za Machi, ilipotoka sare dhidi ya Uruguay na baadaye kufungwa na Japan kwenye Uwanja wa Wembley.
Akiwa na miaka 32, afya na utimamu wa Kane ndiyo jambo litakalompa wasiwasi mkubwa Tuchel wakati England ikijiandaa kuanza kampeni yake ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia mjini Dallas tarehe 17 Juni.
Sababu si tu kwamba Kane ndiye mfungaji bora wa muda wote wa England akiwa na mabao 78 katika mechi 112, bali pia kwa sababu England haina mshambuliaji mwingine wa kiwango chake.
Iwapo Kane atabaki fiti na kuendelea na kiwango chake bora kilichomfanya afunge mabao 64 katika mechi 56 akiwa na Bayern Munich msimu huu, matumaini ya England kutwaa Kombe la Dunia yataongezeka sana.
Lakini kama atapata matatizo ya kiafya au kushuka kiwango, hali inaweza kuwa tofauti kabisa.
Kane pia ni mmoja wa majina yanayotajwa kuipata tuzo ya Ballon d’Or, inayotolewa kwa mchezaji bora wa mwaka barani Ulaya. Tayari ameshinda tuzo ya Golden Shoe kwa kuwa mfungaji bora zaidi barani Ulaya msimu huu.
Ingawa Bayern Munich iliondolewa na Paris Saint-Germain katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, jambo hilo halijapunguza ubora wa msimu wake wa kipekee.
Mchambuzi Robinson anaamini Kane anastahili kushinda Ballon d’Or mwaka huu. “Atashinda mwaka huu. Ni nani mwingine atashinda? Ukiangalia mafanikio yake na idadi ya mabao aliyofunga akiwa klabuni, hakuna anayemkaribia.
“Ameshinda mataji na bado ana nafasi ya kupata mafanikio makubwa kwenye Kombe la Dunia, jambo ambalo mara nyingi lina mchango mkubwa katika kumpata mshindi wa Ballon d’Or.
“Kwa mtazamo wangu, hakuna sababu yoyote inayoweza kumzuia kushinda tuzo hiyo.”
England na kocha Tuchel watakuwa na matumaini kwamba Kane ataweka muhuri wa mafanikio hayo kwa kuiongoza nchi yake kutwaa Kombe la Dunia na kumaliza miaka mingi ya kusubiri utukufu wa kimataifa.