Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jamaa hawa wamezifunga timu walizowahi kuzichezea bara

Muktasari:

  • Hata hivyo, wakati Ligi Kuu ikisimama, tayari tumeshuhudia wachezaji mbalimbali msimu huu wakizifunga timu ambazo wamewahi kuzichezea na kuteka hisia za mashabiki wa soka nchini, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea nyota hao na walichofanya.

LIGI Kuu Bara imesimama kwa takribani wiki mbili kupisha mechi za timu za taifa, ambapo hadi sasa tumeshuhudia ushindani mkubwa kwa timu shiriki na wachezaji.

Hata hivyo, wakati Ligi Kuu ikisimama, tayari tumeshuhudia wachezaji mbalimbali msimu huu wakizifunga timu ambazo wamewahi kuzichezea na kuteka hisia za mashabiki wa soka nchini, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea nyota hao na walichofanya.


PAUL PETER VS AZAM

Nyota huyo aliinyima Azam pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni jijini Dar es Salaam, Oktoba 1, 2025, baada ya kuwafungia maafande wa JKT Tanzania bao la kusawazisha la dakika ya 90+2.

Paul Peter aliyewahi kuanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, hadi kupandishwa kuchezea ya wakubwa, alifunga bao hilo la kusawazisha kwa JKT, baada ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutangulia kufunga kipindi cha kwanza dakika ya 42.

Mshambuliaji huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba, msimu wa 2017-2018, aliifungia JKT bao hilo hivyo, kusababisha mechi hiyo iliyokuwa kali na ya kusisimua kuisha kwa sare ya 1-1.

Nyota huyo amejiunga na JKT msimu huu, akitokea Dodoma Jiji, baada ya msimu wa 2024-2025, kufunga mabao manane ya Ligi Kuu, akishika nafasi ya pili kwa wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14. 


MATHEO ANTHONY VS KMC

Mshambuliaji, Matheo Anthony anayeichezea kwa sasa Mbeya City, aliiliza KMC aliyowahi kuichezea kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, baada ya kufunga mabao mawili na kukiwezesha kikosi hicho kilichopanda daraja msimu huu kushinda kwa mabao 3-0.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Mwenge Oktoba 18, 2025, Matheo alifunga mabao hayo mawili (dk21 na 48), huku jingine moja likifungwa na Vitalis Mayanga dk26.

Matheo aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwemo za Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) cha visiwani Zanzibar, Yanga na Mtibwa Sugar, ni miongoni mwa washambuliaji tegemeo ndani ya kikosi cha Mbeya City, chini ya kocha, Malale Hamsini.


VITALIS MAYANGA VS KMC

Vitalis Mayanga anayeichezea Mbeya City msimu huu, ni miongoni mwa wachezaji walioiliza KMC aliyowahi kuichezea msimu wa 2019-2020, wakati kikosi hicho kutoka jijini Mbeya kiliposhinda ugenini kwa mabao 3-0 Oktoba 18, 2025.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Mayanga aliyejiunga na Mbeya City msimu huu akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, alifunga bao moja, huku mawili yakifungwa na Matheo Anthony.

Mayanga aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwamo za Stand United ‘Chama la Wana’, Ndanda, Simba, KMC na Mtibwa Sugar, ni miongoni mwa washambuliaji wanaotegemewa ndani ya kikosi hicho cha Mbeya City msimu huu katika mashindano mbalimbali.


SALEHE KARABAKA VS NAMUNGO

Kiungo mshambuliaji huyu wa JKT Tanzania, aliiokoa timu hiyo na kipigo baada ya kufunga bao la dakika ya 90, Oktoba 19, 2025, likiwa ni la kusawazisha dhidi ya Namungo aliyowahi kuichezea.

Karabaka anayeichezea JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, msimu uliopita aliichezea Namungo kwa mkopo pia, ambapo aliinyima ushindi timu aliyoichezea, baada ya ‘Wauaji wa Kusini’, kupata bao kupitia, Ali Salehe Machupa dakika ya 39.

Kiungo huyo tangu ajiunge na Simba dirisha dogo la Januari 2024, akitokea JKU ya visiwani Zanzibar, amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza, jambo lililomfanya atolewe kwa mkopo Namungo na sasa yuko kwa maafande wa JKT Tanzania.

Msimu huu umekuwa ni mzuri kwa nyota huyo kwani tayari ameshafunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara hadi sasa, akiwa ndiye kinara sambamba na mshambuliaji mwenzake wa JKT Tanzania, Paul Peter, aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Dodoma Jiji.


KELVIN NASHON VS SINGIDA BS

Kiungo mkabaji, Kelvin Nashon alikuwa mwiba mkali kwa waajiri wake wa zamani Singida Black Stars, baada ya kuifungia Pamba Jiji bao la kusawazisha dk50 na mechi hiyo kuisha kwa sare ya 1-1.Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Novemba 8, 2025, Singida ilitangulia kupata bao dk31, likifungwa na Clatous Chama, kabla ya Nashon kusawazisha na kugawana pointi mojamoja.

Nashon aliyewahi kucheza Geita Gold, huku akiwaingiza vitani mara kwa mara vigogo wa soka nchini Yanga na Simba kuhitaji saini yake, msimu uliopita aliichezea Singida, japo kwa sasa yuko Pamba.


WILSON NANGU VS JKT TZ

Beki wa kati, Wilson Nangu anaingia katika rekodi ya nyota waliozifunga timu walizochezea, ambapo msimu huu amefunga bao moja dhidi ya JKT Tanzania aliyowahi kuichezea pia, katika ushindi wa Simba wa mabao 2-1, Novemba 8, 2025.

Nangu aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania, alifunga bao hilo dk63, likiwa ni la kusawazisha kwa timu hiyo baada ya Edward Songo kuwatanguliza maafande dk60, huku Jonathan Sowah akifunga la pili dakika ya 76.

     

Nyota huyo ameonyesha kiwango kizuri akiwa na Simba na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kwa mara ya kwanza, Nangu alijiunga na JKT Tanzania msimu wa 2023-2024, akitokea kikosi cha TMA cha jijini Arusha kinachoshiriki Ligi ya Championship kwa sasa.