ELIZABETH ILANDA; Riadha ilivyombadilishia maisha, anapiga mzigo, kusoma Marekani
Muktasari:
- Katika mandhari hayo ya kawaida kabisa, kulikuwa na msichana mmoja aliyekimbia zaidi ya wengine, si kwa sababu ya mashindano, bali kwa sababu moyo wake ulimwambia akimbie.
KULIKUWA na asubuhi za ukungu mzito kijijini Lighwa, wilayani Ikungi, mkoani Singida, Jogoo akiwika, ng’ombe wakitoka zizini na watoto wakikimbia barabarani peku bila viatu kwenda shuleni.
Katika mandhari hayo ya kawaida kabisa, kulikuwa na msichana mmoja aliyekimbia zaidi ya wengine, si kwa sababu ya mashindano, bali kwa sababu moyo wake ulimwambia akimbie.
Hakujua kuwa siku moja mbio hizo zingempeleka maelfu ya kilomita kutoka kijiji chake hadi viwanja vya kisasa vya Marekani.
Huyo ndiye Elizabeth Boniphace Ilanda (21), mtoto wa mchungaji, dada, mwanafunzi na mwanariadha anayechipukia kwa kasi duniani.
Safari yake si hadhithi ya bahati, ni ya jasho, machozi, majeraha, maneno ya kukatisha tamaa, lakini zaidi ni ya Imani. Imani ya kuwa msichana wa kijijini anaweza kuota na ndoto yake ikawa tiketi ya maisha mapya.
Hii leo, jina lake linaanza kutajwa sambamba na nyota wa riadha Tanzania, lakini nyuma ya mwanga huo, kuna giza la mapambano makubwa aliyoyapitia.
MWANZO WA NDOTO
Safari yake ya riadha ilianzia kijijini na alikuwa akikimbia tu kwa kujifurahisha kama kufanya mazoezi bila kujua siku moja riadha inaweza kuja kubadilisha maisha yake.
“Nilianza kukimbia tu kama mazoezi ya kawaida, sikujua riadha inaweza kuwa kazi au kunipeleka mbali, nilikuwa nakimbia kwa kujifurahisha tu”.
Anaongeza kwa wakati huo akiwa anasoma shule ya msingi Ligwa, alikuwa anapenda michezo hasa wa kukimbia lakini kwake ilikuwa ni kama kuweka mwili sawa na kuiwakilisha shule yake na kuiletea heshima nzuri.
KUPENDA RIADHA
Anasema alichagua riadha na siyo michezo mingine kutokana na mafanikio yake na aliyaona kwa dada yake aliyekuwa anakimbia mbio za uwanjani mita 800 na 1500.
Anasema alivutiwa sana kwa sababu alikuwa anasafiri nchi mbalimbali kama China, Botswana na nyingine nyingi, akiiwakilisha Tanzania, pia mafanikio ya kaka zake, Epimack Ilanda na Alphonce Simbu nayo yalimfanya aone mchezo huo unaweza kubadilisha maisha na kukufanya utimize ndoto zako.
“Nilimwona dada yangu akisafiri, nilijiuliza kwa nini mimi nisiwe kama yeye? Nikasema nitakimbia na siku moja nitabadilisha maisha yangu”.
“Mafanikio ya Simbu nayo yalinisukuma sana, nikasema kama ndugu zangu wanapambana hivi kutimiza ndoto kutokana na riadha kwa nini na mimi nisiwese”.
KIPAJI SHULENI
Elizabeth anasema kipaji chake kilioneka shule ya msingi Lighwa kupitia kwa mwalimu maarufu wa michezo mkoani Singida, mwalimu Jambau ambaye amewaibua nyota wengi akiwemo bingwa wa medali ya dhahabu ya marathoni ya dunia mwaka 2025, Alphonce Simbu na bingwa wa taifa wa nusu marathoni kwa upande wa wanawake, Jackline Sakilu.
Anasema shuleni, macho ya mwalimu huyo yaliona kitu tofuati, mwendo wake ulikuwa mwepesi, pumzi yake ndefu na moyo wake wa kupambana na kuona hapa kuna staa mwingine ajae.
Anasema baada ya kumaliza shule ya msingi alijiunga na shule ya michezo ya Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani, shule iliyompa mwelekeo wa kitaaluma na kimichezo kwa pamoja.
“Hapo ndipo nilijua sasa hiki si kipaji cha kawaida, nilianza kufundishwa kitaalamu, ndoto ikaanza kuwa halisi”.
ARUSHA HADI MAREKANI
Baada ya kumaliza masomo, nyota huyo alikwenda mkoani Arusha, ambako kuna sehemu nzuri ya kufanyia mazoezi na wanariadha wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje hupatumia.
Anasema alianza kukimbia kama mwanariadha wa kulipwa kwa mbio za Km10 na Km5 na alianzia NBC Marathon, Tulia Marathon, Msoga Marathon na nyingine nyingi na yote alifanya vizuri na fedha na zawadi alizopata zikaanza kubadili maisha yake.
Anasema pia alipata ufadhili wa masomo katika chuo cha michezo cha Odessa College kilichopo Texas, Marekani na baadaye akahamia Clemson University, ambako sasa anasomea masuala ya afya huku akiendelea na taaluma yake ya kukimbia.
“Riadha imenipeleka darasani Marekani, bila michezo, nisingefika hapa, hii ni Baraka kabisa”.
REKODI BINAFSI MAREKANI
Akiwa Marekani anaendelea kufanya vizuri zaidi na amekusanya pointi nyingi za ubora wa kiwango cha kimataifa (performance points), huku akijiwekea rekodi yake binafsi katika mbio mbalimbali za viwanjani vya ndani (indoor) na nje (outdoor).
Rekodi hizo ni mita 3000 (ukumbi/short track), dakika 9:11.79 (pointi 1088), Mile 1 (short track), dakika 4:50.73 (pointi 1002), mita 5000 (short track), dakika 16:39.09, Mita 1500 (nje/outdoor), dakika 4:31.39 (pointi 966) na mita 10,000 (nje/outdoor), dakika 35:32.01 (pointi 959).
Rekodi hizo binafsi zinamweka kwenye ramani ya wanariadha wa kiwango cha juu vyuoni Marekani na anaendelea pia kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
KUIWAKILISHA TANZANIA
Elizabeth amewahi kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ya vijana Uganda, pia mwaka huu 2026 alikuwa ni miongoni mwa wanariadha ambao waliiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia ya mbio za nyika ambazo zilifanyika nchini Marekani, nahodha wa timu akiwa ni mashindi mara mbili mfululizo wa mbio za Daegu marathoni za nchini Korea Kusini, 2025, 2026, Gabriel Geay.
“Kuvaa bendera ya Tanzania kifuani ni kitu kinachonipa nguvu kuliko chochote, unakimbia siyo kwa ajili yako, unakimbia kwa taifa”.
CHANGAMOTO
Anasema safari yake ya mafanikio katika riadha haikuwa rahisi na aliwahi kukatishwa tamaa baada ya kuumia na kukaa nje kwa miaka mingi.
Anasema watu walimshauri aachane na riadha wakiamini hataweza kurejea na kufanya vizuri, ukizingatia pia ni mtoto wa kike.
“Kuna watu wengine huwa wapo kwa ajili ya kuwakatisha tamaa watoto wa kike wakiamini hatuwezi kufanikiwa kwenye michezo, nahisi wao nia yao wanataka kutuona jikoni na siyo kwenye uwanja wa mapambano wa mafanikio.”
“Watu waliniambia niache, lakini mimi tayari nilishaona matunda ya riadha, nilijua nikirudi, nitarudi nikiwa bora zaidi, nikaziba masikio na ndiyo maana leo niko Marekani nasoma huku nakimbia kwa sababu ya uvumilivu”.
FAMILIA NGUZO YAKE
Anasema miongoni mwa vitu ambavyo vimemfanya afanikiwe kwa kiasi chake hadi sasa kwenye riadha ni pamoja na baba yake ambaye ni mchungaji, hivyo maadili, sala na sapoti vimekuwa silaha yake siku zote na katika kila anachokifanya kwanza anamtanguliza Mungu.
Anasema tofauti na kwengine ingeonekana mtoto wa kike na wa mchungaji anakimbia, ila kwa wazazi wake walikuwa wanamtia moyo anaweza na siku moja atakuwa mwanariadha mkubwa hapa nchini na hasa kutokana na mafanikio aliyoyaona kwa ndugu zake waliopita na kutambua na kuthamini kipaji cha mtoto wao.
“Baba yangu alikuwa ananiambia, endelea kupambana, Mungu ataifungua njia, maneno hayo yalinibeba sana, pia ndugu zangu hawakuniacha, walinipa sapoti ambayo imenifanya leo niko hapa.”
Anaongeza pia kaka yake Alphonce Simbu amekuwa ni mshauri mkubwa sana kwa upande wake katika kila jambo, kuhakikisha anamtia moyo ili asome huku akipambania kutimiza ndoto pia kupitia miguu yake kwa maana ya kufanya vizuri kwenye riadha.
MAISHA YAMEBADILIKA
Anasema japo ni binti mdogo wa miaka 21 tu lakini riadha imebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa sana, kwani amepata nafasi ya kusoma shule nzuri kama Filbert Bayi, pia amekutana na viongozi wakubwa mashuhuri wa Tanzania pamoja na kupata ufadhili wa kimasomo Marekani.
“Mimi kwa sasa maisha yangu ni riadha, nikiwa Tanzania nilikuwa nakimbia napata pesa, nakaa meza moja na watu ambao hata sikuwahi kufikiria kukutana nao na hata sasa hapa nilipo ni kwa sababu ya riadha.”
RIADHA KAMA AJIRA
Anatoa ujumbe kwa wasichana ambao wana vipaji vya michezo kusimama kidete na kuvipambania ili kuja kuishi vizuri kama mastaa na kuiwakilisha nchi kimataifa, huku wakijua pia kuna kukatishwa tamaa na jamii na hata viongozi, lakini wanachotakiwa ni kujitambua wewe ni nani na unataka ufikie wapi na kipaji chako.
“Kukatishwa tamaa ipo lakini kama ukiziba masikio na kupambana lazima utatimiza ndoto zako, mimi kama ningesema niache riadha leo hii ningekuwa kwetu Ikungi nalima, lakini nilisimama kidete na kupambania ndoto zangu.”
“Japo bado sina jina kubwa kama walivyo wanariadha wengine wa kike Tanzania, lakini naamini miaka ijayo na mimi nitakuwa miongoni mwa majina makubwa yanayotamkwa kila kona.”
“Michezo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, msione aibu, msione kama ni ya wavulana, inaweza kubadilisha maisha yenu kabisa.”
WITO KWA SERIKALI, WAZAZI
Anaomba serikali kuongeza uwekezaji kwa watoto wa kike, ikiwezekana kuwe na programu ya kuchukua wasichana wenye vipaji vya michezo mbalimbali kwa kupitia michezo ya shule, pia hata wale wa vijijini ambao miundombinu inafanya wasionekana wafikiwe ili kuwapata wengi ambao watakuja kuiwakilisha nchi kimataifa.
“Vipaji vipo vingi sana vijijini, wapewe nafasi tu, pia wazazi wasiwazuie watoto wao kwani michezo inaweza kuwafungulia dunia.”
NDOTO KUBWA OLIMPIKI
Nyota huyo anasema ndoto yake kubwa katika riadha ni kuvunja rekodi ya taifa ya mbio za mita 3000 na 5000, pia kuiletea Tanzania medali ya dunia na kushinda medali ya Olimpiki, akiamini kutokana na ubora wake na jitihada ambazo anaendelea nazo ipo siku atafanikiwa kutimiza ilo.
“Nataka siku moja Tanzania isimame kwenye jukwaa la dunia na wimbo wa taifa uimbwe kwa sababu yangu.”