Prime
Eeeh buana Simba mpya ina jipya pia
SIMBA imemaliza mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa bao 1-0 mbele ya Stade Malien ya Mali na kulipa kisasi cha kipigo ilichopewa ugenini mwishoni mwa mwaka jana, japo imesalia mkiani mwa msimamo wa Kundi D ikiwa ni mara ya kwanza kwake kumaliza mkiani tangu ianze kushiriki CAF tangu 2018.
Ushindi huo ulioifanya Simba kufikisha pointi tano kupitia mechi sita ukiwa ni wa kwanza kwa msimu huu nyumbani katika michuano ya Afrika, ni wa kwanza pia katika hatua ya makundi.
Simba ilishacheza mechi nne za Ligi hiyo NYUMBANI kwa msimu huu, zikiwamo mbili za hatua ya awali zilizoisha kwa sare tofauti, kisha kupoteza mechi ya kwanza ya makundi mbele ya Petro Atletico ya Angola kabla ya kutoka sare ya 2-2 na Esperance ya Tunisia na juzi kujipata Kwa Mkapa.
Hapa chini ni dondoo kwa uchache namna Simba ilivyozinduka mwisho wa msimu wa michuano hiyo ikishindwa kwenda robo fainali kwa mara ya kwanza tangu ilipocheza hatua ya makundi 2003.
INAJIPATA MDOGO MDOGO
Simba iliendelea kuonyesha mabadiliko ya ubora uwanjani katika mechi hiyo. Ilitawala vizuri ikicheza kwa kasi na kufanikiwa mapema tu kupata bao hilo la pekee katika dakika ya pili, likiwekwa kimiani na kiungo mshambuliaji mpya, Anicet Oura.
Bahati mbaya sana kwa mashabiki wa Simba ni kwamba wameanza kushuhudia kuimarika kwa kikosi chao wakati ambao timu hiyo imeshaaga michuano, kwani kama mechi zingekuwa bado zipo huenda habari ingekuwa nyingine kwa jinsi timu inavyocheza kulinganisha na mechi zilizopita.
POINTI TANO MKIANI
Ushindi wa juzi umeifanya Simba kufikisha pointi tano kupitia mechi sita, ikipata sare mbili na kupoteza tatu, ikifunga jumla ya mabao matano, ikiburuza mkia wa msimamo wa Kundi D lililoongozwa na Malien kama kinara ikiwa na pointi 11, ikifuatiwa na Esperance yenye pointi tisa, huku zote zikienda robo fainali.
Petro Atletico ilimaliza ya tatu kwa pointi sita na Simba ikiwa mkiani, timu hizo mbili zikiaga michuano na sasa zitakuwa watazamaji wakati wababe wanane watakapokuwa wakianza msako wa ubingwa kwa msimu huu, ambapo droo ya mechi za hatua zinazofuata itafanyika kesho Jumanne.
MBELE MABAO BADO
Katika mechi ya juzi, Simba ingeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wa timu hiyo uliwaangusha kwa kushindwa kutumia nafasi ilizotengeneza hasa kwa Seleman Mwalimu 'Gomes' na Elie Mpanzu, kwani walikosa utulivu kumalizia mipira wavuni.
Eneo la kati la Simba linazidi kuimarika ambapo viungo wake wanaonyesha kuwa na nguvu ya kusukuma mashambulizi lakini pia ukabaji ukifanyika vyema.
MPANZU KUNANI?
Mpanzu bado ni mchezaji anayehitajika Simba, lakini kitu anachotakiwa kufanya ni kupunguza kukaa na mpira wakati wenzake wameshajiweka kwenye maeneo mazuri kuharakisha mashambulizi.
Anachofanya Mpanzu ni kama kinaichelewesha Simba kutengeneza mabao mengi zaidi, hatua ambayo pengine ilichangia atolewe katika dakika ya 69 baada ya kuchelewesha shambulizi la haraka katika dakika ya 65 wakati wenzake walishakaa maeneo sahihi.
OURA TISHIO
Kama kuna silaha ambayo Simba imeiongeza kwenye timu hiyo basi ni winga Oura ambaye wepesi wake, kasi yake na akili yake vimeiongezea Simba nguvu kubwa kwenye eneo la kiungo kwenda mbele.
KASALLI SIMBA IKO SALAMA
Kipa Djibrilla Kasali ameonyesha hakuna wasiwasi kwa Simba akiwa langoni ambapo dakika ya 69 alifanya kazi nzuri ya kupangua kwa ubora shuti la mshambuliaji Taddeus Nkeng ambalo kama si vidole vya kipa huyo lingekuwa bao zuri la kusawazisha.
Kasali anaendelea kuonyesha pia hesabu zake nzuri akiwa na ujuzi wa kuwapanga mabeki wake ili kuhakikisha wapinzani hawakamilishi kwa ubora mashambulizi yao.
KIBABAGE NA MASHABIKI SIMBA
Kuna kosa moja kubwa alilolifanya beki Nickson Kibabage kwenye shambulizi hilo la Nkeng, ambapo alitaka kuupiga mpira kwa nyuma tena akiwa eneo la hatari, bahati nzuri golini kwake Kasali alikuwa amesimama imara.
Kilichofurahisha ni kwamba baada ya kosa hilo Kibabage alifanya kitu cha haraka akiinua mikono yake juu akiwaomba radhi mashabiki ambao nao kwa haraka walionyesha uungwana kwa kumpigia makofi kwa hatua alizochukua.
BARKER KAZI HAPA
Kocha wa Simba, Steve Barker anatakiwa kuongeza mkazo kwenye kuiboresha safu yake ya ushambuliaji ambayo bado inaonekana kuna mambo ya kiufundi yanatakiwa kusukwa ili Simba iweze kutengeneza ushindi mkubwa zaidi.
Msimamo Kundi D