Devota Kihwelo: Nilisajiliwa kwa jezi ya Chelsea
Muktasari:
- Lakini safari yake haikuanzia kwenye kuhoji watu mbalimbali ilianzia kwenye vumbi la Kariakoo na Temeke, akicheza soka la ‘chandimu’ na wavulana huku akiwa na ndoto za kuwa nyota wa soka duniani.
Katika tasnia ya habari nchini, jina la Devotha Kihwelo limejijengea heshima kama mwandishi shupavu wa habari za uchunguzi na michezo. Lakini safari yake haikuanzia kwenye kuhoji watu mbalimbali ilianzia kwenye vumbi la Kariakoo na Temeke, akicheza soka la ‘chandimu’ na wavulana huku akiwa na ndoto za kuwa nyota wa soka duniani.
HISTORIA YAKE
Devotha alizaliwa kwenye ukoo wa soka ambapo baba yake mkubwa, Julio Kihwelo, ni kocha wa Mashujaa FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara, lakini mapenzi yake na soka yalianzia mtaani Kariakoo kati ya 1999-2002 ambapo alikuwa akicheza soka na wavulana.
Mwaka 2002, familia ilihamia Temeke akalazimika kuweka kando mpira ili kumaliza masomo ya elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Temeke.
Anasema akiwa kidato cha pili 2004 ilitokea fursa ya michuano ya shule iliyofanyikia Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam iliyomkutanisha na rafiki yake wa zamani, Fatma Rajabu, ambaye alikuwa mchezaji aliyemshawishi kujiunga na Klabu ya Tanzanite na hapo ndipo safari ilipoendelea katika soka.
“Nilikuwa nacheza na wavulana tu tena sikuwa najua sana, lakini nikipelekwa kwenye mashindano nacheza vizuri tu labda kitakachoniangusha ni ufiti tu,” anasema.
ISHU YA UMRI
Kumekuwa na tetesi kuwa baadhi ya wachezaji wanadanganya umri na hapa Devotha anaeleza ilibidi adanganye umri ili aweze kushiriki mashindano ya East African Competition iliyokuwa inahitaji mabinti chini ya miaka 14.
Devotha, akiwa tayari ameshavuka umri huo, alilazimika kutumia ujanja. “Tulichokifanya kwa sababu nilikuwa nahitaji kushiriki mashindano tulipiga kopi ya cheti cha kuzaliwa cha mdogo wangu wa mwaka 1992 tukahariri umri ukaonekana unafanana.”
Hilo linayoonyesha uhalisia wa soka la vijana, presha ya ushindani na ukosefu wa mifumo sahihi ya kukuza vipaji.
NILISAJILIWA KWA JEZI YA CHELSEA
Hii ndiyo sehemu inayobeba kichwa cha simulizi yake, Mwaka 2009, alijiunga na Evergreen ya Temeke tofauti na sasa hivi wachezaji wanasajiliwa kwa fedha kubwa na mishahara kwake hakukuwa na pesa wala mkataba bali jezi ya Chelsea.
"Kipindi hiko hata ligi bado hakuna kwa hiyo ilikuwa bado kabisa, wakati huo ukisajiliwa unapelekwa kwenye timu unacheza tu hakuna chochote," anasema Devotha na kuongeza
“Niliposajiliwa nikamwambia kiongozi aninunulie hata jezi wakati ule ilikuwa inauzwa 12,000, Niliona bora hiyo jezi kuliko kukosa kabisa,” anaongeza.
MAMBO YA USHIRIKINA
Anasema suala la mambo ya ushirikina yapo kwenye michezo hususani soka na baadhi ya timu zimekuwa zikiamini mambo hayo ili kupata ushindi.
"Kabla ya mechi moja ya ligi ya mkoa, timu yetu ilipewa ulinzi wa ajabu.Tuliambiwa tuweke vijiti miguuni tukavunja nazi njiani hadi uwanjani,” anasema Devotha na kueleza
"Tulipoingia uwanjani tulifungwa mabao 14-1 na tulistahili kwa kuwa wachezaji hatukulenga kile tulichofundishwa akili ikarudi kwenye mambo ya ushirikina."
KUJIWEKA KIUME
Kwa hapa Tanzania kumekuwa na mtindo wa wachezaji wengi wanawake kuvaa na kujiweka kiume tofauti na Ulaya ambako wachezaji wa kike wanavaa kama wanawake wa kawaida.
Devotha anahadithia kuwa hata yeye wakati anacheza mpira alikuwa hivyo kuanzia mavazi alivaa traki za kike.
“Nilikuwa sipendi kabisa magauni wala mambo ya saluni… kujiremba mimi nguo zangu zilikuwa traki muda wote na nilikuwa najiona kawaida tu,” anasema.
Anaongeza kadri muda ulivyopita alianza kubadilika baada ya rafiki yake Fatma kumshawishi kujiweka wa kike.
"Nilikuwa sioni tofauti ila Fatma alikuwa na mwanaume wake kwa hiyo alikuwa hapendi kujiweka kama mwanaume alikuwa anajipamba akiingia uwanjani hiyo ikaanza kunibadilisha kidogo kidogo,"
"Alikuwa akinisisitiza sana wewe ni mwanamke na unapaswa kuvaa kama wengine na sio kubadili muonekanao wako hata kama unacheza mpira, nafikiri hata kwa wengine labda kwa sababu ya asili ya mchezo wenyewe ndio maana wanajiweka hivyo."
UANDISHI
Baada ya kuacha soka, alijikita kwenye masomo na kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari TSJ (2011-2013). Baada ya kumaliza masomo alianza kazi Tanzania Daima (2013) akiripoti habari za polisi na mahakamani.
“Nilijua bado nina mapenzi na michezo, kucheza niliacha kwa sababu haikunilipa ndio maana nikaachana na mpira lakini wapo wenzangu waliokomaa hadi leo wametoboa wakina Mwanahamis Omary na wengineo," anasema
"Ila sikutaka kuacha kabisa nikaona kuna fursa kwenye kuandika ndio nikaona nisomee lakini awali sikuanza kuandika habari za michezo nilianzia polisi."
ANAVYOLIONA SOKA LA WANAWAKE
Akiwa na leseni ya ukocha, Devotha anasema bado hakuna usawa kwenye timu za wanawake kwani makocha wanaume wanapewa nafasi kubwa hadi kwenye timu za taifa.
“Unakuta timu za wanawake zinafundishwa na wanaume wakati wanawake wapo na sio kwamba makocha wanawake hamna kocha mmoja anafundisha timu za wanawake zote sasa hapo unawajengea nini makocha wengine,” anasema.
MIPANGO YAKE
Baada ya miaka kadhaa ya kazi, Devotha ana mpango wa kustaafu kuandika.“Nafikiria ifikapo 2028 niachane na uandishi kabisa,” anasema.
Anataka kujikita kwenye biashara na maisha binafsi na nje ya uandishi, Devotha ni mwanamke mjasiriamali. Ni msusi na mtaalamu wa makeup, ujuzi alioupata baada ya kusomea 2020/21.
"Mimi nimefanya vitu vingi sana kwenye harakati za kujitafuta nilisomea hadi mambo ya kupamba watu 'makeup' lakini ndio hivyo tena."
Anasema kwenye harakati zote za kujitafuta angalau uandishi umemlipa kwani amefanikiwa kuwa mhimili wa familia yake, akiwa msemaji na mshauri mkuu anayesaidia ndugu zake kwa mawazo na fedha.