Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Canada kusaka ushindi wa kwanza Kombe la Dunia

CANADA Pict

Muktasari:

  • Davies, 25, alikumbwa na jeraha hilo wakati wa mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Bayern Munich ilifungwa na Paris Saint-Germain. Hata hivyo, benchi la ufundi linaamini nyota huyo atakuwa tayari kucheza sehemu ya mashindano hayo makubwa ya dunia.

TORONTO, CANADA: NYOTA wa Bayern Munich, Alphonso Davies amejumuishwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 wa timu ya taifa ya Canada kitakachoshiriki Kombe la Dunia 2026, licha ya kuwa bado anaendelea kuuguza majeraha ya msuli wa paja.

Kocha mkuu wa Canada, Jesse Marsch ametangaza kikosi hicho na kukielezea ndiyo timu bora zaidi kuwahi kuundwa katika historia ya soka la nchi hiyo.

Davies, 25, alikumbwa na jeraha hilo wakati wa mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Bayern Munich ilifungwa na Paris Saint-Germain. Hata hivyo, benchi la ufundi linaamini nyota huyo atakuwa tayari kucheza sehemu ya mashindano hayo makubwa ya dunia.

Mbali na Davies, Canada pia imemjumuisha mshambuliaji hatari wa Juventus, Jonathan David ambaye anatarajiwa kuwa mmoja wa silaha muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Wachezaji wengine waliopata nafasi katika kikosi hicho ni kiungo Stephen Eustaquio anayekipiga Porto, Tajon Buchanan wa Villarreal, mshambuliaji Tani Oluwaseyi pamoja na nyota wa Southampton, Cyle Larin.

CANA 01

Akizungumza baada ya kutangaza kikosi hicho, Marsch anasema ana imani kubwa na uwezo wa wachezaji wake licha ya baadhi yao kutokuwa katika kiwango cha asilimia 100 kutokana na majeraha yaliyowasumbua katika kipindi cha karibuni.

"Tuna kundi bora zaidi la wachezaji 26 ambalo Canada imewahi kuwa nalo kwa wakati mmoja. Si wote ambao wako katika utimamu wa asilimia 100 kwa sasa lakini wengi wao wako karibu kufikia kiwango hicho," anasema Marsch.

Kauli hiyo pia ilionekana kuonyesha kutoridhishwa kwake na maswali ya mara kwa mara kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu hali za kiafya za baadhi ya nyota wake. Davies yupo mbioni kurejea uwanjani kabla ya mchezo wa ufunguzi wa Canada dhidi ya Bosnia na Herzegovina utakaopigwa Juni 12.

Nyota huyo amekuwa akipambana na changamoto za majeraha tangu aliporejea kutoka katika majeraha makubwa ya goti yaliyomweka nje kwa takribani miezi minane.

Kocha huyo anasema mchakato wa kuchagua kikosi ulijikita zaidi katika kutathmini hali za kiafya za wachezaji na uwezo wao wa kufikia kiwango bora kabla ya kuanza kwa mashindano.

"Tulikuwa tayari tunafahamu msingi wa kikosi chetu kwa muda mrefu. Kilichokuwa muhimu ni kujua ni nani atakuwa na afya nzuri na nani atakuwa karibu na kiwango chake bora wakati wa mashindano," anasema.

Anaongeza ana matumaini makubwa kutokana na maendeleo mazuri ya baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi, akisisitiza timu itakuwa imara zaidi kadri mashindano yatakavyoendelea.

"Huenda si kila mchezaji atakuwa tayari kwa asilimia 100 katika mchezo dhidi ya Bosnia, lakini tutakuwa na kikosi imara kitakachoweza kuanza mashindano kwa nguvu. Tunaamini pia tutazidi kuwa bora kadri Kombe la Dunia litakavyoendelea," anaongeza.

Canada itakuwa moja ya nchi tatu wenyeji wa Kombe la Dunia 2026 pamoja na Marekani na Mexico. Kutokana na hadhi hiyo, timu hiyo itacheza mechi zake zote za hatua ya makundi nyumbani.

Baada ya mchezo wa ufunguzi dhidi ya Bosnia na Herzegovina mjini Toronto, Canada itavaana na Qatar pamoja na Uswisi katika michezo itakayofanyika mjini Vancouver.

Canada bado haijawahi kushinda mchezo wowote katika historia ya ushiriki wake wa Kombe la Dunia, jambo ambalo linaifanya michuano ya mwaka 2026 kuwa fursa muhimu ya kuandika historia mpya mbele ya mashabiki wake wa nyumbani.

Kombe la Dunia 2026 litakuwa la kwanza kushirikisha timu 48 badala ya 32 zilizokuwa zikishiriki hapo awali. Mashindano hayo yataanza Juni 11 na kufikia tamati Julai 19 huku yakitarajiwa kuwa makubwa zaidi katika historia ya soka duniani.

CANA 02

FULL MZIKI

Makipa: Dayne St Clair (Inter Miami), Maxime Crepeau (Orlando City), Owen Goodman (Crystal Palace).

Mabeki: Alistair Johnston (Celtic), Derek Cornelius (Marseille), Richie Laryea (Toronto), Niko Sigur (Hajduk Split), Joel Waterman (Chicago Fire), Luc de Fougerolles (Fulham), Moise Bombito (Nice), Alphonso Davies (Bayern Munich), Alfie Jones (Middlesbrough).

Viungo: Stephen Eustaquio (Porto), Ismael Kone (Sassuolo), Tajon Buchanan (Villarreal), Mathieu Choiniere (Los Angeles FC), Ali Ahmed (Norwich City), Nathan Saliba (Anderlecht), Liam Millar (Hull City), Marcelo Flores (Tigres UANL), Jacob Shaffelburg (Toronto), Jonathan Osorio (Toronto).

Washambuliaji: Jonathan David (Juventus), Cyle Larin (Southampton), Tani Oluwaseyi (Villarreal), Promise David (Union SG).

CANA 03

HII NDIYO CANADA

Soka lilianza kushika kasi Canada mwishoni mwa karne ya 19 huku vyama vya Dominion Football Association kilichoanzishwa mwaka 1877 na Western Football Association (WFA) mwaka 1880 vikiongoza maendeleo ya mchezo huo kabla ya kuanzishwa kwa Chama cha Soka cha Canada kinachotambulika leo.

Mwaka 1885 uliandika ukurasa muhimu katika historia ya soka la Canada baada ya WFA kutuma kikosi chake kwenda New Jersey, Marekani, kucheza dhidi ya timu iliyoandaliwa na American Football Association, ambayo wakati huo ilikuwa ikisimamia mchezo huo Marekani.

Katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa Novemba 28, 1885 kwenye Uwanja wa Clark Field, Canada ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Marekani na kuweka historia ya ushindi katika moja ya mechi za mwanzo kabisa za kimataifa kati ya mataifa hayo mawili. Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye Marekani ilijibu mapigo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa marudiano.

Mwaka 1888, Canada iliendelea kutangaza soka lake kimataifa baada ya timu iliyowakilisha WFA kufanya ziara katika Visiwa vya Uingereza. Katika safari hiyo, Canada ilicheza mechi 23 na kupata ushindi mara tisa, sare tano na kupoteza michezo tisa. Kikosi hicho kilikuwa na wachezaji 16 waliozaliwa Canada huku David Forsyth pekee akiwa mzaliwa wa nje ambaye alihamia Canada akiwa mtoto mchanga.

CANA 04

REKODI INATAFUTWA

Canada itakuwa inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tatu katika historia yake baada ya kufuzu kucheza michuano hiyo mwaka 1986, 2022 na sasa 2026 na ni moja ya wenyeji wa mashindano hayo pamoja na Marekani na Mexico.

Licha ya kuwa moja ya mataifa makubwa katika ukanda wa CONCACAF kwa sasa, Canada bado haijawahi kuvuka hatua ya makundi katika historia yake ya Kombe la Dunia.

Mara ya kwanza kwa Canada kucheza Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1986 nchini Mexico. Katika mashindano hayo ilipangwa kundi moja na Ufaransa, Hungary pamoja na Umoja wa Soviet.

Hata hivyo safari yao haikuwa nzuri baada ya kupoteza mechi zote tatu. Ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Ufaransa kabla ya kuchapwa mabao 2-0 na Hungary, kisha ikamalizia kwa kupoteza tena mabao 2-0 dhidi ya Soviet na kuondolewa mapema katika hatua ya makundi bila kufunga bao hata moja.

CANA 05

Baada ya kusubiri kwa miaka 36, Canada ilirejea tena kwenye Kombe la Dunia mwaka 2022 Qatar ikiwa na kizazi kipya cha nyota wakiongozwa na Alphonso Davies na Jonathan David. Timu hiyo ilipangwa kundi moja na Ubelgiji, Croatia pamoja na Morocco katika moja ya makundi magumu zaidi ya mashindano hayo.

Katika mchezo wake wa kwanza, Canada ilionyesha soka la kuvutia lakini ilifungwa bao 1-0 na Ubelgiji baada ya kukosa nafasi kadhaa muhimu ikiwemo penalti ya Alphonso Davies. Licha ya kupoteza, kiwango walichoonyesha kilisifiwa na mashabiki wengi wa soka duniani kutokana na namna walivyocheza kwa kujiamini dhidi ya timu iliyokuwa miongoni mwa vigogo wa dunia.

Mchezo wa pili dhidi ya Croatia uliandika historia kwa Canada baada ya Alphonso Davies kufunga bao la kwanza kabisa la nchi hiyo katika historia ya Kombe la Dunia. Hata hivyo furaha hiyo haikudumu kwa muda mrefu kwani Croatia ilirejea mchezoni na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1. Katika mchezo wa mwisho wa kundi, Canada ilifungwa mabao 2-1 na Morocco na hivyo kumaliza mashindano bila kupata pointi hata moja.

Kwa jumla, Canada imecheza jumla ya mechi sita za Kombe la Dunia katika historia yake na imepoteza zote sita. Sasa macho ya mashabiki wake yanaelekezwa kwenye Kombe la Dunia 2026 wakiamini kizazi cha sasa kinaweza kuipa nchi hiyo ushindi wake wa kwanza wa kihistoria na labda kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.