Prime
CAF chimbo la Simba, Yanga kuvuna mabilioni
SIRI ya Yanga na Simba kupigania vikumbo kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mabilioni ya fedha wanazopata kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika utafiti uliofanywa na Mwanaspoti umebaini katika kipindi cha kuanzi msimu 2018/19 hadi sasa Yanga na Simba mafanikio yao katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, klabu hizo mbili zimeingiza jumla ya Dola8.725 milioni (takribani Sh23.6 bilioni), fedha ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha kuimarisha bajeti zao za uendeshaji na usajili.
Simba ndiye kinara kwa mapato hayo akiwa ameingiza Dola 5.15 milioni (zaidi ya Sh13.9 bilioni), huku Yanga ikikusanya dola 3.5 milioni (zaidi ya Sh9.7 bilioni) kupitia ushiriki wake katika mashindano hayo.
MKWANJA WA SIMBA
Safari ya Simba ya mafanikio ilianza katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19 walipofika robo fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi wakiwa chini ya Patrick Aussems.
Simba, ikiwa na pointi tisa, ilimaliza ya pili katika Kundi D nyuma ya Al Ahly kabla ya kukutana na TP Mazembe ya DR Congo katika robo fainali na kuondolewa kwa jumla ya mabao 4-1. Kufika hatua hiyo kuliipa Simba Dola 650,000 ( zaidi ya Sh1.76 bilioni) kutoka CAF.
Msimu wa 2020/21 Simba ilirejea tena robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza kinara wa Kundi A ikiwa na pointi 13 mbele ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Al Ahly.
Hata hivyo, safari yao ilisimamishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 4-3. CAF iliwazawadia tena Dola 650,000 (zaidi ya Sh1.76 bilioni) kwa kufika hatua hiyo.
Msimu wa 2022/23 Simba iliandika historia nyingine kwa kufika robo fainali na kukutana na Wydad Casablanca ya Morocco. Simba ilishinda mchezo wa kwanza Dar es Salaam kwa bao 1-0 kabla ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalti nchini Morocco baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika msimu huo Simba ilipata Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.43 bilioni) kufuatia ongezeko la fedha za zawadi za CAF.
Msimu wa 2023/24 Wekundu wa Msimbazi walifika tena robo fainali ambapo walikutana na Al Ahly ya Misri, mabingwa watetezi wa michuano hiyo. Simba iliondolewa baada ya kupoteza mechi zote mbili, nyumbani kwa bao 1-0 na ugenini kwa mabao 2-0. Kufika robo fainali kuliiingizia klabu hiyo Dola nyingine 900,000 (zaidi ya Sh2.43 bilioni).
Katika msimu wa 2025/26 Simba iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata Dola 700,000 (zaidi ya Sh1.89 bilioni).
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilifika robo fainali mwaka 2021/22 na kupewa Dola 350,000 (zaidi ya Sh945 milioni).
Mafanikio makubwa zaidi kwa Wekundu hao wa Msimbazi yalikuwa msimu wa 2024/25 walipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yao tangu mashindano hayo yaanze kuitwa kwa jina hilo.
Hata hivyo, walishindwa kutwaa ubingwa huo wakiwa chini ya kocha Fadlu Davids, ambaye kwa sasa ni kocha wa Raja Casablanca, baada ya kufungwa na RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1. Licha ya hivyo, walijihakikishia zawadi ya Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2.7 bilioni) kama washindi wa pili.
MAMILIONI YA YANGA
Kwa upande wa Yanga, mapato yao ya kwanza makubwa ya CAF katika miaka ya karibuni yalikuwa mwaka 2018 walipofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, hatua iliyowapa Dola 275,000 (zaidi ya Sh742.5 milioni).
Lakini mafanikio makubwa zaidi yalikuwa msimu wa 2022/23 walipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika chini ya kocha Nasreddine Nabi.
Katika fainali hiyo walikutana na USM Alger ya Algeria na kupoteza ubingwa kwa kanuni ya mabao ya ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2. Hata hivyo, Yanga ilivuna Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2.7 bilioni) kama mshindi wa pili.
Msimu wa 2023/24 Wananchi waliweka historia nyingine kwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika mfumo wa sasa wa mashindano. Waliondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini wakapata Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.43 bilioni).
Msimu wa 2024/25 na 2025/26 Yanga ilifika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika misimu yote miwili na kuvuna Dola 700,000 (zaidi ya Sh1.89 bilioni) kwa kila msimu.
NANI ANAONGOZA?
Kwa mujibu wa hesabu za zawadi za CAF katika misimu hiyo, Simba inaongoza kwa tofauti ya Dola 1.5 milioni (zaidi ya Sh4.25 bilioni) dhidi ya Yanga.
Tofauti hiyo imechangiwa zaidi na Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne ndani ya kipindi hicho pamoja na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/25.
Kwa pamoja, vigogo hao wa Tanzania wameingiza Dola 8,725,000 (zaidi ya Sh23.6 bilioni) kutoka CAF katika kipindi hicho, jambo linaloonyesha namna ambavyo mafanikio ya kimataifa yanavyozidi kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa klabu za Tanzania.