BROADIS: Mwanasoka aliyefariki akiacha ujumbe Kombe la Dunia apelekewe kaburini
Muktasari:
- Mwaka 2018 Broadis akiwa na umri wa miaka 97 alikuwa amepanga kwenda Russia kama timu ya England ingefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Dunia la 21 lililofanyika huko. Alichokuwa na hamu ya kukiona kwa mara ya pili katika uhai wake ni kuiona England ikibeba Kombe la Dunia. Wakati alipokuwa akiichezea timu hiyo hakufanikiwa.
HIVI sasa ni miaka saba tangu mmoja wa wanasoka maarufu wa England, Ivor Broadis, aiage dunia, lakini hivi karibuni habari zake zilitawala vyombo vya habari kama vile aliiaga dunia majuzi. Hii ilitokana na kukutwa maandishi yake yenye ombi la kutaka England ikibeba Kombe la Dunia kwa mara ya pili likawekwe kwenye kaburi lake japo kwa dakika moja. Alifariki dunia Aprili 12, 2019 akiwa na umri wa miaka 97.
Mwaka 2018 Broadis akiwa na umri wa miaka 97 alikuwa amepanga kwenda Russia kama timu ya England ingefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Dunia la 21 lililofanyika huko. Alichokuwa na hamu ya kukiona kwa mara ya pili katika uhai wake ni kuiona England ikibeba Kombe la Dunia. Wakati alipokuwa akiichezea timu hiyo hakufanikiwa.
Mzee huyo alikuwepo Uwanja wa Wembley na wachezaji wenzake wa zamani wa England pale nahodha Bobby Moore alipokabidhiwa kombe baada ya England kuifunga Ujerumani mabao 4-2 katika fainali 1966. Tangu siku ile hamu yake kubwa ilikuwa kuiona England ikilibeba tena kombe hilo la mbabe wa soka duniani. Kwa bahati mbaya ndoto yake ilizimwa kwa kipigo cha bao 1-0 ilichopata England katika nusu fainali ilipocheza na Ufaransa, ambayo hatimaye ilichukua kombe kwa ushindi wa mabao 4-2 katika mchezo dhidi ya Croatia.
Baada ya England kushindwa kuingia fainali aliamua kuvunja safari ya kwenda Russia kwa sababu alichotaka ni kuiona inabeba kombe. Mzee huyo wakati ule alikuwa mchezaji mkongwe kabisa aliyekuwa hai kuichezea England na alikuwa akionekana mara kwa mara katika vituo vya televisheni vya England.
Akiwa na kumbukumbu nzuri alikuwa mara kwa mara akizungumzia mengi juu ya kandanda ilivyokuwa zamani na habari za timu ya England wakati alipokuwa katika kikosi cha timu hiyo. Kwa masikitiko mzee huyo ambaye baadaye kwa miaka 45 alijitokeza kama mwandishi wa habari mahiri, alielezea habari za wachezaji wenzake wa zama hizo wa England na wa nchi mbalimbali ambao wote walishafariki dunia.
“Nimebaki peke yangu kuchukua kumbukumbu za kuwaeleza wenzangu waliotangulia nilichokiona baada ya wao kuaga dunia,” aliwahi kueleza.
Broadis aliyeichezea England michezo 14 ya kimataifa ambayo kwa wakati ule ilikuwa ni mingi kwa vile haikufanyika mara kwa mara kutokana na usafiri kutokuwa rahisi na wa haraka kama ilivyo sasa.
Aliifungia England mabao manane na alikuwemo katika kikosi cha England kilichocheza fainali za 1954 zilizofanyika Uswisi na kufunga mabao mawili. Mara nyingi alipokwenda katika shughuli mbalimbali alivaa koti lenye namba 3 aliyoivaa katika fainali za Kombe la Dunia 1954.
Katika zama zake alipokuwa akisakata kandanda, Broadis alishirikiana na Stanley Matthews, Tom Finney na Billy Wright. Katika fainali za 1954 England iliwafunga wenyeji Uswisi 2-0 na siku tatu baadaye ilitolewa na Uruguay katika robo fainali kwa kufungwa mabao 4-2.
Wakati ule Hungary ndiyo iliyokuwa na kikosi bora cha kandanda duniani na mara nyingi katika simulizi zake alisema alishangaa kuona haikufanikiwa kulibeba Kombe la Dunia.
Alielezea yaliyotokea Budapest, Hungary, mbele ya watazamaji 92,000 wiki tatu tu kabla ya kuanza fainali 1954, ambapo Hungary ilipoichezesha nyumbani England na yeye akiwa mmoja wa wachezaji waliotoka uwanjani baada ya kuchapwa mabao 7-1. Hicho ni kipigo kikubwa kabisa katika historia ya England.
“Hungary walikuwa wachezaji hatari. Ukikutana nao unatumia muda mwingi kujizuia usifungwe badala ya kutafuta bao,” alisema.
Aliwahi kueleza kuwa katika maisha yake alimuona Ferenc Puskas wa Hungary ndiye mchezaji bora duniani na hatari zaidi alipotumia mguu wa kushoto kupiga chenga na kufyatua mashuti. Mwaka 1967 alifurahi alipokutana na Puskas katika Uwanja wa St James’ Park wa Newcastle United kwenye mchezo maalumu ulioandaliwa.
Broadis, mbali na kupenda kuzungumzia kandanda, pia alipenda kutoa simulizi juu ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia (1939-45) ambapo aliungana na Jeshi la Uingereza akiwa mwandishi wa habari. Ivan Arthur Broadis alizaliwa Desemba 18, 1922 katika eneo la Isle of Dogs (Kisiwa cha Mbwa), London na kujiunga na Tottenham Hotspur akiwa na miaka 17 akaichezea kwa muda mrefu. Mwaka 1949 alijiunga na Sunderland akiwa mwalimu wa timu na kupata umaarufu mkubwa, na akabandikwa jina la Bank of England, yaani Benki ya England.
Miongoni mwa mambo yaliyomshitua hapo mwanzo na kumfurahisha baadaye ni pale alipofika nyumbani kwa polisi akiwa na pingu mkononi. Alishangaa na kujiuliza amefanya nini. Baadaye askari alimwambia wakati akiwa katika doria alipata ujumbe wa kumtafuta afike kumpa taarifa ya kuchaguliwa kujiunga na kikosi cha England.
Miongoni mwa michezo iliyompa faraja ni England ilipoifunga Scotland 4-2 katika Uwanja wa Hampden Park, Scotland, mbele ya watazamaji 130,000. Kabla ya kuaga dunia alitoa ombi kwa wachezaji na viongozi wa kandanda wa England kuzuru kaburi lake na kumpa taarifa itakapotokea siku imebeba Kombe la Dunia. Hivi sasa yamepatikana maandishi ya kutaka kombe liwekwe juu ya kaburi lake.
Mpaka miezi michache kabla ya kuaga dunia Broadis alifika katika viwanja kuangalia kandanda na kusema hakuwa anapenda kuangalia taarifa za habari kwa sababu kila siku alichosikia ni mauaji, ubakaji na nchi kuwa katika uhasama, mambo ambayo mwanamichezo hayapendi.
Broadis alistaafu kucheza kandanda 1960 na kuwaachia vijana akiwemo aliyekuja kuwa kocha maarufu wa Manchester United, Alex Ferguson. Hapa lipo somo kubwa kwa Watanzania. Je, tunamjua mchezaji mkongwe kuliko wote ambaye yupo hai aliyewahi kuichezea timu ya Tanganyika au Zanzibar? Tujifunze kutoka kwa wenzetu ili tuwe na historia inayoeleweka ya michezo hapa nchini.