BRAZIL 'SELECAO'; Kutoka Pele mpaka Neymar
Muktasari:
- Macho ya dunia kwa sasa yameelekezwa ndani ya kambi ya Brazil baada ya kocha Carlo Ancelotti kutangaza kikosi chake kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia 2026, huku jina la Neymar likiwa gumzo.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: KUREJEA kwa Neymar ndani ya kikosi cha Brazil kumeamsha matumaini mapya ya taifa hilo kubwa la soka huku historia yao ya Kombe la Dunia ikiendelea kuwafanya kuwa timu yenye heshima kubwa zaidi duniani
Macho ya dunia kwa sasa yameelekezwa ndani ya kambi ya Brazil baada ya kocha Carlo Ancelotti kutangaza kikosi chake kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia 2026, huku jina la Neymar likiwa gumzo.
Kurejea kwa nyota huyo ndani ya timu ya taifa kumeibua hisia kubwa kwa mashabiki wa Brazil ambao kwa muda mrefu walikuwa wameanza kupoteza matumaini ya kumuona tena akiwa sehemu ya safari ya taifa hilo kuelekea katika mashindano hayo makubwa zaidi duniani.
Kwa miezi mingi Neymar alikuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha yaliyomuweka mbali na soka kwa muda mrefu. Kulikuwa na mashaka mengi kuhusu uwezo wake wa kurejea katika kiwango cha juu huku baadhi ya wachambuzi wakiamini kuwa huenda safari yake ndani ya timu ya taifa ilikuwa imefika mwisho.
Lakini sasa kila kitu kimebadilika baada ya jina lake kurudi rasmi kwenye kikosi cha Brazil, jambo ambalo limewafanya mashabiki wengi kurejesha imani yao juu ya ndoto ya taifa hilo kutwaa Kombe la Dunia kwa mara nyingine.
Kurejea kwa Neymar ambaye kwa sasa anaichezea Santos ya nyumbani kwao Brazil si taarifa ya kawaida kwa Wabrazil. Huyu ni mchezaji ambaye kwa miaka mingi amebeba matumaini ya taifa lote.
Kuanzia akiwa kijana mdogo kwenye klabu ya Santos hadi alipohamia Ulaya ambako alitesa akiwa na Barcelona pamoja na PSG.
Uwezo wake wa kucheza soka la kuvutia, kufunga mabao na kubeba timu katika nyakati ngumu ulimfanya kuwa mchezaji ambaye mashabiki walimpa jukumu la kuendeleza historia kubwa ya Brazil kwenye Kombe la Dunia.
Lakini ili kuielewa Brazil vizuri, lazima kwanza uielewe historia yao kubwa ndani ya mchezo wa soka. Hakuna taifa lililowahi kutengeneza simulizi kubwa katika Kombe la Dunia kama Brazil.
Kwa zaidi ya miaka 90 wameendelea kuwa alama ya soka la kuvutia, ubunifu mkubwa na vipaji vilivyobadilisha mchezo huo duniani. Wakati mataifa mengi yakibadilika na kupotea kwenye ushindani wa kimataifa, Brazil wameendelea kubaki kuwa sehemu ya historia ya kila Kombe la Dunia.
Brazil ndiyo taifa pekee lililoshiriki kila michuano ya Kombe la Dunia tangu mashindano hayo yaanze rasmi mwaka 1930. Hilo pekee linaonyesha ukubwa wa taifa hilo kwenye mchezo wa soka.
Jezi yao ya njano imekuwa moja ya alama maarufu zaidi katika michezo duniani, huku mashabiki wao wakijulikana kwa mapenzi makubwa waliyonayo kwa timu yao ya taifa. Popote Kombe la Dunia linapofanyika, Brazil huwa moja ya timu zinazotazamwa zaidi kutokana na historia yao na namna wanavyocheza soka.
Kilichowafanya Brazil kuwa tofauti na mataifa mengine si mataji yao pekee, bali ni mtindo wao wa kucheza. Brazil waliubadilisha mchezo wa soka kwa kuleta aina ya soka lililojaa burudani, pasi za haraka, chenga za kuvutia na uhuru mkubwa wa kushambulia.
Dunia ilikuja kulitambua soka hilo kwa jina la “Jogo Bonito”, yaani mchezo mzuri. Kwa Brazil, soka si kazi tu wala mchezo wa kawaida. Ni sehemu ya maisha ya kila siku, utamaduni na fahari ya taifa.
Watoto wengi nchini humo hukua wakicheza mpira kwenye fukwe za Rio de Janeiro, kwenye mitaa yenye vumbi na kwenye viwanja vidogo vilivyojaa kelele za mashabiki. Kutoka mazingira hayo ndipo walipozaliwa baadhi ya wachezaji wakubwa kabisa kuwahi kutokea duniani.
Brazil imekuwa kama kiwanda cha kuzalisha vipaji vya soka kwa miongo mingi, jambo ambalo limeifanya dunia kuendelea kuwaheshimu hata katika nyakati ambazo hawashindi mataji.
Hata hivyo safari yao ya kuwa wafalme wa dunia haikuwa rahisi mwanzoni. Kabla ya kutawala soka la dunia, Brazil walipitia maumivu makubwa yaliyolibadilisha taifa hilo milele. Mwaka 1950 walipewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza huku taifa lote likiamini huo ungekuwa mwaka wao wa kwanza kutwaa ubingwa wa dunia mbele ya mashabiki wao wenyewe.
Mashabiki walifurika kwenye Uwanja wa Maracana kwa maelfu wakisubiri kuona Brazil wakitwaa kombe hilo. Walihitaji sare tu dhidi ya Uruguay ili kuwa mabingwa wa dunia. Kila kitu kilionekana kuwa upande wao. Lakini kilichotokea kilibadilisha historia ya taifa hilo milele. Uruguay waliifunga Brazil mabao 2-1 mbele ya maelfu ya mashabiki waliobaki kimya kwa maumivu makubwa.
Tukio hilo lilikuja kujulikana kwa jina la “Maracanazo” na mpaka leo linaendelea kuwa moja ya siku zenye maumivu makubwa katika historia ya soka duniani. Mashabiki walilia viwanjani, wengine walizimia huku taifa lote likiingia kwenye simanzi kubwa.
Lakini maumivu hayo ndiyo yaliyoijenga Brazil mpya yenye njaa ya mafanikio na kiu ya kuthibitisha ubora wao mbele ya dunia.
Miaka minane baadaye dunia ilianza kushuhudia kuzaliwa kwa mfalme mpya wa soka. Brazil walienda kwenye Kombe la Dunia la mwaka 1958 nchini Sweden wakiwa na kijana mdogo mwenye miaka 17 aliyeitwa Pelé.
Hakuna aliyedhani kwamba kijana huyo angekuja kubadilisha historia ya soka milele na kuwa moja ya majina makubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye mchezo huo.
Pele alikuwa na kipaji cha ajabu. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, akili ya mchezo na utulivu uliowashangaza hata wachezaji wakubwa wa kipindi hicho. Brazil walicheza soka la kuvutia sana huku Pelé akiwa gumzo kubwa duniani.
Walifika fainali na kuifunga Sweden mabao 5-2 na kutwaa Kombe lao la kwanza la Dunia. Kuanzia hapo Brazil wakaanza kutambulika rasmi kama taifa kubwa zaidi la soka duniani.
Pele hakubadilisha Brazil pekee, bali aliubadilisha mchezo wa soka wenyewe. Alikuwa sura mpya ya mchezo huo na jina lake likawa alama ya mafanikio ya Brazil duniani. Miaka minne baadaye Brazil walitetea ubingwa wao nchini Chile mwaka 1962 na kuonyesha kuwa mafanikio yao hayakuwa ya bahati mbaya.
Hata baada ya Pele kuumia, Garrincha aliibeba timu na kuiongoza Brazil kutwaa tena ubingwa wa dunia.
Lakini timu iliyokuja kuifanya dunia isimame na kutazama kwa mshangao ilikuwa Brazil ya mwaka 1970. Hiki ndicho kikosi ambacho mpaka leo wengi hukitaja kama timu bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka. Brazil walikuwa na mastaa waliocheza soka kwa uhuru mkubwa walikuwa wanafanya sanaa badala ya kucheza mpira wa miguu.
Pelé alikuwa bado ndani ya timu huku akiwa na Jairzinho, Rivelino, Tostao na Carlos Alberto. Pasi zao zilikuwa za haraka, mashambulizi yao yalikuwa ya kuvutia na kila mchezaji alionekana kuwa na uwezo wa kubadili mchezo muda wowote. Katika fainali dhidi ya Italia, Brazil waliifunga timu hiyo mabao 4-1 na kutwaa ubingwa wao wa tatu wa dunia.
Bao la Carlos Alberto katika mchezo huo linaendelea kutajwa mpaka leo kama moja ya mabao bora kabisa kuwahi kufungwa kwenye Kombe la Dunia. Timu hiyo ya Brazil ya mwaka 1970 ilibaki kuwa mfano wa soka safi la kushambulia na mpaka leo video zao zinaendelea kutazamwa duniani kote kama kumbukumbu ya ubora wa kweli wa mchezo huo.
Baada ya mafanikio hayo, Brazil walipitia kipindi kigumu cha kusubiri ubingwa mwingine wa dunia. Walikuwa na vipaji vikubwa lakini walishindwa katika nyakati muhimu za mashindano. Mashabiki waliendelea kusubiri kwa hamu kuona taifa lao likirejea tena kileleni mwa soka duniani.
Hatimaye mwaka 1994 nchini Marekani, Brazil walirejea kuwa mabingwa wa dunia kupitia kizazi kilichoongozwa na Romário na Bebeto. Walicheza kwa nidhamu kubwa zaidi huku wakionyesha uwezo mkubwa wa kushinda hata katika mechi ngumu. Walitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Italia kwa penalti 3-2 katika fainali iliyokuwa ngumu sana.
Lakini kizazi kilichokuja kuteka dunia zaidi ni kile cha Ronaldo Nazario. Ronaldo alikuwa mshambuliaji mwenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kufunga mabao. Akiwa pamoja na Ronaldinho na Rivaldo, Brazil waliunda moja ya safu kali zaidi za ushambuliaji kuwahi kuonekana duniani.
Katika Kombe la Dunia la mwaka 2002, Brazil walicheza soka la kuvutia sana na kufika fainali dhidi ya Ujerumani. Ronaldo alifunga mabao mawili katika mchezo huo na kuipa Brazil ubingwa wao wa tano wa dunia. Mpaka leo hakuna taifa lililowahi kufikia mafanikio hayo ya mataji matano ya Kombe la Dunia.
Baada ya kizazi hicho kuondoka, macho yote yalielekezwa kwa Neymar. Kutoka akiwa kijana mdogo kwenye klabu ya Santos, Neymar alionekana kuwa mrithi wa ufalme wa soka wa Brazil.
Alikuwa na chenga, kasi, mabao, ubunifu na uwezo mkubwa wa kubeba timu. Mashabiki wengi walimfananisha na Ronaldinho kutokana na uwezo wake wa kuburudisha mashabiki uwanjani.
Lakini safari yake kwenye Kombe la Dunia imekuwa na maumivu mengi. Mwaka 2014 Brazil waliandaa Kombe la Dunia nyumbani kwao huku Neymar akiwa tegemeo kubwa la taifa hilo. Katika robo fainali dhidi ya Colombia alipata jeraha baya lililomtoa kwenye mashindano.
Kutokuwepo kwake kulionekana wazi katika nusu fainali ambapo Brazil walifungwa mabao 7-1 na Ujerumani katika mchezo ulioushtua wengi.
Matokeo hayo yalikuwa moja ya maumivu makubwa zaidi katika historia ya Brazil. Mashabiki walilia viwanjani huku wengine wakionekana kushika vichwa vyao kwa maumivu makubwa. Mpaka leo mchezo huo unaendelea kuwa doa kubwa katika historia ya taifa hilo.
Sasa Brazil imeanza ukurasa mpya chini ya Carlo Ancelotti. Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa amepewa jukumu la kuirudisha Brazil kwenye siku zake za utawala. Kikosi cha sasa kina mchanganyiko wa damu changa na uzoefu mkubwa huku nyota kama Vinícius Júnior na Endrick wakionekana kuwa matumaini mapya ya taifa hilo.
Lakini bado macho yote yataendelea kuwa kwa Neymar. Wengi wanaamini hii inaweza kuwa nafasi yake ya mwisho kujaribu kuipa Brazil Kombe la Dunia. Presha ni kubwa, matarajio ni makubwa na historia ya Brazil ndiyo inayofanya kila Kombe la Dunia lionekane kama jukumu la lazima kwa taifa hilo.
Kutoka Pelé mpaka Neymar, kutoka Maracana mpaka viwanja vya kisasa vya dunia, Brazil wameendelea kubaki kuwa moyo wa soka la dunia. Na sasa dunia inasubiri kuona kama Selecao wataweza kuandika historia nyingine kwa kutwaa Kombe la Dunia la sita na kurejesha heshima yao kama wafalme wa soka duniani.