Bernardo Silva anaondoka Man City na utajiri wake
Muktasari:
- Mbali ya mataji na heshima ambayo anaondoka navyo, Silva pia anaondoka Man City akiwa na utajiri wa kutosha alioupata kutokana na mshahara na madili mengine ya nje ya uwanja. Leo katika ATM tumekusogezea utajiri wake na mali anazomiliki.
MANCHESTER, ENGLAND: BAADA ya safari ndefu, hatimaye staa wa Manchester City, Benardo Silva aliweka wazi atashuka katika treni ya klabu hiyo mwisho wa msimu huu.
Silva ambaye ameshinda mataji lukuki akiwa na Man City, inadaiwa ataachana na wababe hao ili kwenda sehemu nyingine na kupata changamoto mpya.
Mbali ya mataji na heshima ambayo anaondoka navyo, Silva pia anaondoka Man City akiwa na utajiri wa kutosha alioupata kutokana na mshahara na madili mengine ya nje ya uwanja. Leo katika ATM tumekusogezea utajiri wake na mali anazomiliki.
ANAPIGAJE PESA
Hadi kufikia sasa, Silva analipwa mshahara unaokadiriwa kufikia Pauni 300,000 kwa wiki Manchester City.
Kwa mwaka, mshahara wake pekee unakadiriwa kufikia zaidi ya Pauni 15 milioni kabla ya bonasi, lakini baada ya mjumuisho wa bonasi hupata takriban Pauni 17 milioni.
Mbali na mshahara wa kawaida, Silva hupata bonasi zinazotokana na ushindi wa mechi, ubingwa wa Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na idadi ya asisti atakazotoa.
Kawaida katika msimu mmoja ikiwa atafanya vizuri sana hupata bonasi za hadi Pauni 5 milioni kiujumla.
Mbali ya pesa anazopata kutoka Man City, Silva pia anapata pesa za kutosha kutokana na madili mengine ya nje ya Uwanja.
Kwanza ana mkataba na kampuni ya Nike inayomlipa kwa kuvaa viatu vyenye nembo yao. Inaelezwa kutokana na dili hilo Silva anapata takribni Dola 3 milioni kwa mwaka.
Staa huyu pia ni balozi wa EA Sports ambayo imekuwa ikimtumia katika kampeni mbalimbali.
Ana dili pia na kampuni ya Axi inayojihusisha na utoaji wa huduma za kifedha.
Vilevile fundi huyu amewekeza katika sekta mbalimbali, ikiwemo
maduka ya vifaa vya michezo Ureno na majengo. Kijumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 60 milioni.
MIJENGO
Bernardo Silva anaishi kwenye jumba la kifahari jijini Manchester lenye thamani ya zaidi ya Pauni 5 milioni ambalo ndani yake kuna Gym binafsi, bwawa la kuogelea, sehemu ya mapumziko na bustani ya kisasa.
Pia anamiliki nyumba nyingine kwao Ureno yenye thamani ya takribani Pauni 2 milioni.
NDINGA
Silva anapenda magari ya kisasa na yenye kasi, hivyo katika maegesho yake kuna ndinga kadhaa ikiwemo:
Audi RS7 – Pauni 100,000
Mercedes-Benz G-Class – Pauni 120,000
Porsche Panamera – Pauni 90,000
Ferrari F8 Tributo – Pauni 250,000
BMW M8 – Pauni 120,000
SAADA KWA JAMII
Kutokana na taasisi mbalimbali, Silva amekuwa akisaidia watu wasiojiweza. Kwa mwaka amekuwa akitoa takribani Pauni 200,000 kusaidia kampeni na miradi mbalimbali England na Ureno ambayo inahusisha nyanja kadhaa ikiwemo elimu na michezo.
FAMILIA, MAISHA BINAFSI
Silva yupo kwenye ndoa na mrembo Ines Degener Tomaz, ambaye ni modo maarufu Ureno.
Silva ni mtu wa maisha ya utulivu na mara nyingi hupendelea kutumia muda wake wa mapumziko kutulia na familia na marafiki wa karibu.
Kwa sasa ana mtoto mmoja wakike aliyezaa na mkewe Ines mwaka 2023.