Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AZIZ KI - Usupastaa uwanjani hadi kwa Hamisa Mobetto

Aziz KI Pict

Muktasari:

  • Sherehe ya maharusi hayo imefanyikia Super Dome, Masaki, Dar lakini ukiachana na ndoa iliyokuwa gumzo kabla ya kufungwa kwake kumezidi kumweka Aziz KI katika matawi ya juu baada ya awali kufunika uwanjani tangu ajiunge na Yanga misimu mitatu iliyopita hadi kumbeba Hamisa.

JANA usiku ilikuwa ni sherehe ya kupongezwa Hamisa Mobetto aliyefunga ndoa na Stephane Aziz KI, Jumapili iliyopita na kuwaacha midomo wazi mashabiki waliokuwa hawaamini kama wataoana.

Sherehe ya maharusi hayo imefanyikia Super Dome, Masaki, Dar lakini ukiachana na ndoa iliyokuwa gumzo kabla ya kufungwa kwake kumezidi kumweka Aziz KI katika matawi ya juu baada ya awali kufunika uwanjani tangu ajiunge na Yanga misimu mitatu iliyopita hadi kumbeba Hamisa.

Kwa namna Aziz KI alivyo, inaonyesha mwamba ameubeba usupastaa kisha akatembea na levo ya matukio ya kikubwa.

Jamaa hajashuka wala kupotea amesimamia viwango akiendelea kuonyesha matukio makubwa yalibeba hadhi yake kwa kutingisha kila alipofanya kitu tofauti tangu atue nchini.

Tangu alipotua raia huyo wa Burkina Faso amekuwa na upekee kwa wachezaji waliotajwa mara kwa mara katika orodha ya walio bora msimu kutokana na mchango wake Yanga na hata nje.

Hapa chini tuyaangalie matukio matano ambayo yamembeba Aziz KI kistaa tangu atue nchini akijiweka kwenye hadhi ya kutingisha kila anapogusa tukio.

Aziz 01

GUMZO LA USAJILI

Usajili wa Aziz Ki ndani ya Yanga uliofanyika Julai, 2022 akitokea Asec Mimosas uligeuka gumzo nchini ukiondoa klabu zingine za nje, kwani  Tanzania alikuwa akiwaniwa na Simba na Azam kila moja ikivizia saini yake kivyake.

Simba wakati huo ilimweka mbele aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez aliyekuwa akiipigania klabu yake kusaka saini Aziz wakati Azam wakiwa na Abdulkarim Amin ‘Popat’ huku Yanga ikiwa na Hersi Said kabla ya kuwa rais wa klabu hiyo. Mwishoni mwa mawindo zikabaki Simba na Yanga ndizo ziliendelea kupasuana na hatimaye Yanga kufanikiwa kumnasa.

Itakumbukwa Mwanaspoti kitambo lilishazinasa na kuandika kwamba kiungo huyo amesajiliwa na Yanga, lakini mwisho klabu hiyo ilithibitisha imefanikiwa kwa utambulisho ambao mashabiki walilazimika kusubiri hadi usiku wa manane Julai 15, 2022 ambao ulivunja rekodi ya watu waliofuatilia video yake.

Msingi wa gumzo kubwa la watu wengi kufuatilia taarifa hiyo ulitokana na ubora wake ambao aliuonyesha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na klabu nyingi kuvutiwa naye na kuanza kumfuatilia. Kuna baadhi ya wachambuzi na watangazaji wa vituo vya redio walikaririwa wakila viapo kwamba kwa kiwango na thamani aliyokuwa nayo ilikuwa ngumu kutua Yanga, lakini leo ni mali ya klabu hiyo.

Aziz 02

MABAO YA KISTAA

Akiwa na Yanga, Aziz KI alipepesuka kidogo katika msimu wa kwanza, lakini ule wa pili aliuwasha moto akiwa staa muhimu ndani ya kikosi kwa kufunga mabao muhimu. Wanasema mchezaji mkubwa anajipambanua katika mechi kubwa na Aziz KI ndani ya mechi saba alizokutana na Simba kwenye mashindano yote amefunga mabao matatu.

Ukiachana na mechi za Simba, aliibeba timu yake kwenye mechi kubwa nyingine dhidi ya Azam ambapo tangu atue nchini ameifunga mabao sita ikiwemo hat trick moja.

Sio hapo tu, Aziz KI aliifungia bao pekee muhimu ugenini Yanga ikiing’oa Club Africain ya Tunisia na kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ambao ilikwenda kucheza fainali ya mashindano.


MFUNGAJI BORA, MVP

Msimu uliopita fundi huyo wa mguu wa kushoto alijiimarisha kwenye ustaa akiibuka na tuzo mbili kubwa - kwanza akichukua  ya mfungaji bora wa ligi akimaliza msimu na mabao 21 akimuacha Feisal Salum ‘Fei toto’ nyuma akiwa na 19.

Mbali na kufunga, pia Aziz KI alishika namba mbili kwa kuasisti akiwa na nane akizidiwa moja na aliyeibuka kinara, Kipre Junior aliyekuwa na tisa kabla hajaondoka Azam kwenda MC Alger ya Algeria. Tuzo hiyo ikazaa nyingine ndani yake akiibuka Mchezaji Bora wa msimu (MVP) akiwabwaga wenzake akiwemo Fei Toto ambapo inakuwa ya pili kwake nyingine akiichukua Asec Mimosas.

Aziz 03

BAO LA MAMELODI

Unalikumbuka bao alililofunga Aziz Ki dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika pambano la marudiano la robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita? Nalo lilimfanya kuwa gumzo Afrika baada ya mwamuzi kulikataa na kuizuia Yanga isiandike rekodi ya kutobeba ubingwa wa michuano hiyo. Licha ya Yanga kubeba ndoo, lakini Aziz KI alibaki alitajwa na kujadiliwa sana katika vyombo vya habari na mitandao kwa shuti lake na utata ukaja kumalizwa na rais wa CAF, Patrice Motsepe akiwa Zanzibar wakati alipofanya ziara yake nchini, aliyedai kwamba bao la mchezaji huyo lilikuwa halali.


MKATABA WA PILI

Gumzo la Aziz KI halikuishia tu kwenye hayo maeneo, jamaa akasumbua tena kistaa kwenye kuongeza kandarasi nyingine ya kusalia ndani ya klabu hiyo.

Hapa pia hapakupoa bali kulikuwa na vita kubwa ambayo Yanga ilipigana nje ya uwanja kumbakisha mchezaji huyo ndani ya klabu.

Mwisho wa msimu uliopita kuliibuka ofa nyingi kwa kiungo huyo kutoka klabu mbalimbali za Afrika Kusini na Afrika Kaskazini kutaka huduma yake, lakini baada ya sintofahamu kubwa mchezaji huyo alifanya uamuzi mgumu wa kubaki Jangwani ikielezwa pia kwamba alivuta mkwanja mrefu ili kukubali mkataba mpya.

Aziz 04

MSIMU HUU

Mwanzoni mwa msimu huu Aziz KI alianza kwa kusuasua kiasi cha kuelezwa kwamba amekwisha, lakini hadi sasa unaposoma makala haya amefunga mabao matano katika Ligi Kuu na kuasisti saba, ikiwa na maana amehusika na mabao 12.

Asisti alizonazo zimemfanya abakishe moja tu kufikia rekodi ya msimu uliopita na lile gumzo kwamba ameisha kwa kuendekeza starehe baada ya picha yake akivuta shisha kuzua mjadala, sasa imebaki stori tu mwamba anazidi kuwaka. Aziz KI kwa sasa pia ndiye mchezaji aliyepiga penalti nyingi zaidi katika Ligi Kuu Bara msimu huu akipiga sita, japo mbili amepoteza na kufunga nne akiwa kinara sambamba na Leonel Ateba wa Simba (kabla ya mechi ya jana)

Aziz 05

NDOA YAKE SASA

Umeona kishindo cha Aziz KI katika ndoa yake na mwanamitindo na msanii Hamisa Mobeto? Jamaa kaendeleza ukubwa wa jina lake akiiteka nchi kwa tukio lililoteka hisia za watu wengi akimchukua mrembo huyo kwa mahari ya ng’ombe 30 na rasilimali nyingine nyingi.

Ilikuwa kama inaonekana jamaa wanaigiza hivi kumbe mambo yalikuwa kweli na baada ya kutoa mahari na kukubaliwa siku iliyofuata Aziz KI akachukua jiko lake kitajiri  akiwaacha watu wengi wakiwa midomo wazi waliodani awali kwamba alikuwa anatania.

Lakini kesho yake akatinga uwanjani na kwenda kuipigania timu yake. Huyo ndiye Aziz KI. Hatujui nini kitafuata baadae. Tusubiri!