Aliyefia uwanjani 1979 sio Hussein Tindwa
KWANZA sina budi kuwaomba radhi wasomaji wangu, makala haya ya Mjuaji hayakuwapo katika gazeti la Jumapili iliyopita. Ni kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu.
Turudi kwenye mada. Kifo cha mchezaji aliyetambulika kama Hussein Tindwa kilitikisa nchi Mei 12, 1979 katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam.
SIO HUSSEIN TINDWA
Lakini leo baada ya miaka 44, Mjuaji anaufahamisha ulimwengu wa michezo kwamba aliyefariki dunia uwanjani siku hiyo hakuwa Hussein Tindwa kama inavyofahamika na wengi, bali ni Hassan Tindwa.
Kila mmoja anapozungumzia kifo hicho cha mchezaji wa kwanza nchini kufariki uwanjani basi ni lazima jina linalomjia ni Hussein Tindwa.
KWANINI NI HASSAN?
Hapa kuna siri na kuwafanya baadhi ya watu kushindwa kuweka wazi pamoja na kwamba wanafahamu ukweli wa jina la Hassan Tindwa. Watu wa kwanza kabisa waliopaswa kuweka wazi ukweli wa jina la mchezaji huyo kuwa ni Hassan na si Husseini ni wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, pia viongozi wa Simba.
Lakini kitu cha ajabu taarifa hii imeachwa ipotoshwe na wengi kushindwa kuujua ukweli hadi leo hii ambapo wengi watafunguka macho na masikio na kuzua mjadala mzito.
ALICHEZA NA KAKA YANGU
Akitumia jina lake kamili la Hassan alilopewa na wazazi wake, Tindwa akiwa mkazi wa Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, aliitumikia timu ya Tambaza, akisajiliwa kwa jina la Hassan Tindwa.
Ikumbukwe Tambaza ilikuwa ikishiriki Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo Simba na Yanga nazo zilikuwa zikishiriki.
Hapo Tindwa alicheza na kaka yangu, aliyekuwa akicheza kama kiungo katika timu hiyo, Yahya Omari Mohammed Mtulya.
Nilipozungumza na kaka Mtulya alikiri wazi alimfahamu Tindwa kwa jina la Hassan wakati akicheza naye Tambaza na si Hussein.
“Nilishangaa aliporudi kutoka Majimaji alitambulishwa kwa jina hilo, lakini siku zote alifahamika kwa jina la Hassan,” alisema Mtulya.
HAKUWA NA PACHA
Pia, Mtulya alikana madai kwamba Hassan alikuwa na pacha wake aliyekuwa akitumia jina la Hussein.
“Nimeyasikia madai hayo, lakini sio ya kweli, binafsi nilimfahamu Hassan ambaye tulisajiliwa naye pale Tambaza,” alisema.
Kabla ya kwenda Majimaji, Tindwa aliitumikia timu ya Breweries ya Dar es Salaam aliendelea kulitumia jina lake la Hassan hadi aliposajiliwa na Majimaji ya Songea.
SIMBA ILIFANYA YAKE
Inafahamika mwaka 1979 Majimaji ilimsajili kwa jina la Hassan Tindwa akipelekwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’.
Kibadeni alikuwa amejiunga na Majimaji baada ya ushawishi wa kiongozi aitwaye, Lawrance Gama. Ni hapo ndipo Simba ilipomrudisha Tindwa Dar es Salaam na kumbadili jina na kumwita Hussein badala ya Hassan.
Lengo la kumwita jina hilo ilikuwa ni kumtofautisha Hassan na Hussein katika usajili ingawaje mchezaji alikuwa ni huyo huyo.
Katika usajili wa Majimaji alisomeka kama Hassan, lakini kwa usajili wa Simba uliopelekwa FAT na CAF alisomekana kama Hussein. Inadaiwa kulikuwa ni vigumu kuwatofautisha Hussein na Hassan Tindwa kwa kuwa usajili wa kipindi hicho ulikuwa bado haujaanza kutumia picha za wachezaji.
Ushawiwishi wa Tindwa kujiunga na Simba pia ulichangiwa na jirani yake wa Magomeni Mikumi ‘Snow Camp’, Habibu Segumba ‘Underline’ aliyekuwa dereva wa teksi na Mnyama kindakindaki.
LIMEFANYIKA SANA
Jambo hilo lililofanywa na Simba limefanywa sana na hata na klabu ya Yanga. Ni kama vile Charles Boniface alipoikana Simba mwaka 1982 kwa kuongeza jina la Mkwasa mbele au Yussuf Bana mwaka 1981 alipojiita Yussuf Ismail na kuikacha Simba iliyokuwa imemsajili kwa jina la awali.
Pamoja na hili la Hassan Tindwa, Simba ilifanya tena kitendo kama hicho kwa Francis Mwikalo kutoka Muheza Shooting na kumsajili kwa jina la Fura Mwikalo wakimaanisha ni wachezaji wawili tofauti, yaani kulikuwa na Francis na Fura Mwikalo.
Hata hivyo, hili liliwatokea puani viongozi wa Simba, baada ya Coastal Union ya Tanga kukata rufaa iliyofika hadi Mahakama ya Kisutu na kuigharimu kwa kukosa ubingwa baada ya kunyang’anywa pointi.
Coastal Union ikiwa chini ya katibu wake mkuu, Salim Bawaziri iliifahamisha mahakama kwamba Francis Mwikalo aliyesajiliwa na Muheza Shooting ndiye mchezaji yuleyule aliyesajiliwa na Simba kama Fura Mwikalo. Patamu hapo. Kesi ilifika mahakamani baada ya Coastal Union kukomaa na kupita hatua zote za awali za FAT, BMT na kwa waziri wa michezo. Kipindi hicho mambo ya michezo yaliruhusiwa kufika mahakamani.
Je, unajua ni nini kilimuua
Tindwa? Usikose makala haya wiki ijayo.