SIMULIZI YA HADITHI: Machozi ya mshumaa - 2

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Zawadi baada ya kunywa funda chache za maji alishusha pumzi, alitulia kwa muda kisha alianza kwa sauti ya chini.

ZAWADI alijikuta akishangaa busara za yule mwanaume aliyeonekana mwenye busara na huruma. Japo hakupenda kuyakumbuka alichofanyiwa na mpenzi wake ambayo huufanya moyo uvuje damu kwa ndani. Hakuwa na jinsi zaidi ya kumhadithia  mkasa mzima uliosababisha kuvunjika penzi lake na mchumba wake aliyebakisha siku chache afunge ndoa.

Zawadi baada ya kunywa funda chache za maji alishusha pumzi, alitulia kwa muda kisha alianza kwa sauti ya chini.

“Yaani hata sielewi una nguvu gani kuweza kuubadili moyo wangu lakini niliapa sitaongea tena na mtu zaidi ya shoga yangu kipenzi Sheila. Mwaka mmoja na nusu iliopita niliangukia kwenye penzi la kijana mmoja mashaallah ambaye alinifanya niamini kuwa pepo ya dunia ipo  hapahapa duniani.

“Nilipendwa dunia nzima ikajua napendwa nami sikuhofu kujitupa kwenye kina kirefu cha mapenzi bila hofu ya kuzama kwa vile boya langu lilikuwepo. Mmh Siamini...Siamini,” Nuru aliinama na kulia kilio cha kwikwi kutokana na kuchubua donda la moyo.

“Najua inauma jikaze kike umalize,” Abby alisema huku akimpa tishu afute machozi baada ya kufuta aliendelea.

“Bado siamini kilichotokea juzi ni kweli au nipo ndotoni, heri iwe ndoto ili nikiamka isiwe kweli. Lakini haikuwa hivyo kilichotokea ni kweli kabisa, penzi langu na Jimmy lilifutika ghafla kama vumbi lililopitiwa.”

Zawadi alijitahidi kumuadithia Abby kila kitu akiwa katika maumivu makali akiamini kabisa ameonewa.  Mpaka anamaliza kumhadithia alikuwa kwenye hali mbaya sana iliyosababisha presha kupanda. Ilibidi wamuwahi kumtundikia dripu ya kuteremsha iliyomfanya apitiwe na usingizi.

Abby alimwangalia Zawadi kwa huruma lakini alimhakikishia shoga Sheila kuwa atakuwa vizuri akiamka nawe alishinda naye pale hospitali.

                                   MIEZI MITATU ILIYOPITA

 Machozi ya msichana  Mage yalikuwa yakibubujika kama maji yanayoporomoka kutoka juu ya kilima bila kuzuizi chochote na kusababisha fulana aliyokuwa amevaa mpenzi wake Jimmy kulowa kama imechovya kwenye maji.

“Mage mpenzi wangu ni mapema sana kujikatia tamaa kwa vile hili wameamua wao na si mimi.”

“Jimmy huko ni kudanganyana hakuna kitachobadirika ikiwa wazazi wako wameishaamua.”

“Thamani yako naijua mimi.”

“Muongo mkubwa, kama ungekuwa unaijua thamani yangu usingekubali wazazi wako wamchumbie mwanamke usiyemjua?” Mage alisema kwa sauti ya kilio.

“Mage nikueleze mara ngapi hakuna mwanamke ninayempenda zaidi yako, nakuapia chini ya anga ya mwenyezi Mungu mwanamke niliyechaguliwa na wazazi wangu sitamuoa ila nitakuoa wewe,” Jimmy alizidi kujitetea mbele ya mpenzi wake.

“Muongo mkubwa kama umesema maandalizi ya harusi yameanza kadi zimeanza kusambazwa ni muujiza gani utakaozuia harusi yako?” Mage alimuuliza Jimmy huku macho yake yakiwa yamefunikwa na machozi.

“Unaniamini au uniamini?” Jimmy alimuuliza kwa sauti kavu.

“Nakuamini, ila nakuhakikishia siku ukifunga ndoa ndiyo siku ya mauti yangu.”

“Amini uhai wako upo mikononi mwangu nakuhakikishia sitautupa chini.”

“Jimmy nakuamini ila ukienda kinyume sitakwenda kunyume na niliyokueleza nitajiua.”

“Mpenzi siwezi kwenda kinyume na ahadi yangu siwezi kuyaacha machozi yako yapotee bure kama ya mshumaa.”

Kijana Jimmy alikuwa kwenye wakati mgumu baada ya kumweleza mpenzi wake uamuzi wa wazazi wake kumtafutia mchumba mwingine tofauti na kipenzi chake Mage ambaye alimuahidi angemuoa pia alikuwa akifahamika kwao.

Lakini wazazi wake Jimmy hasa mama yake hakumpenda Mage kutokana na tabia zake ya ughaibuni za kuvaa nguo zilizomuweka nusu utupu kupenda starehe kujirusha kwenye kumbi za usiku kitu kilichokwenda tofauti ya mila na desturi ya Mtanzania kuvaa nguo zenye heshima na utulivu.

Wazazi wa Jimmy walimweleza mtoto wao juu ya mavazi aliyokuwa akivaa mpenzi wake yalikuwa yakiwachukiza na kuamini hakuwa mwanamke sahihi kwa mtoto wao hasa kwa kuwa watu wacha Mungu ambao waliishi walikula na kuvaa vitu vilivyo mpendeza Mungu.

Jimmy alitumia muda mwingi kumshawishi mpenzi wake abadili mavazi, lakini ilikuwa kazi ngumu kubadilika kwa vile aliamini wazazi wa mpenzi wake walikuwa wamepitwa na wakati kwani aliamini kuvaa kwake kulikuwa kwenda na wakati, hivyo hakuwa tayari kubadili uvaaji wake.

Hali ile ilisababisha wazazi wake kumpiga marufuku mtoto wao kuwa karibu na Mage kitu kilichochochangia kuishi maisha ya kujificha Mage kuingia usiku nyumbani kwao na Jimmy na kuondoka bila wazazi kumuona. Hali ile iliweka ufa katika uhusiano wao uliopelekea Jimmy kumtaadhalisha mpenzi wake.

Taarifa za Jimmy kutafutiwa mchumba na wazazi wake zilimshtua sana, aliamini Mage akibadilika basi angekuwa na nafasi kubwa ya kuwa mkewe. Kabla ya kumweleza uamuzi wa wazazi wake juu ya kumtafutia mchumba alikwenda dukani na kununua nguo za heshima zaidi ya pea kumi na kumpelekea mpenzi wake ili abadli mavazi kabla ya kumtetea kwa wazazi wake.

“Mpenzi nguo hizi za nini?” Mage alimuliza Jimmy huku akizitoa kwenye mifuko.

“Unatakiwa kuanza kuvaa kuanzia leo hii.”

“Mpenzi haya siyo mapigo yangu.”

“Zivae ili wazazi wangu waone umebadilika nimewaahidi umebadilika.”

“Jimmy mpenzi siwezi kuvaa nguo hizi sijui magauni marefu kama mtawa au mwanamke mjane,” Mage alisema huku akibinua midomo.

   “Mage kiburi chako ipo siku kitalipoteza penzi letu,” Jimmy alimtahadharisha mpenzi wake.

“Lakini Jimmy mpenzi hivi mavazi yangu mbona ya kawaida sijawahi kusikia wazazi wangu wakishtuka. Siwezi kuvaa mavazi ya kizee  hivi umbile hili ungeliona kama nigevaa mavazi kama mtawa?” Mage aliuliza huku akijigeuza katika vazi la gauni fupi lililoishia chini ya makao.

“Ni kweli mpenzi wangu, lakini utamaduni wa kitanzania una mavazi yake usipo badilika kimavazi utanipoteza.”

“Jimmy utakuwa ameamua, kumbuka wewe ndiye aliyeniambia mavazi ninayovaa ndiyo unayapenda.”

“Ni kweli nayapenda kwa sasa itafute ndoa kisha tukiwa kwetu vaa utakavu hata ukitembea na nguo ya ndani tutakuwa kwetu hakuna wa kutuingilia.”

“Ukisikia nidhamu ya uoga ndiyo hiyo lazima wazazi wako waende na wakati.”

“Mage unajua kwa nini nimekuletea nguo hizi uvae?”

“Ili kuwafurahisha wazazi wako.”

“Si kweli.”

“Haya, kwa nini umeniletea nguo za kizee?”

Alimweleza mpenzi wake alichokikuta nyumbani kwao jana yake usiku baada ya kurudi nyumbani.


JANA YAKE USIKU

Jimmy baada ya kutoka kula raha na mpenzi wake  Mage akiwa ametoka kuoga akijifuta maji kwa taulo mlango wa chumbani kwake uligongwa.

“Nani?” aliuliza bila kugeuka akiwa bado ameupa mgongo mlango.

“Ni mimi  kaka,” ilikuwa sauti ya dada wa kazi.

“Ooh! Suzy leo siri nimeshiba huko nilipokuwa.”

“Hapana kaka unaitwa na mama.”

“He! Kuna nini tena kuitwa usiku huu?”

“Mi kaka nitajuaje.”

“Sawa nakuja.”

Jimmy baada ya kuvaa singland na bukta alikwenda hadi sebuleni walipokuwa amekaa wazazi wake kwenye kochi moja. Alikwenda kukaa kwenye kochi la mtu mmoja lililokuwa karibu na wazazi wake. “Naam wazazi wangu.”

“Leo lini?” baba yake aliuliza.

Jimmy kwa vile aliulizwa swali na kushtusha lilimfanya asahau siku ile kupelekea kuangalia juu na kuitafuta siku ile na kugundua ni jumapili.

“Jumapili.”

“Sawa, jumamosi ijayo  tutakuwa na safari ya pamoja.”

“Ya kwenda wapi tena wazazi wangu?”

“Tunakwenda Kilimahewa .”

“Kuna nini?”

“Kuna binti mmoja tumemuona kwa kweli ni mwanamke nzuri anajiheshimu pia mcha Mungu, kwa vile wazazi wako tumemuona na kumfuatilia kwa muda tumevutia nae pia familia yake wacha Mungu nina imani Mungu kasikia maombi yetu katupa tulichokiomba.”

“Ha!  wazazi wangu lakini mbona mi nina mchumba tayari,”  Jimmy alishtushwa na kauli ya wazazi wake ya kumtafutia mchumba wakati wakijua ana mpenzi wake Mage.

“Mchumba wako nani? Mbona sisi wazazi wako hatumjui.”

“Mchumba wangu si ni Mage wote mnamjua.”

“Yule mwanamke kahaba mtembea uchi?” alidakia mama yake.