Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 6

Muktasari:

  • Mishi, binti mrembo wa Kitanga, anakolea kwa kijana dereva wa malori, Musa, ambaye amefika bei anataka kumuoa mwanadada  huyo. Musa anaenda kumfanyia 'shopping' ya begi la harusi Kariakoo...

“Twenzetu,” nikamwambia.

“Huyo shemeji yuko wapi?”

“Ameniambia tukutane naye kwenye kituo cha daladala, atakuja kwa teksi.”

Tuksanza mwendo wa miguu hadi kwenye kituo cha daladala. Vile tunafika tu tuliona teksi ikisimama kando yetu. Musa akatoa kichwa kwenye dirisha na kutuita.

“Musa yule, twende,” nikamwambia Amina.

Tukaenda kujipakia kwenye ile teksi iliyotupeleka Kariakoo. Tuliposhuka kwenye teksi tukaanza kuzunguka kwenye maduka. Tulipoteza karibu saa mbili tukiwa tunazunguka kwenye maduka mbalimbali kuulizia hiki na kile.

Tulianza kununua begi kubwa ambalo tulilijaza nguo na vitu vingine vilivyohitajika. Kila kitu nilichonunua nilikuwa nikijadiliana na Amina. Musa alikuwa kimya akitutazama tu.

Baada ya kukamilisha vitu tulivyokuwa tunahitaji, Musa alikodi tena teksi iliyotupeleka hadi nyumbani kwetu Ilala. Lakini Musa hakushuka. Nilishuka mimi na Amina tukaingia ndani na begi letu. Musa aliondoka na teksi.

Tukiwa chumbani mimi na Amina nikawa na kazi ya kujaribu nguo nilizonunua.

Kila nguo niliyovaa, Amina alikuwa akiitilia tiki.

Nguo moja nikampa yeye.

Hebu ijaribu kwanza,” nikamwambia.

Amina akaijaribu ile nguo.

“Unaionaje?” Akaniuliza huku akijitazama tazama.

“Imekutoa,” nikamwambia.

“Nitaichukua na ndiyo nitakayovaa siku ya harusi yako.”

Tukacheka kisha nikamuita shangazi na kumuonyesha lile begi.

“Litakaa kwangu hadi hiyo siku litakapohitajika.” Shangazi akaniambia.

“Ngoja niliingize chumbani mwako.”

Nikalibeba lile begi na kuliingiza chumbani kwa shangazi.

“Unajua kwamba keshokutwa asubuhi ndio unapelekwa kwa kungwi?” Shangazi akaniambia tulipokuwa chumbani kwake.

“Kumbe ni keshokutwa?”

“Ndiyo keshokutwa asubuhi.”

“Kwani vile vifaa vinavyotakiwa vimepatikana?”

“Vimeletwa vyote, si vitu vingi. Ni mswala, mto, vyombo vya kulia chakula na doti tatu za khanga pamoja na mitalawanda.”

“Si nimeambiwa kuwa nitasingwa huko huko?”

“Msio pia umeshapatikana. Tulikuwa tunatafuta siku tu ya kukupeleka na tumeona siku muafaka ni keshokutwa.”

“Sawa shangazi.”

Niliporudi chumbani kwangu sikumueleza Amina yale niliyozungumza na shangazi. Nilijiambia nitamjulisha nikiwa tayari nimeshapelekwa kwa kungwi.

Usiku wa siku ile nikiwa chumbani kwangu Musa akanipigia simu. Tukazungumza sana. Nilimjulisha kwamba ningepelekwa kwa kungwi keshokutwa yake.

“Utakuwa huko kwa siku ngapi?” Akaniuliza.

“Sijajua bado lakini mara nyingi inakuwa ni siku ile ile ambayo sherehe za harusi zinaanza.”

“Mimi nimepanga tuoane juma lijalo.”

“Una maana kwamba mipango yako iko vizuri?”

“Mimi nimeshajiandaa.”

“Sawa. Sasa nitamuuliza shangazi ili nijue nitakaa huko kwa siku ngapi.”

Muulize halafu uniambie ili mipango yetu iende sawa.”

“Basi nitakupigia kesho nikujulishe.”

Baada ya kumaliza kuzungumza na Musa nikatoka chumbani na kwenda chumbani kwa shangazi.

“Shangazi nimekuja kukuuliza?”

“Wewe huishi kuuliza, unataka uulize nini?”

“Nataka nijue huko kwa kungwi nitakaa siku ngapi?”

“Sasa itategemea siku mliyopanga kuoana.”

“Musa hawezi kupanga siku mpaka ajue siku ambayo nitatoka kwa kungwi.”

“Kule kwa kungwi unakwenda kuandaliwa kwa ajili ya harusi, hakuna muda maalum. Kama ni muda tunaupanga sisi, si kungwi.”

“Sasa mimi nataka nikakae kwa wiki moja tu. Baada ya hiyo wiki ndio harusi ifanyike.’

“Ndio mwambie huyo mchumba wako atuletee hiyo siku ambayo atakuja kuoa.”

“Basi nitampigia simu nimwambie.”

Baada ya kuzungumza hivyo na shangazi nikabaki kimya.

“Una jingine?”  Shangazi akaniuliza.

“Nilitaka kukuuliza hilo tu, shangazi naye! Eti una jingine?”

Nikatoka mle chumbani na kurudi chumbani kwangu. Nilifikia kushika simu na kumpigia Musa.

“Nimeshazungumza na shangazi,” nikamwambia.

“Amesemaje?’

“Amesema wewe ndio utoe siku ya kuja kuoa.”

“Hilo si suala tulilozungumza. Tulizungumza kuhusu muda ambao wewe utakuwa kwa huyo kungwi. Siwezi kutaja siku kabla sijajua huko kwa kungwi utarudi lini!”

“Shangazi amesema kwa kungwi hakuna muda maalum. Muda nitakaokaa huko utategemea siku ya harusi yetu, inaweza ikawa wiki moja, wiki mbili au zaidi.”

“Sasa mimi nakusikiliza wewe, ungependa tuoane siku gani mchumba wangu?”

“Baada ya wiki moja kutoka leo, yaani tusiweke muda mrefu.”

“Sawa. Basi nitakupa siku kesho.”

“Sio unipe mimi, uje mwenyewe uzungumze na shangazi au utume mtu.”

“Nitakuja mwenyewe kuzungumza naye lakini nitakupigia simu asubuhi kukujulisha muda ambao nitakuja.”

“Poa.”

“Unajua mimi sina watu wengi hapa Dar, mambo yangu ninayapanga mwenyewe.”

“Hata mimi pia sina watu wengi. Wazazi wangu wenyewe wameshakufa. Nimezaliwa peke yangu. Walioko ni ndugu na jamaa tu wa pembeni. Kwa hiyo mambo yangu mengi anayasimamia shangazi.”

“Sawa. Basi ni hapo kesho.”

Asubuhi kulipokucha shangazi akanifuata akiwa na ratiba mpya. Akaniambia.

“Nimezungumza na huyo kungwi wako amesema upelekwe leo usiku. Kwa hiyo kwa siku ya leo huruhusiwi kutoka, umeshakuwa mwari.”

“Loh, sasa itakuwaje?

“Hivyo hivyo itakavyokuwa, kwani wewe wataka iweje?”

Shangazi aliponiuliza hivyo sikuwa na jibu nikabaki kucheka. Hapo hapo Musa akanipigia simu. Shangazi alipoona napokea simu akaondoka.

“Habari ya subuhi?” Musa akaniuliza.

“Nzuri. Niambie…’

“Nimepanga hiyo shughuli iwe Jumapili ijayo.”

“Saa ngapi?”

“Usiku. Kwenye saa mbili hivi.”

“Tutafunga ndoa msikitini au nyumbani?”

“Unajua hata sheikh wa kutufungisha hiyo ndoa namtegemea kutoka kwenu. Kwa hiyo ninyi ndio mtapanga iwe msikitini au nyumbani.”

“Sawa, nitamwambia shangazi iwe msikitini na sheikh atapatikana. Kuna misikiti mingi huku.”

“Mimi nitafika muda ule ule wa kuoa. Baada ya kufunga ndoa tunaondoka.”

“Utakuja na watu wangapi?”

“Si watu wengi sana.”

“Sasa wewe utakuja saa ngapi kuzungumza na shangazi?”

“Kwenye saa tano nitakuwa nimeshafika hapo.”

“Sawa. Nitamjulisha. Halafu ile ratiba ya kwenda kwa kungwi imebadilika.”

“Imekuwaje?”

“Badala ya kwenda kesho, nitakwenda leo usiku.”

“Mnataka kuharakisha.”

“Sijui, shangazi mwenyewe ndio anajua.”

“Sawa.”

“Na nimeambiwa nisitoke leo, nimeshakuwa mwari.”

Musa akacheka kwenye simu.

“Mbona unacheka?” Nikamuuliza.

“Nimefurahi ulivyoniambia kuwa umekuwa mwari.”

“Unazijua mila za pwani?”

“Ninazijua.”

“Basi ndio hivyo.”

Ilipofika saa tano Musa akaja nyumbani. Nilipomuona nikaingia chumbani. Kwa mujibu wa mila zetu, mimi sikutakiwa kuingilia mazungumzo yake na shangazi na pia hakutakiwa anione.

Walizungumza na shangazi kwa karibu saa nzima. Nilisubiri mpaka usingizi ukanipitia. Shangazi akaja kuniamsha. Akaniambia Musa ameshakwenda zake.

“Naona mmezungumza sana,” nikamwambia.

“Tumezungumza na tumekubaliana, ameniambia atakuja kuoa siku ya Jumapili saa mbili usiku.”

“Kwa hiyo tuna wiki moja ya maandalizi, si inatutosha shangazi?” Nikamuuliza shangazi.

“Inatosha. Na wewe itabidi ukae kwa kungwi kwa wiki moja.”

“Sawa.”

“Tatizo ni kuwa niko peke yangu na mambo ni mengi.”

“Jitahidi shangazi, utafanyaje sasa?”

“Ninajitahidi lakini ndio hivyo mnanichokesha haraka.”

Nikatoa kicheko hafifu cha kumfariji shangazi.

“Usijali shangazi. Mungu atakulipa.”

“Namkumbuka sana marehemu kaka yangu, angekuwepo ningekuwa na mwenzangu wa kunisaidia lakini ameshatangulia mbele ya haki.”

“Ni kweli shangazi, jitahidi tu.”

Shangazi akanitazama kisha akageuka na kutoka.

Ilikuwa ni kweli tangu alipofariki marehemu baba yangu, shangazi alikuwa amechukua majukumu yote yanayonihusu mimi. Maandalizi yote ya harusi yalikuwa mikononi mwake. Pamoja na utu uzima wake hakuwa mwanamke legelege. Alikuwa amekaza kama mwanamume akiendesha biashara zake na kuhakikisha maisha pale nyumbani yanakwenda vizuri.

Ilipofika saa moja usiku wadada watatu waliokuwa wameandaliwa na shangazi kunipeleka kwa kungwi wakawasili. Walikusanya vitu vilivyokuwa vinahitajika kupelekwa kwa kungwi wakaniandaa na mimi kisha teksi ikaitwa.

Wakati natolewa chumbani kwenda kupanda teksi nilikuwa nimefunikwa ushungi kuziba uso wangu ikimaanisha tayari nilikuwa mwari nisiyetakiwa kuonekana uso wangu.

Nilipakiwa kwenye teksi tukaondoka na wale wadada. Safari ilikuwa ni ya kwenda Buguruni ilikokuwa nyumba ya huyo kungwi. Tulipofika teksi ilisimama tukashuka. Mimi bado nilikuwa nimefunikwa ushungi.

Inaendelea...