HADITHI: Bomu Mkononi - 3
Muktasari:
- MISHI Ramadhani Mzaka, Binti wa Kitanga aliyewachanganya waume watatu kwa mpigo. Walimuoa kwa ndoa halali kila mmoja kwa wakati wake. Akawa anaishi nao wote bila wenyewe kujuana. Alijiona mjanja mpaka siku bomu lilipomlipukia mikononi…Baada ya kupewa lifi na dereva wa malori aitweaye Musa, anamvutia mwanaume huyo.
ILIKUWA ni sehemu ambayo nilipenda kwenda kula chakula kila nilipokuwa na pesa. Niliwahi kufika mara kadhaa nikiwa na Amina, hivyo alikuwa akipajua vizuri.
Nilipofika hapo nilikuta watu wachache sana. Nilikuta watu wachache kwa sababu haikuwa sehemu inayojaza watu kwa vile vyakula vyake vilikuwa ghali sana. Mimi mwenyewe nilikuwa nakula hapo pale ninapopata pesa za bure kama zile elfu arobaini alizonipa Musa.
Ni kwa sababu nilikuwa napenda sana starehe na maisha ya kifahari.
Niliagiza pilau ya kuku na juisi. Nilipoletewa nilianza kula pilau ya moto na kuku wa kuvunja mifupa huku nikisukumia na juisi ya nanasi baridi.
Wakati namaliza chakula hicho shoga yangu Amina akatokea.
“Umekuja na mguu mbaya shoga, ndio kwanza namalizia pilau na kuku,” nikamwambia Amina kimzaha mzaha.
“Mimi nimeshashiba ugali, niagizie juisi tu.” Amina akaniambia.
“Juisi kunywa shoga, usijali.”
Nikaagiza juisi nyingine mbili. Zilipoletwa kila mmoja aliwekewa juisi yake. Tukaanza kunywa.
“Niambie shoga yangu,” nikamwambia Amina baada ya kufyonza funda la juisi kwenye mrija.
“Poa tu. Hivi mshikaji wako Sele hamjawasiliana hadi leo?”
“Sele nimeshamsahau mwenzangu…”
“Uchumba umeishia hewani!”
“Umeishia hewani dada kwa gundu nililonalo. Sijui nitampata mganga gani aliondoe.”
Amina akacheka kwa maneno yangu ya mzaha.
“Wasema wewe, mimi je huniulizi!” Akaniambia.
“Kwani yule Mwarabu wako vipi?”
“Tulishaachana. Mpumbavu yule, anataka kuniharibu.”
Nikaanza kucheka kabla sijajua Amina amekusudia nini.
“Kivipi?” Nikamuuliza.
“Tabia yake si nzuri.”
“Lakini si alikuwa anakupa pesa nzuri.”
“Ananipa pesa sikatai lakini anachotaka yeye, mimi sikiwezi.”
“Kipi sasa?”
Amina akakunja uso kabla ya kuniambia.
“Mambo ya kinyume cha maumbile mimi siyataki.”
“Haaa! Kumbe ndio mambo yake!”
“Hata akinipigia simu yake sipokei. Sitaki upuuzi.”
“Loh ni shida!”
“Mimi mtu akiniletea habari hiyo, hata kama nampenda kiasi gani, naachana naye.”
“Achana naye dada atakuharibia maisha yako.”
“Nimeshaachana naye mwenzangu.”
“Nasikia siku ya kujifngua inakuwa tabu kweli.”
“Sasa ya nini tabu yote.”
“Mimi mwenzako nimeamua kupumzika, sitaki mabwana wasioeleweka.”
“Wajidanganya tu. Utapumzika hadi lini?”
“Hadi hapo atakapojitokeza mwanaume atakayetaka kunioa kabisa.”
“Siku hizi kuna wanaume waoaji, wanataka wakuchezee tu halafu wakuache.”
“Ndio sitaki sasa.”
Niliendelea kuzungumza na Amina hadi juisi zetu zikaisha. Nikalipa bili niliyeletewa, tukatoka.
“Nisindikize saluni, nataka kwenda kuosha nywele na kupakwa dawa,” nikamwambia Amina.
“Twende.”
Kulikuwa na saluni moja ambayo nilizoea kwenda kutengeza nywele zangu. Tukaenda hapo.
Tulipofika hakukuwa na wateja wengi nikashughulikiwa haraka haraka. Nilioshwa nywele nikapakwa dawa. Baadaye dawa iliondolewa nikawekwa nywele zangu vizuri. Amina akaniambia.
“Umependeza shoga!”
“Asante.”
Mpaka ninaachana na Amina ilikuwa saa mbili usiku. Nikarudi nyumbani.
Siku iliyofuata niliamshwa alfajiri saa kumi na moja na nusu asubuhi. Ulioniamsha ulikuwa ni mlio wa simu yangu. Nikanyoosha mkono wangu na kuichukua. Nikaona namba ya dereva Musa.
“Vipi Musa?” Nikasema mara tu baada ya kuipokea simu yake.
“Oh Mariam bado umelala?”Sauti ya Musa ikasikika kwenye simu.
“Ni saa ngapi sasa?” Nikamuuliza.
“Kunakaribia kucha. Ni saa kumi na moja na nusu.”
“Mbona umenipigia muda huu kuna nini?’
“Ndio naondoka.”
“Ahaa ndio unakwenda Burundi?”
“Ndiyo.”
“Kumbe mnaondoka mapema sana.”
“Safari yenyewe ni ndefu inabidi kuondoka mapema.”
“Nakutakia safari njema lakini usisahau kuniletea zawadi.”
“Zawadi ni lazima. Niombee nifike salama na nirudi salama.”
“Ninakuombea. Utakwenda na utarudi salama.”
“Samahani kwa kukatisha usingizi wako, nilitaka kukuaga tu, endelea kulala.”
“Bila samahani, nashukuru kwa kuniamsha.”
“Haya kwaheri.”
“Asante kaka.”
Musa akakata simu. Baada ya hapo sikulala tena. Nikawa ninamuwaza Musa, dereva wa malori aliyenipa lifti ya gari kutoka Kigoma.
Baada ya muda kidogo simu yangu ikatoa mlio wa kupokea meseji. Nilipoitazama meseji yenyewe, nikaona Musa amenitumia shilingi elfu hamsini.
Nilipoona ile meseji ya pesa kutoka kwa Musa nilitabasamu peke yangu.
“Hakuniambia kama angenitumia pesa,” nikajisemea.
Nilirejea kwenye eneo la kutuma meseji nikaandika maneno mawili tu.
“Asante sana.”
Kisha nikamtumia Musa. Baada ya muda kidogo, meseji nyingine kutoka kwa Musa ikaingia.
Nilipoisoma ilisema. “Usijali.”
“Yule kaka ananifurahisha sana,” nikaendelea kujisemea peke yangu.
Nilishuka kitandani nikaenda uani kujisaidia kisha nikarudi chumbani na kulala tena.
Kitendo kile cha Musa cha kukumbuka kuniaga na kunitumia shilingi elfu hamsini kilinipa imani kuwa angeniletea zawadi, tena zawadi ya kuridhisha.
Sikukosea. Zilipita wiki tatu hivi. Siku hiyo nilikuwa nyumbani nimelala. Ilikuwa kama saa nane na nusu mchana, Musa akanipigia simu.
Nilipopokea simu yake akaniambia.
“Niko Mlandizi, tunarudi.”
“Poleni kwa safari,” nikamwambia.
“Tunashukuru, safari ilikuwa nzuri.”
Nikataka kumuuliza kuhusu zawadi aliyoniahidi lakini nilisita. Niliona aibu kumuuliza.
Badala yake nikamuuliza kitu kingine.
“Mtaingia saa ngapi Dar?”
“Kwenye saa kumi na moja hivi.”
“Unadhani tutaonana kwa leo?”
“Ni wewe tu. Kama utakuwa na nafasi, njoo pale tuliposimama siku ile tuonane.”
“Nije saa ngapi?”
“Njoo saa kumi na moja.”
“Sawa, nitakuja.”
Baada ya hapo sikulala tena. Nikaanza kujitayarisha. Ilipofika saa tisa na nusu nikatoka. Nilikwenda kupanda daladala hadi Kariakoo kisha nikapanda nyingine iliyonipeleka Kimara.
Wakati ninashuka kwenye daladala Musa akanipigia tena.
“Umeshafika?” Akaniuliza.
“Ndiyo nashuka kwenye daladala.”
“Harakisha uje hapa, tumeingia mapema.’
“Sawa, ninakuja.”
Niliposhuka kwenye daladala nikatembea kwa miguu kuelekea pale mahali tulipoachana na Musa siku ile. Nililiona kwa mbali lori lenye trela limeegeshwa mahali hapo. Nikahisi lilikuwa ndilo lori alilokuwa akiendesha Musa.
Nilipolifikia Musa alifungua mlango wa dereva akashuka. Nilifurahi sana kumuona. Alikuwa amependeza sana japokuwa alikuwa anatoka safari.
“Oh muadhamu hujambo?” Akaniuliza kwa kunichangamkia.
“Sijambo, za safari?”
“Nzuri. Niambie.”
“Poa tu.”
“Kuna mzigo wako ndani ya gari,” akaniambia.
“Ni mzigo mkubwa?” Nikamuuliza.
“Ni mkubwa kiasi,” akaniambia kisha akafungua mlango wa gari. Akamwambia taniboi wake.
“Hebu shusha lile boksi.”
Taniboi wake akashusha boksi kubwa lenye umbo la upapa. Akaliweka chini kando ya mlango.
“Ni nini?” Nikauliza.
“Ni sabufa kubwa.” Musa akaniambia na kuongeza.
“Nimeinunua Bujumbura.”
Kwa kweli nilifurahi sana. Nikamuuliza Musa.
“Ndiyo zawadi yangu uliyoniletea?”
“Ndiyo hiyo.”
“Asante sana kwa zawadi nzuri.”
“Itabidi ukodi bajaj. Hili boksi ni kubwa na zito.”
“Sawa. Nitakodi bajaj.”
Musa akamuagiza taniboi wake alete bajaj. Taniboi akaenda kukodi bajaj. Bajaj ilipofika Musa alimwambia alipakie lile boksi. Boksi lilipopakiwa Musa alitoa pochi yake akanipa shilingi laki moja.
Hapo ndipo nilipoanza kumpenda Musa.
“Nitakupigia,” akaniambia baada ya kunipa pesa hizo.
Alikuwa ameshanilegeza.
“Sawa. Nipigie tuzungumze.”
“Okey, basi wewe nenda. Tutazungumza zaidi kwenye simu.”
“Sawa.”
Nikajipakia kwenye bajaj na kuondoka. Ilipofika saa nne usiku nikiwa nyumbani, Musa akanipigia simu tukazungumza sana. Katika mazungumzo yake alinieleza wazi kuwa alitaka kuwa na mimi kimapenzi. Aliniambia alikuwa amenipenda tangu ile siku ya kwanza aliponipa lifti.
Lakini na mimi nilikuwa nimeshampenda. Kilichonifanya nisite kumpa jibu ni kutojua tabia zake. Nilikuwa ninahitaji kujipa muda wa kumchunguza na kujiridhisha naye kabla ya kumkubalia ombi lake.
“Usijali, ninakufikiria,” nikamwambia.
“Nitakuja kukutembelea huko Ilala kesho.”
“Karibu. Utakuja mida gani?”
“Itakuwa jioni.”
“Kama saa ngapi?”
“Nafikiri itakuwa saa kumi.”
“Sasa tutakutana wapi?” Nikamuuliza.
“Niambie wewe.”
“Nitakusubiri kwenye kituo cha daladala zinazotoka Kariakoo.”
“Sawa, basi nisubiri hapo saa kumi.”
“Usijali.”
Musa akakata simu.
Inaendelea...