Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 22

Muktasari:

  • Binti mrembo cheupe, ambaye ukimwangalia unaweza kusema ni Mwarabu, anawavuruga wanaume kwa kuolewa na mume zaidi ya mmoja. Hili ni bomu mkononi...

Sehemu ya 22

NIKWAMBIA msaidizi wa kazi: “Wewe utabaki hapa hapa, utakuwa unajipikia chakula unachotaka mwenyewe, mchele upo, unga upo, maharage yapo, dengu lipo. Ni wewe tu.”

“Sawa dada, kwa hiyo wewe utarudi baada ya wiki moja?”

“Nimepanga hivyo lakini tutakuwa tunawasiliana kwa simu. Kama kutakuwa na tatizo lolote utaniambia.”

“Sawa.”

“Nikija nikute nyumba ipo safi, yaani angalia mazingira kama vile uko kwako.”

“Sawa dada.”

Nikafungua pochi yangu na kumpa shilingi elfu thelathini.

“Hizi zitakusaidia kununua vitafunio au kitu chochote unachotaka.”

“Asante dada.”

Nikaondoka. Nilikwenda kwa shangazi. Shangazi alishangaa alipoona naingia na mtoto. Alikuwa akijua kuwa nilikuwa mjamzito lakini habari ya kujifungua hakuwa nayo.

“Ni mwanao huyo?” Akaniuliza.

“Ni mwanangu.”

“Umejifungua lini?”

“Kama wiki mbili hivi.”

Nilimdanganya. Ukweli ni kuwa tangu nilipojifungua zilikuwa zimepita karibu wiki nne.

“Mbona hamkuniambia?”

“Mume wangu alikuwa hayupo na mimi mwenyewe baada ya kujifungua nikawa na tatizo la presha ya kushuka, nikalazwa. Nimetoka hospitalini jana.”

“Sasa ni nani aliyekuwa anakusaidia.”

“Wauguzi wa hospitali walikuwa wakinisaidia na pia majirani zangu walikuwa wanakuja hospitalini.”

“Kwanini hukutuma mtu kuja kuniambia?”

“Niliona nitakutia wasiwasi shangazi, wewe mwenyewe umeshakuwa mtu mzima. Sitaki usumbuke shangazi yangu.”

“Mh! Wewe mtoto una moyo mgumu sana!”

“Yameshapita shangazi, usijali.”

Shangazi akamchukua mwanangu na kumbeba.

“Mmempa jina gani?”

“Siku ile naumwa na uchungu babake ndio anaondoka kwenda Burundi, si unajua safari zao…”

“Una maana hajarudi hadi sasa?’

“Hajarudi bado na mimi siwezi kumpa jina mtoto bila yeye.”

“Kwani alikwambia atarudi lini?’

“Huwa haniambii siku ya kurudi, anarudi siku yoyote tu. Inaweza kuchukua hata wiki sita.”

“Kumbe anachelewa sana.”

“Anachelewa.”

“Na hana taarifa kuwa umejifungua?”

“Hana.”

Baada ya kumdanganya shangazi nilikaa kwake kwa siku mbili. Siku ya tatu yake Musa akanipigia simu kunijulisha kuwa anakuja, Siku hiyo hiyo nikaondoka kurudi nyumbani kwangu Kimara.


Musa aliporudi usiku alinikuta nyumbani. Akashangaa kunikuta nimeshajifungua.

“Umejifungua lini?”

“Hii ni wiki ya tatu tangu nijifungue.”

“Hongera mke wangu, umenizalia mtoto wa kiume.”

“Wewe ulipenda mtoto wa kike?’

“Wa kwanza akiwa wa kiume ni vizuri.”

“Mpe jina basi.”

“Huyu ni baba yangu mzee Ramadhani. Kama angekuwa hai angefurahi kumpata wajina wake.”

“Mbona huniulizi matatizo yaliyonipata?’

Umepata matatizo gani?”

“Nililazwa hospitalini siku tatu, presha ilikuwa imenishuka baada ya kujifungua.”

“Eh! Pole sana. Sasa nani alikuwa anakusaidia?”

“Shangazi, nilipotoka hospitalini nikaenda kukaa kwa shangazi anisaidie.”

“Inabidi nikutafutie dada wa kazi.”

“Ndio nilikuwa nataka kukwambia.”

“Ningejua ningekuja naye, huko vijijini tunakopita kuna wasichana wengi wanaotaka kazi za ndani.”

“Sasa itabidi umtafute hapa hapa.”

“Nitajitahidi.”

Siku ile Musa alilala kwa furaha ya kupata mtoto. Asubuhi kulipokucha aliondoka mapema kuliko kawaida yake. Ilipofika saa nne akarudi akiwa na taniboi wake. Alikuwa ameshika mfuko uliokuwa na vitu vya mtoto, nguo, nepi, chandarua na kijigodoro kilichokunjwa, akaviweka juu ya kochi.

Vitu hivyo tayari nilikwishanunuliwa na Mustafa lakini Musa hakuwa na habari.

Musa akamzungumzia taniboi wake kuhusu suala la dada wa kazi. Taniboi huyo akatuambia kwamba kama tutampa nauli anaweza kumuagiza kutoka kijijini kwao Chalinze.

    “Utamuagiza lini?” Musa akamuuliza.

    “Ninyi mnamtaka kwa lini?”

    “Ikiwezekana hata kesho.”

    “Naweza kumuagiza hii leo kama mtanipatia pesa ya nauli, kesho anaweza kuja.”

    “Nauli ya nani sasa, ya wewe kumfuata huko au ya yeye kuja huku?”

    “Nauli yake yeye, mimi nitamtumia mama yake kwenye simu.”

    “Kwa hiyo atakuja yeye mwenyewe?”

    “Ndiyo, atakuja yeye mwenyewe, akifika hapa atanipigia simu nimfuate alikoshukia.”

    “Sawa. Nikupatie kiasi gani?”

    “Nipe elfu thelathini tu.”

    “Tukitoka hapa nitakupa.”

    Walipoondoka Musa alirudi tena usiku, akaniambia taniboi wake ameshamuagiza dada wa kazi ambaye atanisaidia kazi za ndani.

    Tulitarajia kuwa angekuja siku iliyofuata lakini hatukuona mtu, siku ya tatu yake ndio taniboi wa Musa alipowasili naye nyumbani.

  “Anaitwa Mage,” akaniambia, kisha akamwambia Mage: “Aliyekuagiza ndiye huyo na nyumba ambayo utafanya kazi ndio hii. Huyo ni mke wa dereva wangu. Naomba uonyeshe uaminifu, nidhamu na bidii ya kazi.”

    “Sawa. Nitakuwa mwaminifu na nitafanya kazi kwa bidii.” Mage akatuambia na siku ile ndipo alipoanza kazi.

Ikapita wiki kabla ya Musa kupata tena safari ya kwenda Burundi. Mara kwa mara nilikuwa nawasiliana na mtumishi wangu wa Mbezi. Nilikuwa nikimuuliza hali ya pale nyumbani na kama Mustafa ametokea.

    Majibu yake yalikuwa ya kuniridhisha. Alikuwa akiniambia anaendelea vizuri na hakukuwa na matatizo. Kuhusu Mustafa aliniambia bado hajatokea.

    “Utarudi lini dada?” Kila mara alikuwa akiniuliza.

    “Siku ya kurudi nitakwambia, usijali.”

    Siku ile aliyoondoka Musa kwenda Burundi ndipo nilipompigia simu dada wa kazi wa Mbezi nikamwambia kwambia nitakwenda kesho yake.

    “Angalia kama atatokea Mustafa mwambie nimempeleka mtoto hospitalini, usimwambie kuwa niko huku umesikia?”

    “Ndio dada.”

  “Anaweza kugomba kwa sababu sikumuaga.”

    “Sasa nimwambie umekwenda hospitali gani na umeondoka muda gani?”

    “Muda wowote atakaofika mwambie dada ameondoka sasa hivi kwenda hospitalini, halafu nipigie simu uniambie.”

    “Akiniuliza mtoto ana nini nimwambieje?”

    “Mwambie alikuwa analia sana, mama yake anadhani tumbo linamuuma.”

    “Sawa. Umesema utarudi kesho?”

    “Natarajia kurudi kesho.”

    Niliongea na dada wa kazi huyo asubuhi, nikashinda pale nyumbani hadi jioni. Ilipofika saa moja usiku akanipigia simu.

    “Dada kaka amekuja,” akaniambia. Moyo wangu ulishituka kidogo.

    “Una maana mume wangu?” Nikamuuliza.

    “Ndio.”

    “Umemwamabiaje?”

    “Vile ulivyoniambia.”

    “Akasemaje?”

    “Ameniuliza mtoto alikuwa analia sana, nikamwambia ndio alikuwa analia sana.”

    “Enhe…”

    “Ameniuliza mmekwenda hospitali gani nikamwambia sijui.”

    “Alikuwa anataka kutufuata?”

    “Labda.”

    Sikutarajia kuwa Mustafa angerudi siku ile ambayo nilikuwa nimepangia kulala Kimara. Ile habari ikawa imenishitua.

    “Sasa itabidi uje. Usipokuja atajua nimemdanganya.” Dada wa kazi akaniambia.

    “Nitakuja,” nikamwambia kisha nikakata simu na kuizima kabisa.

    Niliogopa kuwa Mustafa angeweza kunipigia na kuniuliza niko hospitali gani, nikakosa jibu. Nikajiandaa kuondoka.

  “Mage nimepigiwa simu, shangazi yangu anaumwa naenda huko na nitalala huko huko, ninakuachia nyumba. Mlinzi yupo nje hakuna tatizo,” nikamdanganya Mage.

    “Huyo shangazi yuko wapi?” Mage akaniuliza. Maneno yangu yalikuwa yamemuingia.

    “Yuko Ilala.”

    “Utarudi kesho?”

    “Huenda pia nisirudi kesho, lakini nitakupigia simu kukujulisha.”

    Nikampa Mage shilingi elfu hamsini.

    “Hizi ni za kununua chakula chako mpaka nitakaporudi, umenielewa?”

    “Nimekuelewa dada.”

    Nikatoka nje na mwanangu pamoja na begi langu, nikamuaga mlinzi wetu, naye nikampa shilingi elfu kumi ya sigara. Akanishukuru.

    Nilikwenda kupanda teksi. Kwanza ilinipeleka kwenye duka la dawa, nikanunua dawa za tumbo za mtoto ingawa alikuwa haumwi. Nilipotoka hapo ndipo nikaenda Mbezi.  

    Nilipofika dada wa kazi akaniambia Mustafa ameondoka na gari.

    “Amekwenda wapi?” Nikamuuliza.

    “Sijui, hakuniambia?”

    Nikawasha simu yangu ili nimpigie na kumjulisha kuwa nimeshafika nyumbani.

Wakati nawasha simu tu, simu yangu ikaita. Nikaona aliyenipigia alikuwa Mustafa. Nikaipokea.

“Nimeshafika nyumbani,” nikamwambia hata kabla ya kusalimiana naye.

“Sasa mbona ulizima simu?”

“Si unajua nilikuwa hospitalini. Kelele za milio ya simu hazitakiwi,” nikamdanganya, akajua ni kweli.

“Mimi nilikuwa nimewafuata nyinyi huku hospitalini lakini sikuwakuta.”

“Tumeshaondoka, njoo nyumbani.”