Dili iliyokufa - 21
ILIPOISHIA
Wakwetu alilipa faini ya makosa mawili. Kosa la kuendesha kwa uzembe lilitozwa shilingi laki mbili na kosa la kusababisha ajali lilitozwa shilingi laki tatu.
Upande wa mashtaka uliahidi kumfikisha mtu aliyejeruhiwa siku iliyofuata na James alitakiwa afike siku hiyo.
Baada ya shauri hilo kuishia hapo, Wakwetu alikwenda tena hospitalini kumjulia hali Masumbuko. Aliruhusiwa kusalimiana naye tu. Baada ya kusalimiana naye, Wakwetu alimpa shilingi laki moja ili zimsaidie kwa matumizi madogo madogo kisha akamuaga na kuondoka.
Alipotoka hospitalini, Wakwetu alikwenda kazini kwake. Mchana akarudi nyumbani. Mara tu alipoingia ndani, Sharifa alimpa mfuko uliokuwa na kitu ndani.
SASA ENDELEA...
“NINI?” aliuliza wakati akipokea.
“Bastola yako imeletwa na Majaliwa”
“Yuko wapi?” Wakwetu aliuliza kwa kutaharuki huku akiitoa bastola hiyo kwenye mfuko.
“Mimi pia sikumuona. Huo mfuko alimpa mlinzi kwenye geti, yeye hakuingia huku ndani. Mlinzi ndiye aliyeileta”
Wakwetu aliitazama tazama ile bastola kisha aliipindisha mtutu wake na kutazama risasi zilizokuwemo. Ilikuwa na risasi tisa. Mwenyewe alipoiweka ilikuwa na risasi kumi.
“Risasi moja imetumika, ndiyo ile aliyompiga yule kijana” Wakwetu alisema na kuongeza.
“Sasa ni kwanini hakuingia humu ndani?”
“Ameacha na hii barua kwa mlinzi, amesema upewe wewe”
Sharifa akampa Wakwetu bahasha iliyokuwa na barua. Wakwetu aliipokea na kuifungua.
Aliitoa karatasi ya barua iliyokuwemo na kuiweka mbele ya macho yake.
Alikuta mistari michache iliyoandikwa.
“Baba nisamehe sana kwa kitendo nilichofanya. Ninakuomba radhi baba na niko chini ya miguu yako”
Hakukuwa na jingine.
Wakwetu akamtazama Sharifa kwa uso wa hasira.
“Huu ni upuuzi!” alimwambia huku akimuonesha ile barua, akaongeza.
“Nimsamehe kitu gani! Mbona hakueleza hapa ni kwanini ameiba bastola yangu na kwenda kumpiga mtu risasi. Ameona lile ni kosa dogo?”
“Kwani ameandika nini?”
Wakwetu alimpa ile barua.
“Soma mwenyewe uone upuuzi wake!”
Sharifa alichukua ile barua na kuisoma.
“Si amekuomba radhi kwa kosa lake” Sharifa alimfafanulia baada ya kuisoma ile barua.
“Kwanini hakutaka kuja kuniomba msamaha mimi mwenyewe na kunieleza ni kwanini ametenda kosa kama lile?” Wakwetu akamuuliza kwa mkazo.
“Lakini si ameomba radhi?”
“Radhi gani inaombwa kwa barua namna hii! Huyu mtoto hana adabu. Mimi nataka aje hapa anieleze ni kwanini amempiga risasi mwenzake!”
“Anaogopa. Ndiyo sababu amekuandikia barua. Wajibu wako ni kukubali msamaha wake”
“Hivi wewe unakubaliana na barua hii? Hii si dharau ambayo mwanangu ananionesha!” Wakwetu alizidi kupamba moto.
“Usichukulie kuwa ni dharau, ndio uwezo wake wa akili ulivyomuelekeza akuandikie barua kukuomba radhi. Sasa wewe mkubalie tu ili arudi nyumbani”
Wakwetu akatikisa kichwa.
“Kama wewe umemkubalia, mimi siwezi kumkubalia hata kidogo. Bado namuhitaji Majaliwa aje anieleze ni kwanini ameiba bastola yangu na kwenda kumpiga mtu. Yule kijana amemkosea nini?”
“Ni makosa ya vijana, hataweza kukueleza wewe”
“Kosa lake ni kubwa sana. Kama angemuua mwenzake angekabiliwa na kesi ya mauaji ambayo ukipatikana na hatia unanyongwa. Si kosa dogo la kuomba msamaha namna hii na ninashangaa kwanini wewe unamtetea namna hii?”
“Mimi simtetei ila ninakushauri tu. Mtoto kufanya kosa ni kawaida na mzazi ni wajibu wako kumsamehe mwanao pale anapokuomba msamaha”
Wakwetu hakusema kitu tena. Akiwa amekunja uso alinyanyuka na kuelekea chumbani. Sharifa alikuwa akimtazama kwa nyuma.
“Siwezi kumfuata tena, anaweza kunipiga makofi” alijiambia kimoyomoyo.Alikuwa akifanya jitidada kubwa kumpigania mwanawe Majaliwa ili aweze kurejea pale nyumbani.
Kitendo cha Wakwetu kuendelea kuonesha hasira dhidi ya Majaliwa kilikuwa kinamkera Sharifa. Alijua ni yeye peke yake ambaye angeweza kuubadili moyo wa Wakwetu ili suluhu ipatikane kati yake na Majaliwa.
Alijiambia angekuwa tayari hata kwenda kwa mganga wa kienyeji kumroga mume wake amsamehe mwanawe.
Wazo hilo la kwenda kwa mganga, Sharifa alijiambia, litakuwa la mwisho endapo Wakwetu hatakubali kutoa msamaha.
Kitendo cha Majaliwa kuendelea kuishi nje ya nyumbani kwao kilimpa wasiwasi Sharifa juu ya usalama wa mwanawe huyo japo alikuwa akiwasiliana naye kwa siri.Lakini mawazo yake yalikuwa tofauti na ya Wakwetu ambaye aliona Majaliwa alikuwa ameshaharibika na asiyefaa kuishi naye. Alikuwa tayari kumfukuza kabisa pale nyumbani na yeye ajihesabu kuwa hana mtoto.
Alipofika chumbani alikaa kitandani. Mawazo yakamjia kwamba aende akazungumze na mlinzi ili apate ukweli wa mwanawe.
Baada ya kuwaza hivyo alitoka chumbani akaenda nje. Sharifa alikwenda kumchungulia dirishani na kumuona anazungumza na mlinzi.
“Eti huyu mtoto alikupa nini?” Wakwetu alimuuliza mlinzi.
“Alinipa mfuko na barua, nimempa mama” Mlinzi alimjibu.
“Alipokupa alikwambia nini?”
“Aliniambia nikupe wewe”
“Hakukwambia kitu kingine”
Mlinzi akatikisa kichwa.
“Kwa kweli hakuniambia kitu kingine, ningekwisha kueleza”
“Je aliingia ndani au aliishia hapa hapa?”
“Aliishia hapa hapa kwenye geti lakini aliongea na mama kwenye simu”
Wakwetu akashituka.
“Eti nini! Alimpigia simu mama yake na kuongea naye?”
“Ndiyo alimpigia akiwa hapa”
“Mbona mwenyewe hakunieleza hivyo!”
“Labda alikuwa anaongea na mtu mwingine”
“Mbona unabadilisha maneno?”
“Mimi nilidhani aliongea na mama. Sikuwa na hakika”
Wakwetu alimtazama mlinzi kisha akarudi ndani. Sharifa alikuwa ameshaondoka na kwenda jikoni. Aliondoka baada ya kumuona Majaliwa anarudi ndani akiwa ameelezwa kitu ambacho Sharifa hakutaka aelezwe.
Ilikuwa kweli aliwasiliana na Majaliwa kwa simu lakini hakutaka mume wake ajue hilo.
Wakwetu alipingia ndani alisimama sebuleni na kumuita Sharifa. Sharifa akatoka jikoni.
“Hebu nipe simu yako” Wakwetu alimwambia Sharifa.
Moyo wa Sharifa ulilipuka kisha ukaanza kupiga kwa kasi.
Alitaka amuulize “unataka simu yangu kwa ajili gani?” lakini heshima yake kama mke mbele ya mumewe ilimzuia.
Kwa bahati mbaya simu yake haikuwa mbali. Alikuwa ameiweka pale pale sebuleni juu ya kochi. Laiti kama ingekuwa chumbani angekwenda kufuta namba ambazo hakutaka Wakwetu azione kwenye simu yake.
Bila kuonesha kusita Sharifa aliichukua kwenye kochi na kumpa. Wakwetu aliikagua, akatazama namba zilizopigwa, zilizopokelewa na zilizotonywa. Akagundua namba ya Majaliwa ilikuwemo sehemu nyingi.
Kwa siku ile namba ya mwisho kupokelewa ilikuwa namba ya Majaliwa.
“Uliwasiliana na Majaliwa leo?” Wakwetu akamuuliza Sharifa kwa sauti nzito.
“Ndiyo alinipigia wakati anaacha ule mfuko kwa mlinzi”
“Alikueleza nini?”
“Aliniuliza baba yuko, nikamwambia hayuko”
“Halafu?”
“Akaniambia kuna barua na mfuko anauacha kwa mlinzi ili baba akija apewe. Baada ya hapo akakata simu”
“Mbona hukunieleza kama alikupigia simu?”
“Samahani, nilisahau kukwambia”
Wakwetu akatikisa kichwa.
“Mke wangu sikuelewi. Nimegundua kuwa mnawasiliana mara kwa mara”
“Hapana ni leo tu”
“Namba zilizizomo kwenye simu yako zinaonesha mnawasiliana mara kwa mara”
“Hizo namba ulizoona ni za mawasiliano ya siku za nyuma alipokuwa yuko hapa nyumbani”
Wakwetu aliikagua tena ile simu. Kwa bahati njema namba zilizokuwemo hazikuonesha tarehe zilipopigwa, zilipopokelewa na zilipotonywa. Wakwetu alilazimika kukubali kuwa yalikuwa mawasiliano ya siku za nyuma.
Wakwetu alimrudishia simu Sharifa bila kumuuliza chochote zaidi. Akaingia chumbani akiwa amekunja uso.
Sharifa alipobaki peke yake aliketi na kuanza kuwaza. Alijua kuwa mume wake alikuwa ameudhika na alikuwa ameanza kupata wasiwasi kati yake na Majaliwa.
Alijiambia ilikuwa ni juu yake kuhakikisha kuwa amani inarudi hapo nyumbani na mwanawe Majaliwa pia anarudi na kupokelewa na Wakwetu kwa mikono miwili.
Wakati wa kulala ulipowadia Sharifa alijichangamsha na kuanza kumpa maneno matamu Wakwetu ili kumsahaulisha maudhi na mawazo aliyokuwa nayo.
Usiku huo Wakwetu alioneshwa mapenzi ya hali ya juu ambayo hakuwahi kuyaona kwa Sharifa tangu amuoe. Mzee aliudisha moyo.