Dili iliyokufa - 15
ILIPOISHIA
“Sasa Majaliwa ungependa uendelee na masomo au ufanye kazi?” Wakwetu akamuuliza.
“Ngoja nifikirie halafu nitakwambia.”
“Kama utapenda uendelee na masomo utaniambia, vyuo viko vingi siku hizo, ni wewe tu uchague unataka usomee nini. Na kama unataka kufanya kazi au biashara utaniambia unataka kazi gani au biashara gani lakini kwa mawazo yangu ningependa upate elimu.”
SASA ENDELEA...
“Elimu ni bora zaidi,” Sharifa akamuunga mkono.
“Ndiyo, elimu ni bora zaidi, lakini nitakaa nijishauri halafu nitawaambia nimeamua nini.”
Naam, hivyo ndivyo Sharifa na mwanawe walivyomdanganya Wakwetu. Wakwetu aliamini moja kwa moja kuwa Majaliwa alikuwa mwanawe na kwamba alikuwa amefanana naye.
Alimpenda sana, alimdekeza sana mpaka Majaliwa akawa na kiburi. Alikuwa akipewa pesa anazotaka na mama yake au baba yake. Alitaka pia anunuliwe pikipiki, Wakwetu akampa shilingi milioni tatu akaenda kununua pikipiki.
Haukupita muda mrefu Wakwetu aligundua kuwa Majaliwa hakupenda kusoma wala kufanya kazi. Alikuwa hashikiki. Muda mwingi alikuwa akiupoteza akiwa na marafiki. Mara nyingine akiondoka nyumbani kwao asubuhi hurudi usiku.
Wakwetu alimuonya mara kadhaa lakini Majaliwa hakumsikiliza. Kwa vile Wakwetu aliamini kuwa Majaliwa alikuwa mwanawe na alikuwa akimpenda, alimuacha.
Kutokana na shughuli zake kuwa nyingi, Wakwetu alitafuta dereva wa gari lake. Alitoa tangazo la kutafuta dereva kwenye gazeti. Siku ile tangazo lilipotoka alianza kupokea barua za maombi ya kazi.
Siku ya pili yake kijana mmoja alifika ofisini kwake asubuhi na kuwasilisha barua yake mkononi.
Wakwetu baada ya kuifungua na kuisoma alimuuliza alikuwa na leseni ya daraja gani.
“Nina leseni ya daraja C.”
“Ulianza kuendesha mwaka gani?”
“Miaka sita iliyopita.”
“Uliwahi kufanya kazi ya udereva wapi na wapi?”
“Niliwahi kufanya sehemu mbalimbali lakini ni kwa Wahindi.”
“Hujawahi kuajiriwa katika makampuni au serikalini?”
Kijana akatikisa kichwa.
“Bado sijawahi.”
“Hujawahi kupata ajali?”
“Sijawahi, nina uangalifu sana.”
“Sawa. Nitakuajiri kazi kama ulivyoomba.”
Baada ya kukubaliana mshahara na muda wa kazi, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la James akaanza kazi ya udereva kwa Wakwetu.
Baada ya kufanya kazi kwa mwezi mmoja tu, Wakwetu aligundua kuwa kijana huyo alikuwa hodari wa kazi na mtiifu. Wakwetu akaanza kumchukulia kama mwanawe.
Alikuwa akimleta kazini asubuhi na jioni akimrudisha nyumbani. Pia alikuwa akimtuma sehemu mbalimbali. Bado alikuwa akimuendesha mke wake na kumpeleka sehemu mbalimbali alizohitaji kwenda.
Kwa sababu tabia yake iliwafurahisha Wakwetu na mke wake, wakati mwingine aliruhusiwa kula nyumbani kwa Wakwetu na alikuwa akipewa pesa za ziada kwa ajili ya matumizi yake binafsi mbali na mshahara wake.
Kutokana na Majaliwa kuanza ukorofi pale nyumbani, mara nyingi alikuwa akimkorofisha kijana huyo.
Kuna siku Majaliwa alimkuta James anakula chakula akamuondoa kwenye meza.
“Nani amekupa mamlaka ya kula hapa?” akamuuliza kwa jeuri.
“Mama ndiye aliyenikaribisha chakula,” James akamjibu akiwa pembeni mwa meza.
“Yule ni mama yangu, mimi si mama yako. Wewe ni mfanyakazi tu hapa. Usijitie wadhifa wa kula chakula chetu. Ondoka!”
Sharifa alikuwa jikoni akatoka haraka.
“Wewe Majaliwa unafanya nini?”
“Huyu James anakula hapa kama nani?”
“Wewe Majaliwa, vibaya hivyo! Kwa nini unapenda kumuonea huyu kijana wa watu? Kwani anakula mwenyewe au amekaribishwa?”
“Nimesema hakuna kula chakula hapa!” Majaliwa akasema kwa nguvu.
“Shika adabu yako, unamjibu nani hivyo?” mama yake alimwambia huku akimfokea kwa hasira.
Majaliwa aliondoka kando ya meza na kuelekea chumbani kwake.
“Unajua Majaliwa, siku hizi umekuwa huna adabu. Ngoja nitakuja kumwambia baba yako.”
Majaliwa akaingia chumbani.
“James, nenda ukale, achana na yule...”
“Basi mama, nimetosheka,” James alisema huku akiosha mikono.
“Umeshiba kweli?”
“Nimeshiba mama.”
“Yule mtoto ndivyo alivyo. Kama hujashiba, kula chakula. Usikiache.”
“Hapana mama, nimeshiba.”
Siku nyingine Majaliwa alitaka gari, James akakataa kumpa funguo. Akapigwa kibao.
“Lile ni gari lako au la baba yangu?”
Mama yake aliwahi kutoka akamkuta James amekunja uso.
“Wewe Majaliwa, wewe...!”
“Huyu nitamkomesha, anajifanya yeye ndiye mtoto wa Mzee Wakwetu,” Majaliwa alimwambia mama yake.
“Mtoto wa Mzee Wakwetu ni wewe, haya mwachie kijana wa watu.”
Majaliwa akamuachia.
“Nitakuumiza,” akamwambia kwa kutamba.
“Utamuumiza kwa kisa gani?”
“Kwa nini ananinyima funguo za gari? Kwani hili gari ni lake?”
“Wewe si una pikipiki yako baba yako alikununulia?”
“Pikipiki imepata pancha.”
“Kama imepata pancha, mwambie baba yako akupe pesa uipeleke kwa fundi.”
“Sasa mimi nataka gari, kwa nini ananinyima?”
“Gari hawezi kukupa, anatakiwa arudi tena akamchukue baba yako.”
“Yaani mimi sina haki ya kuendesha gari?”
“Wewe mtoto una matatizo sana!”
Kuna siku nyingine Sharifa alikuwa akifua nguo za mwanawe, akakuta kwenye mfuko wa suruali yake moja kuna kete ya dawa za kulevya. Ilikuwa imesokotwa kama pipi. Sharifa baada ya kuiona na kuinusa aliigundua, akashangaa.
Katika mfuko mwingine alikuta kibiriti. Ndani ya kibiriti hicho kulikuwa na kipisi cha bangi.
“Kumbe huyu mtoto ameanza kutumia unga na kuvuta bangi, ndiyo maana akili zake zimekuwa mbaya!” Sharifa akajisemea kwa mshangao.
Aliacha kufua akaanza kuwaza kuwa mwanawe sasa alikuwa ameanza kuharibika. Akagundua kwamba yalikuwa matokeo ya kumdekeza, kuwa na marafiki wabaya na kuchezea pesa.
“Siku nyingine anaondoka asubuhi anarudi usiku, kumbe kazi ni hii?” Sharifa aliendelea kujisemea kimoyomoyo.
Sharifa alinyanyuka akaenda kuchukua simu yake na kumpigia Majaliwa. Simu haikupokelewa. Alijaribu kupiga tena lakini simu iliita hadi ikakata yenyewe.
“Pengine ameshatumia unga hajielewi, hawezi kupokea simu. Hata sijui nitakuja kumwambia nini baba yake...” Sharifa alijiwazia moyoni mwake.
Wakwetu aliporudi nyumbani Sharifa alishindwa kumweleza kwamba alikuta kete ya unga na kipisi cha bangi mfukoni mwa Majaliwa. Aliona kama angemwambia hivyo Wakwetu angeweza kughadhibika na kumfukuza Majaliwa pale nyumbani, jambo ambalo lingetibua mpango wao.
Akaamua kunyamaza na kumsubiri Majaliwa mwenyewe. Siku ile Majaliwa alirudi nyumbani saa nane usiku. Alimpigia simu mama yake. Mwanamke huyo aliposhituka usingizini na kuona simu inaita huku akiliona jina la mwanawe kwenye skrini ya simu yake, alishuka kitandani kwa tahadhari ili asimwamishe mume wake aliyekuwa amelala.
Alikwenda kuipokea ile simu sebuleni.
“Wewe Majaliwa uko wapi?”
“Mama nifungulie mlango.”
“Uko wapi?”
“Niko nje.”
“Wewe mtoto saa hizi unatoka wapi?”
“Nilikuwa maskani tu na wenzangu.”
“Hujui kama huu ni usiku mwingi?”
“Nifungulie basi.”
“Mtoto ataniponza huyu!” Sharifa alijisemea peke yake na kwenda kufungua mlango na kisha akafungua geti.
Alimkuta Majaliwa akisinzia huku amesimama. Hakuwa na habari kuwa geti lilikuwa limeshafunguliwa.
Sharifa aligundua kuwa mwanawe alikuwa ameshatumia unga na ulikuwa unampelekesha.
“Wewe Majaliwa!” akamwita.
Majaliwa alipozinduka akamtazama mama yake.
“Hebu pita ndani haraka,” alimuhimiza ili Wakwetu asije akaamka na kumuona.
Mara tu Majaliwa alipoingia chumbani mwake Sharifa alimfuata na kumuuliza.
“Majaliwa umeanza kutumia unga?”
Majaliwa akashtuka.
“Unga gani mama, mbona unataka kuanza maneno!”
“Wewe hujioni kuwa unasinzia ovyo ovyo?”
“Sasa huu si usingizi tu mama?”
“Wewe mtoto usinibabaishe, umeanza kutumia unga hata macho yako na sura yako vimeanza kubadilika. Leo nimekuta kete ya unga na kipisi cha bangi kwenye suruali yako. Yaani unachanganya vitu vyote!”
Majaliwa alipoambiwa hivyo akanyamaza kimya.
“Sasa nakwambia kama umeshaanza kuharibika kiasi hicho, ujue nyumba hii itakushinda.”
“Sasa iko wapi hiyo kete yangu?”
“Unaona jinsi ambavyo umerukwa na akili! Unauliza kete yako, unataka kuendelea kuvuta? Wewe mtoto unaelekea pabaya sasa...”