Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa - 14

HADITHI Pict

ILIPOISHIA

“Aliwalea mpaka mlifikia umri gani?”

“Tulishamaliza kidato cha tatu alipotuacha na kurudi Oman”

“Aliwaacha kwa sababu gani?”

“Mume wake alifariki, akaona asingeweza kuishi peke yake akarudi kwao”

“Sasa ilikuwaje mkaenda Zambia?” Sharifa aliendelea kumuuliza maswali rahisi ili asibanwe na Wakwetu kwa maswali.

SASA ENDELEA...


“Ni hekaheka za kimaisha tu zilizotupeleka huko. Tulikutana na wenzetu tukashawishiana kuwa tuende Zambia tukatafute kazi,” Majaliwa alisema.

“Kwa hiyo mliacha masomo?”

“Tuliacha masomo. Hatukuweza kuendelea na masomo kwani yule mtu aliyekuwa akituhudumia hakuwepo tena.”

“Sasa huko Zambia mlikuwa mkifanya kazi gani?” Aliyeuliza sasa alikuwa Wakwetu.

Sharifa alifurahishwa na swali hilo kwa sababu lilikuwa rahisi na alijua kuwa Majaliwa angeweza kulijibu.

“Tulikuwa tukifanya vibarua tu. Kwa mfano, mimi nilikuwa nikiosha magari.”

Wakwetu akatikisa kichwa kusikitika.

“Naamini kuwa mlipata shida. Sasa ndugu yako alipofariki, mlimzika wapi?”

“Tulimzika huko huko. Tulipata msaada kutoka kwa jamaa wa kule kule tukamzika.”

“Ni nani alikuwa mkubwa, wewe au yeye?”

Majaliwa hakutegemea kuulizwa swali kama hilo, akasita kidogo kabla ya kujibu.

“Yeye ndiye alikuwa mkubwa.”

“Unaitwa nani?” Wakwetu akamuuliza swali jingine.

Majaliwa alisita tena. Hakukumbuka kama mama yake alimfundisha ataje jina gani pindi akiulizwa jina lake.

Akajikuta akitaja jina lake halisi.

“Naitwa Majaliwa.”

“Majaliwa nani?” Wakwetu akamuuliza tena huku akitabasamu. Majaliwa aliona atumie ubini wa Wakwetu ili kuonesha kuwa alikuwa akilitambua jina la baba yake.

“Naitwa Majaliwa Wakwetu. Hilo ndilo jina langu nililoandikishwa shuleni.”

Alipojibu hivyo, alimtupia jicho mama yake akamwona akitingisha kichwa kuunda ishara ya kumkubalia. Majaliwa akatambua kuwa hakukosea kutaja jina lake halisi.

“Huyo mama aliyewalea alilijuaje jina la Wakwetu?”

“Aliambiwa na bibi?” Majaliwa alijibu haraka. Wakwetu akamtazama mke wake.

“Unasemaje mke wangu kuhusu maelezo ya huyu kijana?”

Sharifa akajifanya anatabasamu.

“Mimi sina usemi. Nikipima maelezo yake naona ni mwanao tu, tena hata kwa sura mmefanana.”

Kitendo cha Wakwetu kufananishwa na kijana huyo kilimfurahisha, akacheka.

“Eti ni kweli umefanana na mimi?” akamuuliza Majaliwa.

Majaliwa naye akatabasamu.

“Mimi naona nimefanana na wewe, lakini marehemu kaka yangu ndiye umefanana naye zaidi,” Majaliwa akazidi kuongopa.

Wakwetu akazidi kucheka.

“Mmefanana naye kweli,” Sharifa akasisitiza baada ya kugundua kuwa kauli ile ya kufananishwa na Majaliwa ilikuwa ikimfurahisha Wakwetu.

“Sasa Majaliwa, tumesikiliza maelezo yako mimi na mama yako na tumekubali kwamba wewe ni mtoto wetu, ila tumesikitika sana kwamba mwenzako alifariki mlipokuwa Zambia.”

Sharifa aliposikia hivyo naye akaongeza:

“Tunakupokea kwa mikono miwili, karibu nyumbani kwenu, ndio hapa. Waswahili husema, ‘Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani.’ Sasa wewe umerudi ngamani.”

“Ni kweli mama. Mimi nashukuru sana kumpata baba yangu ambaye mimi na marehemu kaka yangu hatukutegemea tena kama tungekutana naye tena. Lile tangazo ndilo lililonifanya nimjue.”

“Na wazo la kutoa lile tangazo nilimpa mimi baada ya kuona amewatafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.”

“Sasa Majaliwa, nataka uhamie hapa nyumbani hii leo. Kumbe ulisema unafanya biashara gani?” Wakwetu akamuuliza.

“Nina mradi wa kukaanga chipsi.”

“Wapi?”

“Huko huko Kwaminchi.”

“Kuanzia leo unaachana na huo mradi na unakuja kuishi hapa nyumbani.”

“Asante baba.”

“Kwenye hicho chumba unachokaa hudaiwi kodi?” Sharifa akamuuliza.

“Nadaiwa kodi ya miezi miwili.”

“Basi baba yako atakupa ili uweze kutoa vitu vyako.”

“Unadaiwa kiasi gani?”

“Hicho chumba nalipia shilingi elfu arobaini kwa mwezi. Ni nyumba nzuri kidogo.”

“Kwa hiyo kwa miezi miwili itakuwa elfu themanini?” Sharifa akamuuliza.

“Ndiyo, itakuwa elfu themanini.”

“Na gari ya kuchukulia vitu vyako kutoka Kwaminchi hadi hapa itakuwa shilingi ngapi?” Sharifa aliendelea kumuuliza.

“Sijajua.”

“Sasa mimi nitakupa shilingi laki mbili. Utalipia chumba na kulipia usafiri,” Wakwetu akamwambia.

“Sawa.”

Wakwetu aliinuka akaingia chumbani kwake. Alipotoka alikuwa ameshika kitita cha shilingi laki mbili mkononi.

“Chukua hizi hapa. Nenda ukahame sasa hivi, ulete vitu vyako hapa nyumbani. Sawa?” Wakwetu alimwambia Majaliwa na kumpa pesa hizo.

“Kwa hiyo niende sasa hivi?”

“Si lazima uende sasa hivi. Unaweza kuendelea kuwepo hapa nyumbani mpaka muda ambao utapenda kuondoka, ila mimi nitawaacha. Nakwenda ofisini kwangu. Nitarudi hapa nyumbani mchana.”

“Sawa. Basi hapo utakaporudi utakuta na mimi nimesharudi.”

“Sawa.”

Wakwetu akaagana na mke wake na kuondoka.

Mara tu Wakwetu alipoondoka, Sharifa na mwanawe waliangua vicheko wakapeana mikono kutokana na kile walichokiona ni ushindi.

“Umejieleza vizuri, mzee ameshakukubali kuwa ni mwanawe,” Sharifa akamwambia Majaliwa.

“Yale maneno uliyonifundisha niliyazingatia, isipokuwa jina tu ndiyo hukuniambia nijiite nani.”

“Jina halina neno sana kwa sababu yeye mwenyewe pia alikuwa hajui watoto wake wanaitwaje. Tumia jina lako hilo hilo tu.”

“Kwa hiyo leo nitahamia hapa?”

“Ndiyo, leo uhamie hapa. Umesema unadaiwa kodi?”

“Nilimwambia tu ili anipe pesa.”

“Sasa hiyo laki moja utaiweka, hiyo laki nyingine utafanyia mipango ya kusafirisha vitu vyako kuvileta hapa. Akirudi mchana au jioni akukute hapa.”

“Na ule mradi wangu wa chipsi utakuwaje?”

“Si amekwambia huo mradi uachane nao?”

“Basi nitauacha.”

“Uache. Utakuwa unaishi hapa, tutamsikiliza baba yako atakutafutia kazi gani.”

“Sawa mama.”

“Si unaona maisha ya hapa ni mazuri tu. Nataka urithi mali za baba yako. Huyu mzee hana mtoto tena. Mtoto wake utakuwa wewe na mama yako ni mimi. Kuna tatizo gani tena?”

“Hakuna tatizo.”

Majaliwa alipoondoka nyumbani kwa Wakwetu, alirudi Kwaminchi akamfahamisha mwenye nyumba wake kuwa anahama. Mama yake alikuwa ameshamlipia kodi ya miezi sita na alikuwa amebakisha miezi miwili.

Baada ya kumfahamisha mwenye nyumba, Majaliwa alitafuta usafiri. Alipoupata alisomba vitu vyake na kuvipakia kwenye lori na kuhamia kwa Wakwetu.

Vitu alivyokwenda navyo viliwekwa stoo. Havikuwa na kazi. Mama yake alimchagulia chumba kimoja miongoni mwa vyumba sita vilivyokuwa katika nyumba hiyo.

“Utakuwa unakaa kwenye chumba hiki,” alimwambia baada ya kumwingiza kwenye chumba hicho. Chumba hicho kilikuwa na kila kitu ambacho Majaliwa angehitaji isipokuwa televisheni tu ndiyo haikuwemo.

“Ile televisheni uliyotoka nayo Mwananyamala utaiweka humu,” Sharifa akamwambia mwanawe.

Alimtandikia kitanda vizuri na kumpa shuka za ziada.

Wakati wa mchana Wakwetu akarudi nyumbani na kumkuta Majaliwa amekaa sebuleni akizungumza na mama yake.

“Umeshahamisha vitu vyako?” akamuuliza.

“Tayari nimehamisha.”

“Umeviweka wapi?”

“Mama ameviweka stoo.”

Wakwetu akamtazama mke wake.

“Umeshamuonesha chumba chake?” akamuuliza.

“Nimemuonesha na nimemtandikia kitanda chake.”

“Sawa. Mmeshakula?”

“Kwa vile ulisema utarudi mchana, tulikuwa tunakusubiri wewe.”

“Mngekula tu. Mnakaa na njaa kunisubiri mimi!”

“Ngoja basi nitayarishe.”

Dakika chache baadaye Sharifa aliwaita mezani Wakwetu na Majaliwa. Baada ya kula chakula, Wakwetu alimwambia Majaliwa mambo muhimu.

“Sijui huko alikotoka ulikuwa unaishije, lakini kwa vile umerudi hapa nataka uzingatie sana nidhamu na utii mbele ya baba yako na mbele ya mama yako.”

“Ndiyo baba.”

“Mtoto mzuri ni yule anayewasikiliza wazazi wake na kuwaheshimu,” Sharifa akadakia.

“Ni kweli mama, nawaahidi kuwa nitawaheshimu kama wazazi wangu.”

“Sasa Majaliwa, ungependa uendelee na masomo au ufanye kazi?” Wakwetu akamuuliza.

“Ngoja nifikirie halafu nitakwambia.”

“Kama utapenda uendelee na masomo utaniambia. Vyuo viko vingi siku hizi, ni wewe tu uchague unataka usomee nini. Na kama unataka kufanya kazi au biashara, utaniambia unataka kazi gani au biashara gani, lakini kwa mawazo yangu ningependa upate elimu.”