Bado Watatu - 54
Muktasari:
- Kama tunakubaliana kwamba wale watu walionyongwa walikuwa wameshahukumiwa kunyongwa, mshitakiwa alipaswa kushitakiwa kwa kujitwalia mamlaka yasiyo yake kwa kuwanyonga watu hao ambao walitakiwa kunyongwa na mkuu wa gereza.
AKANIULIZA: “Lakini bado umesema wazi kwamba katika uchunguzi wako wa alama za vidole hukugundua kwamba mshitakiwa aliwaua hao watu?”
“Uchunguzi mwingine ndio ulionyesha hivyo.”
“Mimi nimekuuliza kuhusu uchunguzi wako wewe.”
“Mimi sikugundua kama mshitakiwa aliua.”
“Asante sana.”
Wakili akakaa na kusema kuwa amemaliza maswali yake.
Nikiwa nimekaa katika safu ya mbele karibu na meza za mawakili, nilijiambia kwamba wakati mwingine maswali ya mawakili ni ya kupoteza muda bure; yalikuwa hayana maana yoyote.
Tena kama ni mtu mwenye hasira, unaweza kutoa majibu yasiyostahili kwa sababu ya hasira.
Baada ya Sajini Meja Ibrahim kutoa ushahidi wake, aliitwa shahidi mwingine ambaye alikuwa afisa upelelezi.
Ushahidi wake ulifanana na ushahidi wangu. Alieleza jinsi alivyoniongoza katika uchunguzi wa mauaji ya watu hao.
Akaeleza jinsi tulivyohangaika kumtafuta muuaji na jinsi tulivyokuja kugundua kuwa watu waliouawa walitoroshwa gerezani. Akaeleza ujanja alioutumia mkuu wa gereza kunyonga na kuzika wafungwa wengine kwa kutumia majina ya kina Unyeke ili kuonyesha kwamba kina Unyeke walikuwa wameshanyongwa.
Akaeleza tulivyokwenda kufukua makaburi yao na kukuta kumezikwa wafungwa wengine ambao pia walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.
Huku akiongozwa na wakili wa serikali, afisa upelelezi alieleza kuwa mkuu wa gereza huyo alitoa majina ya wafungwa aliowanyonga na kueleza kuwa wametoroka jela, jambo ambalo halikuwa la kweli.
Baada ya maelezo yake marefu, naye alihojiwa na wakili wa utetezi.
“Naona mlihangaika sana katika upelelezi wenu. Huyu mshitakiwa mlimpataje?”
“Niliarifiwa kwamba alijitokeza mwenyewe.”
“Katika upelelezi wenu mlikuwa mmeshindwa kumpata mpaka alipojitokeza mwenyewe?”
“Hata kama asingejitokeza tungemkamata tu. Pengine alijitokeza baada ya kugundua kuwa anaelekea kukamatwa.”
“Kitu gani kilichowafanya muamini kuwa mlikuwa mnaelekea kumkamata?”
“Hizi ni siri zetu za kipolisi, hatuwezi kuziweka hadharani.”
“Unakubaliana na mimi kwamba kitendo alichofanya mshitakiwa ndicho kile ambacho mkuu wa gereza alitakiwa kufanya lakini hakukifanya?” Wakili wa utetezi alimuuliza afisa upelelezi.
“Kitendo gani?”
“Kitendo cha kuwanyonga wale watu wanne.”
“Ndio, kitendo kile alitakiwa kufanya mkuu wa gereza.”
“Lakini hakukifanya?”
“Ndio, hakukifanya.”
“Sasa kuna kosa gani endapo alikifanya mtu mwingine?”
“Kosa lipo.”
“Kosa gani?”
“Kosa ni la kisheria.”
“Kila kosa ni la kisheria. Jibu, ni kosa gani?”
“Mshitakiwa hakuwa na mamlaka ya kuwanyonga wale watu.”
“Kwa hiyo alikuwa na kosa gani?”
Hapo afisa upelelezi alinyamaza kimya. Bila shaka alikuwa akifikiria kosa la mshitakiwa.
Kosa aliloshitakiwa nalo mshitakiwa ni la kuua kwa kukusudia. Lakini mara nyingi mawakili huwachanganya mashahidi mpaka wanajibu vinginevyo.
Kutokana na maswali ya wakili wa utetezi na majibu ya afisa upelelezi, inaonyesha kuwa mshitakiwa hakuwa na kosa la kuua kwa kukusudia, bali alikuwa na kosa la kujitwalia mamlaka asiyokuwa nayo ya kuwanyonga watu ambao walihukumiwa kunyongwa.
Kila unapojaribu kuyajibu maswali ya wakili huyo kwa umakini, unajikuta ameshakutia katika mtego wa kujibu vile anavyotaka yeye, kwamba mshitakiwa hakuwa na kosa la kuua kwa sababu watu aliowanyonga walishahukumiwa kunyongwa.
Kama ni hivyo, je, mshitakiwa alipaswa kushitakiwa kwa kosa gani? Hapo ndipo unapojikuta unashindwa kutoa jibu kwa sababu ukisema mshitakiwa alistahili kushitakiwa kwa kosa la kujitwalia mamlaka yasiyo yake, utakuwa umeshamtoa katika kosa la kuua kwa kukusudia. Niliamini kwamba hapo ndipo afisa upelelezi alipopakwepa.
“Afisa upelelezi, huna jibu?” Wakili akamuuliza.
“Kama huna jibu, sema sina jibu,” wakili aliendelea kumwambia afisa huyo.
“Jibu ninalo, isipokuwa maswali yako hayaeleweki.”
“Kipi kisichoeleweka?”
“Unauliza mshitakiwa alikuwa na kosa gani wakati unaona kuwa anakabiliwa na kosa la mauaji.”
“Kama wale watu wangenyongwa, angemuua nani?”
“Sijui.”
Sasa nilijua kuwa afisa upelelezi alikuwa amekasirika kwa maswali ya kipuuzi.
“Lakini unakubali kwamba watu aliowanyonga uhai wao ulikuwa haramu kwa sababu walishaukumiwa wafe. Unalijua hilo?”
“Mahakama ndio itajua.”
“Na kwamba kumshitaki Faustin kwa kosa la kuwaua kwa kukusudia watu ambao walikuwa wanaishi kwa uhai haramu haikuwa sahihi?”
“Mahakama itaamua.”
“Na kwamba kama ni kosa mlipaswa kumshitaki Faustin kwa kosa la kujitwalia mamlaka ya kunyonga watu waliohukumiwa kunyongwa na sio vinginevyo?”
“Mimi jibu langu ninaiachia mahakama iamue.”
“Sasa ninakwambia, uamuzi wa mahakama pia unategemea ushahidi unaotolewa hapa mahakamani.”
Afisa upelelezi akaamua kubaki kimya.
Wakili alimtazama kwa sekunde kadhaa kabla ya kuamua kukaa kwenye kiti.
“Mheshimiwa, nimemaliza maswali yangu,” akasema.
Jaji aliandika, kisha akaahirisha kesi kwa wiki mbili.
Wiki mbili zikaisha, tukakutana tena mahakamani. Upande wa serikali uliendelea kupeleka mashahidi wake ambapo shahidi aliyeitwa siku ile alikuwa daktari aliyezipima maiti za kina Unyeke na kuthibitisha kwamba walikuwa wamenyongwa.
Huku akihojiwa na wakili wa serikali, daktari huyo alieleza alivyoifanyia uchunguzi miili ya marehemu na kugundua kuwa vifo vyao vilitokana na kunyongwa.
Baada ya kutoa ushahidi huo, wakili wa utetezi alisimama na kusema:
“Sote tunakubaliana kwamba hao watu walikufa baada ya kunyongwa. Hatuna utata katika hilo.”
Aliposema hivyo, alimalizia kwa kusema:
“Sina swali.”
Wakili wa utetezi alipokaa kwenye kiti, aliitwa shahidi mwingine ambaye alikuwa ni polisi mwenzetu. Alitoa ushahidi wake lakini wakili wa utetezi hakumuuliza swali lolote. Baada ya shahidi huyo, wakili wa upande wa serikali akaeleza kwamba alikuwa amemaliza mashahidi wake.
Jaji alimuuliza wakili wa serikali endapo alikuwa tayari kutoa mchanganuo wake wa mwisho kuhusu mwendo mzima wa kesi hiyo pamoja na ushahidi uliotolewa.
Wakili wa serikali akasema yuko tayari na akaeleza kwamba upande wake umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba mshitakiwa ametenda kosa aliloshitakiwa.
Akasema hoja ya kwamba mshitakiwa aliwanyonga watu ambao walishahukumiwa kunyongwa haiwi utetezi kwa sababu haina msingi wa kisheria.
Akaendelea kueleza kwamba kama ni suala la hasira, hasira inayokubalika kisheria ni ile ya pale kwa pale.
Akatolea mfano wa mtu anayemfumania mke wake na mwanaume mwingine akifanya tendo la ndoa na kuamua kumchoma mkuki mgongoni hapo hapo kwa sababu ya hasira.
“Hasira kama hii inaweza kukubalika na kuligeuza shitaka la kuua kwa kukusudia na kuwa la kuua bila kukusudia,” akasema na kuongeza,
“Lakini kwa kosa la mshitakiwa la kuwasaka watu waliomuua ndugu yake na kuwanyonga mmoja mmoja, ni kosa jingine kabisa. Huyu alipanga mauaji na hakuua kwa hasira.”
“Kwa sababu hiyo,” wakili wa serikali aliendelea kuieleza mahakama, “Ninaiomba mahakama yako imuone mshitakiwa ana hatia ya kuua kwa kukusudia na impe adhabu inayostahiki ya kunyongwa kwa kitanzi mpaka afe.”
Baada ya kutoa maelezo hayo, wakili wa serikali akakaa kwenye kiti.
Jaji akamtazama wakili wa utetezi.
“Ninakuja upande wako, wakili wa utetezi.”
Wakili wa utetezi akasimama.
“Mheshimiwa jaji, nilichokiona mimi katika ushahidi wote uliotolewa hapa ni kwamba mshitakiwa ameshitakiwa kwa kosa lisilostahili,” wakili alisema kisha akauliza,
“Ni kwa nini nasema hivyo?” Akaendelea kueleza, “Ninasema hivyo kwa sababu kama tunakubaliana kwamba wale watu walionyongwa walikuwa wameshahukumiwa kunyongwa, mshitakiwa alipaswa kushitakiwa kwa kujitwalia mamlaka yasiyo yake kwa kuwanyonga watu hao ambao walitakiwa kunyongwa na mkuu wa gereza.”
Akaendelea kueleza kwamba kosa la kuua bila kukusudia lingethibiti endapo isingethibitika kwamba watu walionyongwa hawakuwa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa.
“Hapo ingekuwa mshitakiwa amedhulumu roho zao, lakini kumbe roho hizo zilishaamriwa na mahakama zitolewe, na mkuu wa gereza akaenda kinyume,” akasema.
“Sasa angalia,” wakili wa utetezi akaendelea, “Ukweli ni kwamba baada ya hukumu yao kutolewa, hawa watu hawakustahili kuishi. Kuishi kwao kulikuwa ni haramu. Kama asingewanyonga mshitakiwa, wangenyongwa na mkuu wa gereza. Ilimradi watu hao hawakustahili kuwepo. Sasa kumshitaki mtu eti amewaua watu hao, kosa kama hili ni lazima mahakama ifikirie mara mbili kabla ya kukubaliana na shitaka hili.”
Wakili aliendelea kuieleza mahakama kwamba hata kama mshitakiwa angetoa ripoti polisi badala ya kuwanyonga yeye, bado watu hao wangekabiliwa na adhabu waliyohukumiwa ambayo ni kunyongwa.
“Kwa hiyo bado mambo yangekuwa yale yale. Mimi nilidhani upande wa jamhuri, kama ambavyo ulimlaani mkuu wa gereza kwa kosa lake, ungempongeza mshitakiwa badala ya kumshitaki.”
Wakili akaendelea, “Kwa maana kama mshitakiwa asingewanyonga, watu hao wangebaki wakiwa hai hadi leo wakati walishahukumiwa kunyongwa na rais tayari alishasaini kunyongwa kwao.”
Inaendelea...