Zuchu asimulia alivyochanganywa na Euro 4,000

Dar es Salaam. Msanii Zuchu amesema katika moja ya mafanikio ambayo hakuwahi kuyadhania awali ni kutengeneza fedha katika mitandao ya kijamii kupitia sanaa yake ya muziki.

Zungu ameyasema hayo leo Jumatatu, Julai 26, 2021 visiwani Unguja wakati wa mafunzo maalum kwa wasanii yaliyolenga kukuza vipaji vyao, pamoja na kutumia sanaa zao kujinufaisha kibiashara.

Akitolea mfano amesema kwa mara ya kwanza anapigiwa simu kwamba amewekewa kiasi cha fedha ‘Euro 4,000’ hakudhani kama ipo siku angetengeneza fedha mitandaoni.

“Kipindi natoa Zuchu Ep nikapigiwa simu hela yangu ya youtube imeingia, kipindi hicho nilikuwa sijui sana mambo ya Euro inachenjiwa vipi, niliambiwa nimewekewa euro 4,000 kwenye akaunti yangu kupitia akaunti ya youtube nikasema aaah hizo zitakuwa ni hela ndogo tu…

“Hapo nimetoka kupewa hela ya nauli Sh20,000 na bosi sijaanza kukamata hela, siku moja nikasema ngoja nipite benki, nikauliza euro 4,000 ni shilingi ngapi nikaambiwa ni kama Sh10 milioni nilishangaa sana. Nikaanza kupiga simu mara mbili mbili hiyo ni pesa yangu ya mwezi mmoja siamini, hivyo msishangae ukiona mtu anashangilia kupata watazamaji milioni moja YouTube ujue anashangilia pesa,” amesema Zuchu.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Waziri wa Sanaa visiwani humo na kuendeshwa na jopo la wataalamu mbalimbali wa sanaa ya muziki kupitia tamasha la ‘Zuchu Home Coming’ linalotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu.

Akizungumza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amewataka wasanii hao kudumisha upendo na ushirikiano pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kuzishughulikia changamoto zinazowakabili.

“Hakuna kitu kizuri kama kuwa na taaluma katika kitu kile unachokifanya, ninawapongeza Zuchu na uongozi wa WCB kwa kuona wasanii wa Zanzibar na wao wanafaidika na sanaa ambayo wao wanaifanya,” amesema.

Amesema ni shauku yake kuona anatoa mchango mkubwa katika sanaa, “Tulianza mbali, nataka mtambue kwamba haki na shauku niliyonayo siku nikiondoka wasanii mnikumbuke japo dakika mbili nilizitumia kuwalinda, kuwaheshimisha na kuhakikisha mnapata neema juu ya kazi ambayo mnaifanya.”

Baadhi ya wataalamu wa muziki waliwaasa wasanii kuhakikisha kuhakikisha wanawekeza kwenye kazi zao.

Meneja wa WCB, Salam Sharafu amesema wasanii wanatakiwa kujituma na kutokukata tamaa, kujiamini mwenyewe ndiyo chapa ‘brand’ anayotakiwa kuitengeneza msanii.

“Kuna msanii hapa Zanzibar ananitumia kila siku kazi zake naziangalia sana na siku zote ninapoziangalia nasema nikija nitamwambia mkubwa Fela, usisubiri mtu akujibu we tuma tu kama mtu anaona kero atakublock lakini ukiona hajakublock endelea kujituma,” amesema Salam.

Naye Mkubwa Fella amesema wasanii wanapaswa kujitambua na kujiheshimu huku wakiwa wakweli na kutofake maisha.

“Heshima siyo shkamoo, kama wewe unahitaji kuingia  katika muziki basi fahamu kwamba kuna watu nimewakuta wanahitaji kufahamu mimi ni nani lakini nisipitilize. Lakini kuna muda sanaa itakulazimisha wewe uwapite, jambo la pili itakubidi uwe mkweli wa maisha yako, wengi wanafeki na wengine kufake mpaka kupitiliza lazima uanguke tu.”