Zuchu abeba tuzo ya Afrimma

STAA wa kike wa muziki wa kizazi kipya kutoka lebo ya WCB, Zuhura Kopa 'Zuchu' ameshinda tuzo ya Afrimma usiku wa kumkia leo Jumatatu Novemba 16 ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki.
Zuchu ameshinda katika kipengele cha Msanii anayechipukia ambapo alikuwa akichuana na wasanii wengine kama Kofi Mole (Ghana), Ami Faku (Afrika Kusini) na Oxlade (Nigeria).
Mbali na Zuchu, wengine walioshinda tuzo hizo kutoka Tanzania mwaka huu ni Diamond Platnuzm ambaye amebeba tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki na mwanamuziki Faustina Mfinanga maarufu Nandy ambaye ameibuka kidedea kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.
Mwaka huu, jumla ya wasanii 10 kutoka Bongo walichaguliwa kushiriki tuzo hizo, akiwemo Alikiba na kundi la dansi la Rabitt Crew. Pia wasanii kama vile rapa wa kike Rosaree, Prodyuza S2keezy na  Kimambo walichaguliwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika tuzo hizo.
Tuzo za Afrimma zilianzishwa mwaka 2014 zikiwa na asili ya Afrika Magharibi huku lengo lake likiwa ni kuunganisha mataifa ya Afrika kupitia sanaa na utamaduni.