Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zay B afariki dunia, kuzikwa leo

ZAY B Pict

Muktasari:

  • Katika safari yake ya muziki, Zay B alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kurap na ushindani wake wa kisanaa na rapa mwenzake Sister P, jambo lililokuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini na kuchochea maendeleo ya Hip Hop ya Tanzania.

TASNIA ya muziki nchini imepata pigo kufuatia kifo cha msanii mkongwe wa Hip Hop na Bongo Flava, Zay B aliyefariki dunia alfajiri ya leo Mei 31, 2026, na anataraji kuzikwa  saa 10 jioni hii nyumbani kwao Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za familia, kabla ya mauti kumkuta, Zay B ambaye jina lake halisi ni Zaynab Lipangile alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo kwa muda, hali ambayo imeelezwa kuwa ndiyo iliyochangia kifo chake.

Akizungumza na Mwanaspoti, msanii mkongwe wa Hip Hop, Juma Nature, alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kueleza kushtushwa na habari hizo kutokana na historia ndefu aliyokuwa nayo na marehemu kwenye muziki.

“Ni kweli nimezipata taarifa za kifo cha Zay B. Ni habari ya kusikitisha kwa sababu alikuwa mmoja wa wasanii waliopambana kuujenga muziki wetu katika kipindi ambacho kila kitu kilikuwa kigumu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” alisema Juma Nature.

Zay B anakumbukwa zaidi kwa nyimbo zake zilizobamba mwanzoni mwa miaka ya 2000 ikiwamo ‘Nipo Gado’ aliyomshirikisha Inspector Haroun, wimbo ambao baadaye ulipata umaarufu zaidi kupitia remix iliyomhusisha Juma Nature. Pia aliwahi kufanya vizuri kupitia nyimbo kama ‘Monica’, ‘Ananitesa’ aliyowashirikisha Unique Dadaz na Odinali pamoja na Banana Zoro.

Mbali na nyimbo hizo, Zay B aliwahi kuachia albamu ya ‘Mama Africa’ iliyofanya vizuri katika soko la muziki wakati huo na kumfanya kuwa miongoni mwa wasanii wa kike waliokuwa wakitikisa katika kizazi cha kwanza cha Bongo Fleva.

Katika safari yake ya muziki, Zay B alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kurap na ushindani wake wa kisanaa na rapa mwenzake Sister P, jambo lililokuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini na kuchochea maendeleo ya Hip Hop ya Tanzania.

Ingawa katika miaka ya baadaye alipunguza muziki na kuonekana mara chache hadharani, Zay B ataendelea kukumbukwa kama mmoja wa wanawake walioweka msingi imara wa muziki wa Bongo Fleva na Hip Hop nchini, huku mchango wake ukiendelea kuishi kupitia kazi alizoziacha.