Wosia wa Tesa wasomwa kwa video

Muktasari:
- Mwili wa Tesa uliagwa jana, kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam na kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni.
WAKATI mmoja wa watoto wawili wa Grace Mapunda (Tesa) aitwaye Rita akipewa nafasi ya kuigiza kwenye tamthilia ya Huba aliyokuwa akiigiza mama yake, wosia wa muigizaji huyo umesomwa kwa njia ya video.
Mwili wa Tesa uliagwa jana, kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam na kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni.
Tofauti na ilivyozoeleka, wosia wake ulisomwa huku zikionyeshwa video za matukio mbalimbali aliyoyafanya enzi za uhai wake, wosia huo ulisomwa na mdogo wa marehemu, Moses Mapunda
Katika video hiyo, miongoni mwa picha zilizooonekana ni ya hayati Steven Kanumba ambaye katika wosia huo naye alitajwa kama mmoja wa maproduzya wakubwa waliofanya kazi na Tesa
“Baada ya kipaji chake kuwa kikubwa alifanya kazi na maproduzya wakubwa akiwamo JB, Kanumba na Lamata Village,” alisema.
Wakati wa kusoma wosia huo, baadhi ya waombolezaji waliangua vilio huku wote wakisimama kwa dakika moja kumuombea baada ya Moses kuhitimisha kuusoma.
Akielezea historia ya Tesa, Moses alisema dada yake aliyeacha watoto wawili na wajukuu wawili ameaga dunia baada ya kusumbuliwa na mchafuko wa damu, mapafu na kisukari.
“Alipelekwa Hospitali ya Palestina kisha Mwananyamala hadi mauti ilipomkuta Novemba Mosi,” alisema Moses.
Mdogo huyo wa marehemu amesema baada ya dada yake kufikwa na mauti, uongozi wa Huba umempendekeza mmoja wa binti zake, Rita, kuingia mkataba wa kuwa sehemu ya ‘series’ za Huba.
Taarifa hiyo ilipigiwa makofi na waombolezaji huku wengine wakieleza namna ambavyo binti huyo anapaswa kufuata nyayo za mama yake kwenye tasnia ya filamu.
Muigizaji huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi katika Hospitali ya Mwananyamala alipokuwa akipatiwa matibabu.
Tesa alijizolea umaarufu kupitia michezo tamthilia na filamu mbalimbali, na hivi karibuni alikuwa akiigiza tamthilia ya Huba.