Waziri Mkuu aagiza Niffer akamatwe na Polisi
Muktasari:
- Hayo yamethibitishwa leo Novemba 18, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa katazo kwa watu mitandaoni kuchangisha fedha kwa ajili ya janga hilo huku akitaka Niffa akamatwe, ndipo Waziri alijibiwa kuwa tayari kakamatwa.
Mwanamitandao na mfanyabiashara Jenifer Jovin 'Niffer' amekamatwa na jeshi la polisi kwa kukusanya pesa za michango kwa ajili ya waathirika wa Kariakoo waliopata majanga baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka katika makutano ya Mtaa wa Congo na Mchikichi.
Hayo yamethibitishwa leo Novemba 18, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa katazo kwa watu mitandaoni kuchangisha fedha kwa ajili ya janga hilo huku akitaka Niffa akamatwe, ndipo Waziri alijibiwa kuwa tayari kakamatwa.
"Tumeona kuna watu wameanza kuchangisha huko pembeni wanasema michango kwa ajili ya waathirika wa Kariakoo hapana, serikali imeendelea kupokea kutoka kwa watu wema wakileta misaada yao hapa na walichokuwa wakileta ni maji. Sijaruhusu mtu yeyote huko nje aanze kuchangisha kwa ajili ya tatizo hili na hatukufanya hivyo kwa sababu kamati ya maafa ipo.
"Huyo binti anaitwa Niffer nimeona anachangisha na anasema mpaka jana amechangisha zaidi ya 37 milioni, atafutwe kwanza atuambie nani alimpa kibali cha kuchangisha umma utaratibu huo anaotumia wa kuingiza pesa kwenye simu yake amepata kibali wapi na amekusanya shilingi ngapi. Anasema amenunua maziwa amepeleka wapi kwa kuwa jeshi la polisi mmeshampata mumhoji mfunge hiyo akaunti na kupitia tangazo hili haturuhusu mtu mwingine yeyote kusimamia michango ya watu," amesema Majaliwa.