Wasanii waondolewa tozo kwenye YouTube

Dar es Salaam. Kuanzia sasa wasanii ruksa kurusha kazi zao kwenye akaunti zao binafsi za YouTube bila kufanya usajili na malipo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Sambamba na hilo pia wametakiwa  ‘kuacha kiki’ na kutumia taaluma zao vizuri katika kutangaza kazi zao badala ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii.


Hayo yamesemwa jana Jumanne Aprili 19, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Hassan Abbasi katika mkutano wake na Viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na vyama vinavyounda shirikisho hilo.

Dk Abbasi amewaeleza wasanii hao kuwa wote wameyaona yaliyokuwa yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii siku za karibuni na kueleza kuwa hiyo inaua sanaa.

Katibu huyo amesema  kuwa kwa kufanya hivyo wanaondoa uaminifu kwa jamii ambao wameujenga kwa gharama kubwa.

“Wote mmeona yaliyokuwa yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii siku za karibuni, sasa ile inaua sanaa.

"Leo hata makampuni yaliyoanza kuwa na imani kibiashara na wasanii wameanza kusita tena, heshimuni sanaa ni maisha ya wengi na hii itawajengea heshima badala ya kutumia kiki za kuchafuana” ameeleza Dk Abbasi.

Wakati kuhusu uondoji wa tozo youtube, Dk Abbas amesema katika kutekeleza hilo tayari Wizara yake, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameshakubaliana kubadilisha Kanuni ili wasanii na wadau wengine wa maudhui yasiyohusisha uchakataji wa habari waweze kurusha kazi zao bila kutozwa malipo yoyote.

Amebainisha kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia kuona umuhimu wa kuwanufaisha Wasanii na kukuza Sanaa nchini, hapo awali tozo ilikuwa Sh1 milioni kwa mwaka.

 “Tumefanya mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na TCRA kuhusu maudhui ya Tv  za mtandaoni, tumeona kuna tofauti kubwa sana kati ya Habari na Sanaa.

"Hivyo tutaboresha kanuni, tumeona eneo hili la Wasanii linapaswa kufanya kazi zao bure, sasa nafurahi kuwaambia kuwa kuanzia sasa wasanii wawe wa muziki au filamu changamoto hii imefika mwisho," amesema Dk. Abbasi.

Wakati kuhusu maslahi ya kazi za Wasanii zinazorushwa kupitia vyombo mbali mbali vya habari, Katibu huyoamesema, Wizara yake kupitia taasisi zinazosimamia Wasanii ikishirikiana na TCRA wanaendelea kupitia na kuanzisha mfumo wa kuangalia namna ya kazi zao zinavyorushwa kwenye vyombo hivyo ili waweze kulipwa kwa jinsi zinavyorushwa.

“Wizara kupitia Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) na wenzetu wa TCRA tunaendelea kukamilisha mfumo wa kuangalia namna ya kazi zenu zinavyoenda katika vyombo vya habari, mfumo huu unalenga kuwanufaisha Wasanii na tayari TV na Redio nyingi wamekubaliana na jambo hili,” amesema Katibu huyo.