Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasanii Bongo wenye lebo waige kwa Mondi

Muktasari:

  • Ni hivi karibuni umeshuhudiwa mgogoro kati ya Ibraah na lebo iliyokuwa inamsimamia ya Konde Music yake Harmonize na mwisho wa siku kila mmoja ameshika njia yake, huku upande wa pili The African Princess yake Nandy ikisitisha mkataba na msanii wake Yammi. 

KWA haya yanayoendelea sasa, ni wazi linapokuja suala la rekodi lebo kwa hapa Bongo bado Diamond Platnumz anaendelea kusimama kama mfano wa kuigwa licha ya yote ambayo amewahi kupitia na WCB Wasafi yake.

Ni hivi karibuni umeshuhudiwa mgogoro kati ya Ibraah na lebo iliyokuwa inamsimamia ya Konde Music yake Harmonize na mwisho wa siku kila mmoja ameshika njia yake, huku upande wa pili The African Princess yake Nandy ikisitisha mkataba na msanii wake Yammi. 

Wasanii wenye lebo Bongo au wanaotaka kuingia katika biashara hiyo wanapaswa kuiga au kujifunza mambo mawili kutoka kwa Diamond ambaye ni mshindi wa tuzo zaidi ya 20 za muziki Tanzania (TMA).

Mosi; ni jinsi anavyotumia nguvu yake ya ushawishi kuhakikisha wasanii wake nao wanakuwa wakubwa kwa kufanya nao kazi nyingi, na pili; ni jinsi anavyowatafutia au kuwatengenezea mazingira ya kufanya kazi na wasanii wengine wa nje.

Kwa miaka yote Diamond amekuwa na utamaduni wa Diamond kushirikiana na wasanii anaowasaini hasa muda mfupi baada ya kuwatambulisha na kazi husika hufika mbali kiasi kwamba baadhi yao kushindwa kutengeneza kazi kubwa tena kama hiyo pekee yake.

Hili ilianza kwa Harmonize ambaye amemshirikisha Diamond katika nyimbo zake mbili, Bado (2016) na Kwangwaru (2018) ambao ulifanya vizuri sana na hadi sasa ndio wimbo pekee wa Harmonize ambao video yake imetazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube.

Rayvanny ndiye msani pekee aliyepita WCB Wasafi ambaye amenufaika zaidi na kolabo na Diamond, wawili hao wameshirikiana kwenye nyimbo 10 hadi sasa ambapo mbili za mwisho zimetoka baada ya kuachana na lebo hiyo.

Nyimbo walizotoa pamoja ni Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024) unaofanya vizuri kwa sasa.

Kwa upande wake Mbosso ameshirikiana na Diamond katika nyimbo tano, Jibebe (2018), Karibu (2021), Oka (2022), Yataniua (2022) na Baikoko (2021) ambao ndio wimbo wake uliotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote.

Naye Zuchu, mshindi mara saba TMA, amefanya kolabo tano na Diamond ambazo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024) na Wale Wale (2025) kutoka katika albamu yake ya kwanza, Peace And Money.

Tukija kwa Rich Mavoko wimbo wake wa pili chini ya WCB Wasafi, Kokoro (2017) alimshirikisha Diamond, ulifanya vizuri ingawa video yake imeondolewa YouTube mara baada tu ya kuachana na lebo hiyo.

Lava Lava kashirikiana na Diamond katika nyimbo tano, Jibebe (2018), Bado Sana (2020), Far Away (2021), Tuna Kikao (2023), Kibango (2024). Na Queen Darleen amefanya kolabo na Diamond kupitia nyimbo za lebo, Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020). Na D Voice ambaye ndiye msanii wa mwisho kutambulishwa na WCB Wasafi, katika albamu yake ya kwanza, Swahili Kid (2023) ambayo ndio alitambulishwa nayo, Diamond alisikika katika wimbo mmoja ‘Kama Wengine’ ambao ulifanya vizuri kwa kiasi chake.


Pili; kama unafuatilia utabaini kuwa sio mara moja wala mbili Diamond kuwasaidia wasanii wake kupata kolabo kwa wasanii ambao ameshawahi kufanya nao kazi hapo awali, alifanya hivyo kwa Rich Mavoko, Rayvanny, Zuchu, Mbosso na Harmonize.

Septemba 2017 ulitoka wimbo ‘Love You Die’ ambao Patoranking kutokea Nigeria alimshirikisha Diamond, bila shaka Chibu alimtumia nafasi hiyo kumtafutia kolabo Rich Mavoko na Patoranking ‘Rudi’ ambayo ilitoka Oktoba 2017.

Ikumbukwe ‘Rudi’ ndio kazi kubwa zaidi ya kimataifa kwa Rich Mavoko kufanya akiwa WCB Wasafi, video yake ilifanyika Uingereza, huku ngoma hiyo ikifanya vizuri kwenye chati mbalimbali za radio, tv na mitandao.

Baada ya Diamond kufanya vizuri na ngoma ‘Yope Remix’ iliyotoka Septemba 2019 akishirkiana na Innoss’B kutokea nchini DR Congo, akawa amefungua njia kwa Zuchu na Rayvanny ambaye naye kaondoka WCB Wasafi.

Rayvanny katika albamu yake ya kwanza, Sound From Africa (2021) alimshirikisha Innoss’B katika wimbo wake ‘Makelebe’ ambao ulifanya vizuri kwa kiasi chake.

Haikuishia hapa, miaka mwili mbele, yaani Juni 2023 Zuchu naye akafanya kolabo na Innoss’B ‘Nani Remix’ ambao video yake ilikuwa ya kutisha sana. Hakuna ubishi bila Diamond ingekuwa ni vigumu kwa Rayvanny na Zuchu kufanikisha hilo. Katika EP yake, First of All iliyotoka Machi 2022, Diamond amemshirikisha Costa Titch kutokea Afrika Kusini katika wimbo ‘Fresh’ ambao ulikutanisha na wasanii wengine kama Focalistic na Papi Cooper.

Miezi kadhaa mbele Costa Titch ambaye alifariki duni Machi 2023 baada ya kudondoka jukwaani, akaja kusikika katika wimbo wa Mbosso ‘Shetani’ unaopatikana katika EP yake, Khan iliyotoka Oktoba 2022 na kumuwezesha kushinda tuzo ya TMA 2021.

Ikumbukwe moja ya nyimbo zinazopatikana katika albamu ya Diamond, A Boy From Tandale (2018) ni ‘Hallelujah’ akiwa na Morgan Heritage, kundi ambalo Harmonize alikuja kufanya nalo kazi katika katika albamu yake ya kwanza, Afro East (2020).