Wanafunzi vyuoni watakiwa kuchangamkia fursa mashindano ya kusaka vipaji

Wednesday May 11 2022
By Nasra Abdallah

Wanafunzi vyuoni wametakiwa kutumia vilivyo fursa zinazopatikana katika mashindano ya kusaka vipaji nje na ndani ya nchi.

Wito huo umetolewa na Ofisa Sanaa Mwandamizi kutoka Baraza la Sanaa Taifa(BASATA),Agustino Makame , wakati wa hafka ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Shindano la Uni Talent.

Makame amesema wanafunzi wana kila sababu ya kuzikimbilia fursa kikamilifu ikiwemo Mashindano ya kusaka vipaji Ili kuendeleza vipaji vyao pamoja na kukuza tasnia ya burudani nchini kwa ujumla.

"Kuwepo Kwa mashindano ya kusaka vipaji ikiwemo ya "Uni Talent" ni ishara tosha kuwa wanafunzi vyuoni wana uwanda mpana wa kuonyesha vipaji hivyo ni vema kuendelea kupeperusha bendera kwa kuzikimbilia fursa kama hizo, " amesema Makame.

Hata hivyo Makame ametoa wito kwa wadau na Makampuni kuunga mkono vipaji vyuoni kwa kushirikiana na wadau wanaoandaa mashindani ya aina hiyo ili wakiwemo Maroon ili kuhakikisha msimu ujao unakua wa kitofauti zaidi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Maroon Entertainment wanaondaa Shindano la "Uni talent" Chrispine Kiondocha amesema msimu huu ni wa tatu kufanyima kwa shindano hilo ambapo malengo yake ni kuhakikisha wanaendeleza vipaji kwa wanafunzi vyuoni na kuahidi msimu wa nne utakuwa mzuri zaidi.

Mmoja wa washindi liyejitambulisha kwa jina la Osmond Soka, amesema atahakikisha anaongeza juhudi katika kazi yake ya ucheshi ili kufika mbali zaidi na kubainisha kuwa
ushindi huo utakuwa chachu ya kuongeza juhudi katika kazi zingine ili kujitangaza na kuitambulisha taifa lake.

"Nawashukuru waandaji wa Unit Talet pamoja na familia yangu uongozi nzima wa chuo changu, nitahakikisha naendeleza kipaji changu cha ucheshi ili kufika mbali zaidi, " alisema Soka.

Katika shindano hilo mshindi wa kwanza kundi kutoka Chuo cha Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo (TaSUBa) ni African Cousins wamepata kitita cha Sh10 milioni huku mshindi was pili Afro Dreams walinyakulia Sh3 milioni wakati mshindi tatu Osmond Soka kutoka Chuo cha Agustino mkoani Mwanza akiondoka na Sh1 milioni.

 

Advertisement