Vichwa vitatu kabla bifu ya Diamond na Ommy Dimpoz

KABLA ya bifu lao walikuwa ni marafiki wakubwa, Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006 inadaiwa ndiye chanzo cha ugomvi wao kufuatia mrembo huyo kutokea kwenye video ya Ommy Dimpoz (Wanjera) ikiwa ni muda mfupi baada ya kuachana na Diamond Platnumz.

Ikumbukwe Diamond ndiye alimshauri Ommy Dimpoz asiutoe wimbo wake, Nai Nai bila kufanya video yake, ndipo Dimpoz akamtafuta Director Adam Juma wakafanya video hiyo na baada ya hapo mengine ni historia.

Kabla ya bifu, kuna vichwa vitatu Afrika Mashariki ambavyo viliwakutanisha Diamond na Ommy Dimpoz katika ngoma zao, ni kipindi Diamond anaanza kuwika na WCB Wasafi, huku Ommy Dimpoz akiwa na PKP (Poz kwa Poz) ambayo ameiweka pembeni kwa sasa.

Hata hivyo, wawili hao ambao sasa ni mfano wa paka na chui hawajawahi kushirikishana katika nyimbo zao, wao wanakutana tu katika ngoma za wasanii wengine kama ifuatavyo;


1. DULLY SYKES

Ngoma ya Dully Sykes, Utamu (2012) iliyotengenezwa kwenye studio yake, 4.12 na Bongo Records ilikuwa ni ngoma ya pili kuwakutanisha Diamond Platnumz na Ommy Dimpoz baada ya ile ya Kigoma All Stars, Leka Dutigite.

Diamond na Dimpoz wakiwa na mkongwe huyo wa Bongofleva walimuonyesha ni jinsi gani wao kama wasanii wapya katika tasnia kwa wakati huo wanavyoweza kutengeneza muziki mzuri na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Video ya wimbo huo iliyoongozwa na Director Adam Juma ilifanya vizuri hadi kuchezwa na vituo vikubwa vya runinga vya nje na hadi sasa ikiwa na imetazamwa (views) zaidi mara milioni 1.2 katika mtandao wa YouTube.

Ikumbukwe Dully Sykes ana mchango mkubwa kwa Diamond na Alikiba hadi kutoka kimuziki, huku Alikiba akimtoa Ommy baada ya kushirikishwa katika wimbo wake 'Nai Nai' ulimtambulisha na kumpatia tuzo yake ya kwanza ya TMA 2012.


2. DIVA

Mrembo huyu akiwa Mtangazaji wa Clouds FM kabla ya Wasafi FM alipo sasa, aliamua kujaribu bahati yake kwenye Bongofleva kama walivyofanya Lady Jaydee, Ray C na Vanesaa Mdee ambao walianza kama Watangazaji na kuja kufanikiwa kimuziki.

Ngoma yake ya kwanza, Piga Simu (2012), Diva alimshirikisha Bosi wake wa sasa, Diamond Platnumz, ngoma hiyo iliyorekodiwa Fishcrub kwa Lamar ilifanya vizuri kwa kiasi chake.

Baada ya muda waliamua kutoa remix ya ngoma hiyo, ndipo Ommy naye akapewa shavu, ila hakuweza kufanya video yake licha ya kukutanisha wasanii wakubwa. Baadaye Diva alikuja kufanya kazi na wasanii kama Mr. Paul, Mwana FA n.k, huku akitangaza ujio wa albamu ambayo hadi sasa haijatoka.  

Hata hivyo, Diva aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa hana mpango wa kuendelea na muziki kwani mwanzo alikuwa anafanya kama sehemu ya kujifurahisha tu. Anashindwa kuendelea na muziki kwa sababu yeye ana aibu sana kufanya shoo jukwaani, na pia ni msanii wa studio tu na sio mtumbuizaji.


3. VICTORIA KIMANI

Hapa tunavuka boda hadi nchini Kenya, muziki wa Bongofleva unakutana na muziki wa Genge, tunakutana na Victoria Kimani anayefanya vizuri pande hizo, alishawahi kufanya kazi na Chocolate City ambayo ni lebo kubwa Nigeria.

Miaka tisa iliyopita Victoria Kimani aliachia ngoma, Prokoto (2014) na kuwashirikisha Diamond Platnumz na Dimpoz, ilikuwa ngoma nzuri iliyolenga soko la kimataifa zaidi, na hata ubora wa video ya ngoma hiyo uliashiria hilo, na kwa kiasi kikubwa walifanikiwa.

Ikumbukwe Victoria amewahi kushirikishwa na wasanii kadhaa wa Bongofleva katika ngoma zao, miongoni mwao ni Stereo katika ngoma 'Never Let You Down', AY ngoma ya 'Love You More' na Prof. Jay wimbo wake wa 'Woman'.

Victoria alikuwa msanii wa kwanza wa kike kusainiwa Chocolate City hapo mwaka 2012 na kuachia wimbo wake 'Moto' ambao ni wa kwanza chini ya lebo hiyo. Amewawahi kufanya kazi na wasanii wengine wa Afrika kama Tekno, Arielle T, Yemi Alade, Sarkodie, Ice Prince, Phyno, Vanessa Mdee n.k.