Uongozi wa Alikiba wafunguka onyo la Cosota

Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imewaonya watu wanaudurufu na kuuza kazi za filamu na muziki ikiwemo albamu mpya ya msanii wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Ally Saleh maarufu ’Alikiba’ aliyoiachia hivi karibuni.
Onyo hilo limetolewa leo na Alhamisi Oktoba 14, 2021 na Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki, Doreen Sinare kupitia taarifa yake kwa umma.
Albamu hiyo iliyopewa jina la ‘Only One King’  yenye  nyimbo 16, ilizinduliwa wiki moja iliyopita, ambapo inakuwa ni albamu ya tatu kwa Alikiba kuitoa tangu alipoanza muziki.
Hata hivyo juzi kupitia ukurasa wake msanii wa Bongofleva, Baghdadi aliandika kwamba anasikitika kuona albamu hiyo ikiwa inauzwa kama njugu maeneo ya Mwenge.
Hili huenda likawa  limewazindua COSOTA na kutoa tamko hilo la kuonya watu wanaendelelea na kazi za kudurufu kazi za wasanii kuacha mara moja huku akigusia  albamu hiyo ya Alikiba.
Katia taarifa hiyo ilisema “Hivi karibuni baada ya mmiliki wa Rekodi ya Lebo ya Kings Music na msanii wa muziki, Alikiba kutoa taarifa ya kupatikana kwa albamu yake ya ‘Only One King’ katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kusambaza kazi za muziki, kumeibuka watu  wanaodurufu kazi hiyo na kuuza mtaani pasipo makubaliano yoyote.
Taarifa hiyo ilienda mbali zaidi na kueleza kuwa Sheria ya Hakimiliki  na Hakishiriki namba 7 ya mwaka 1999 imeeleza kuwa kusamabaza kazi ya mbunifu yoyote bila ridhaa yake ni kosa kisheria na adhabu yake ni faini isiyopungua Sh20 milioni  au kifungo cha miaka mitatu mpaka mitano au vyote kwa pamoja.
“Cosota inatoa wito kwa wazalishaji na wasambazaji wote nchini kuacha kuzalisha na kusambaza kazi zote ambazo hazijazingatia sharia.
“Lazima kuheshimu kazi za wabunifu na wawekezaji wanaofanya kuandaa na kuzalisha kazi hizo kwani hali hii ya uharamia inachangia kudhoofisha ukuaji wa sekta ya Sanaa nchini  na kupoteza mapato ya wasanii,”ilisema taarifa hiyo.
Mwananachi iliutafuta uongozi wa Kings Muziki, kupitia meneja wa Alikiba, Aidan Seif, ambaye amesema hata yeye alishakutana na CD mtaani na kupitia timu yao ya wanasheria iliwasailiana na mamlaka husika ili kushughulikia suala hilo.
Seif alitumia alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Baghdadi kwa kupaza sauti kuhusu uharamia huo ambao alieleza haukubaliki.