UMESIKIA... Zari, Hamisa, Tanasha wote ni pacha kwa Mondi

Muktasari:
- Ili kushikilia mafanikio hayo Diamond amekuwa akihakisha hatoki nje ya utamaduni huo, hilo limefanya wanawake wengi hasa wale aliojaliwa nao watoto ambao ni Zari The Bosslady, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna kuwa na sifa zinazofanana.
UKIACHANA na muziki, hakuna ubishi kuwa umaarufu wa Diamond Platnumz kwa sehemu nyingine umechangiwa kwa kuwa na uhusiano na wanawake wenye majina makubwa katika tasnia ya muziki, filamu na mitindo.
Ili kushikilia mafanikio hayo Diamond amekuwa akihakisha hatoki nje ya utamaduni huo, hilo limefanya wanawake wengi hasa wale aliojaliwa nao watoto ambao ni Zari The Bosslady, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna kuwa na sifa zinazofanana.
Ikumbukwe Diamond amezaa na Zari kutoka Uganda watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016), Hamisa mtoto mmoja, Dylan (2017) na Tanasha kutoka Kenya mtoto mmoja, Naseeb Jr (2019).
Je, ni kwa namna gani Zari, Hamisa na Tanasha wana sifa zilizofanana kwa Diamond kutoka WCB Wasafi?, katika makala haya tunaenda kuangazia mambo matatu yanayoweka wazi hilo.
Mosi; wote wanamuziki, warembo wote aliozaa nao Diamond ni wasanii wakiwa wamewahi kufanya muziki kwa kurekodi nyimbo lukuki kwa nyakati tofauti, pengine hiki ni moja ya kigezo muhimu pale anapochagua baby mama, haiwezi kuwa bahati mbaya.
Zari ana nyimbo zake kama Oliwange, Jukila, Kangume na Kikooma alizoimba kwa lugha ya nyumbani kwao Uganda, nyingine ni Hotter Than Them, In Love With The Dance Floor na Falling In Love.
Vilevile Zari ambaye uhusiano wake na Diamond ulianza mwaka 2014 baada ya kukuta safarini katika ndege, ameonekana katika video mbili za mwimbaji huyo ambazo ni Utanipenda (2015) na Iyena (2018).
Ingawa Hamisa nyimbo zake nyingi zilitoka baada ya kuzaa na Diamond ila tayari alisharekodi awali, ameshatoa EP, Yours Truly (2022) ikiwa na nyimbo sita, huku akishirikiana na Diamond, Otile Brown, Christian Bela, Whozu na Korede Bello wa Nigeria.
Ni Hamisa ambaye pia alionekana katika video ya Diamond, Salome (2016) na inaelezwa kipindi hicho ndipo ukaribu wao ulianza ingawa halifanya siri kwa muda chote hadi walipokuja kupata mtoto.
Kwa upande Tanasha, hakuna asiyejua uwezo wake wa kuimba, ana nyimbo kubwa kama Radio, Gere, Liar na La Vie, huku akitoa EP moja, Donna Tella (2020) akiwashirikisha Diamond, Mbossso na Khaligraph Jones kutoka Kenya.
Tanasha na Diamond wameshirikiana katika wimbo mmoja, Gere (2020) ambao ulimtangaza zaidi mrembo huo katika ulimwengu wa muziki na hadi sasa video yake ikiwa na 'views' zaidi ya milioni 50 YouTube.
Pili; wote wanamitindo, urembo na mitindo ni sifa nyingine anayoizingatia Diamond, hivyo Zari, Hamisa na Tanasha wote wana sifa hizo na kila mmoja ametumikia tasnia hiyo kwa nyakati tofauti.
Hakuna asiyejua ukali Zari upande wa urembo na mitindo na mara kadhaa amesimama kama Jaji kwenye mashindano ya urembo Uganda, pia amesomea masuala ya urembo akiwa na Diploma ya Cosmetology iliyoipata nchini Uingereza.
Kabla ya muziki Hamisa alikuwa anafanya mitindo na ndio fani iliyomtangaza zaidi, ameshinda tuzo Tanzania, Afrika Kusini na Nigeria kama Mwanamitindo Bora, huku akishinda taji la Miss XXL, After School Bash 2010.
Hamisa ameshinda tuzo za mitindo kama Abryanz Style Fashion 2016 (Uganda), Starqt Awards 2017 (Afrika Kusini), Swahili fashion Week Awards 2018 (Tanzania), Scream Awards 2021 (Nigeria), Young C.E.O Round Table 2022 (Tanzania) na kadhalika.
Naye Tanasha kabla ya muziki alikuwa akifanya mitindo chini ya wakala, Dominique Model's huko Brussels nchini Ubelgiji, huku akitumia jina la Zahara Zaire kwenye kazi zake ili kujitambulisha kuwa anatokea Afrika.
Tatu; wote wana ushawishi, wakati Diamond anaanzisha uhusiano na Wema Sepetu hakuwa na maarufu kama mrembo huyo, baada ya kuachana naye Diamond alijenga utamaduni wa kuwa na uhusiano na wanawake maarufu na wenye nguvu ya ushawishi.
Hadi sasa ni wanawake watano Afrika Mashariki ambao wamefikisha wafuasi (followers) zaidi ya milioni 10 Instagram, watatu kati yao Diamond amewahi kuwa na uhusiano nao, huku wawili akizaa nao ambao ni Zari na Hamisa.
Na kwa Kenya pekee, Tanasha mwenye wafuasi zaidi ya milioni 4.1 ni mtu wa tatu kwa ushawishi Instagram akiwa ametanguliwa na Lupita Nyong'o na Eric Omondi.
Utakumbuka wakati Diamond anaanzisha uhusiano na Tanasha mwaka 2018, tayari mrembo huyo alikuwa maarufu Afrika Mashariki kama mtangazaji wa redio NRG, mwanamitindo na msanii, huku wengi wakimfahamu tangu alipotokea katika video ya Alikiba na Christian Bella, Nagharamia (2015).