TUONGEE KISHKAJI: Mashabiki wanapenda ngoma za matusi

MIAKA ya nyuma, nilipokuwa damu changa, kuna mtandao mmoja wa simu ulikuwa unatoa ofa moja ya ajabu sana. Ilikuwa ikishafika saa 4 usiku, ukimpigia mtu na mkaongea kwa dakika tatu, zinazofuata zote ni bure.
Ilikuwa ni ofa ya ajabu kwa maana mbili. Ya kwanza ni kwa watu wazima ambao pengine walishangaa, saa nne usiku unampigia nani? Muongee nini? Wakati hiyo ni mida ya kupumzika ili kesho uwahi kwenye mitikasi.
Na ajabu nyingine ilikuwa ni kwetu sisi wanafunzi. Sisi tulikuwa tunashangaa inawezekana vipi mtu kupewa ofa ya kuongea bure muda wote huo? Hiyo ilikuwa ofa nzuri ajabu.
Sasa wengi wetu tulikuwa tunaitumia hiyo ofa kuongea na wachumba. Unampigia simu mtoto mkali, mnaongea weee! Mnaongea hadi stori zinaisha mnaanza kuambiana, ''Nambie", "Lete Stori" utadhani ndo mnaanza kuongea.
Lakini moja ya jambo la msingi kwenye hayo mazungumzo ilikuwa ni kuimba. Yaani kama kweli wewe ni mtaalamu wa mapenzi ya kwenye simu lazima umuimbie mtoto bhana. Hapo unajua ngoma zote za bongofleva za mapenzi na pia ushakariri sana mistari ya ngoma za mapenzi za kizungu hususan classic. Ma West Life, Ma Lionel Richie, uko vizuri.
Basi unamuimbia mtoto na sauti yako kama chura lakini ukimaliza anakusifia anakuita we mkali.
Nawaza ofa hiyo ingekuwepo sasa hivi madogo wangeteseka sana kupata ngoma za kuimbiana, maana nyimbo za mapenzi hakuna kabisa siku hizi, ngoma za ngono ndo zimejaa.
Zamani kina Diamond wa Lala Salama, Kassim Mganga Tajiri wa Mahaba, Alikiba wa My Everything, Ben Pol wa Nikikupata walitubless sana. Walikesha studio kwa ajili ya kuhakikisha tunapata ngoma za kuwaimbia wachumba.
Lakini ingekuwa leo hii ungekuwa mtihani mkubwa sana. We unadhani unaweza kumuimbia mtoto kamata kamata shika chini kamata? Unadhani unaweza kumuimbia mtoto Amelowa? Huwezi.
Ngoma za mapenzi zimebaki chache sana siku hizi. Kwahiyo hata madogo wangeamua kutumia za siku hizi wangekuwa wanatumia ngoma za wasanii wale wale kila siku. Kina Jay Melody, ngoma kadhaa za Mbosso na Marioo au Zuchu kwa mbali. Na za Zuchu atuzihesabii kwa sababu mwanaume huwezi kuimba ngoma za Zuchu hadharani.
Wasanii, mameneja, waandaa matamasha, vyombo vya habari na wadau wote wanaohusika na masuala ya kuandaa muziki na kuusambaza wanasema ngoma za ngono ndo zinauza sana. Kwahiyo tukiwaambia waache ni kama unamwambia mama ntilie aache kupika ubwabwa, ataishi vipi?
Na pia, kama wanaongopa, kwanini hizo ngoma mpaka leo hazijakosa wasikilizaji? Zinasikilizwa sana tu kuliko ngoma za mapenzi, kuliko ngoma za aina nyingine?
Kama kweli mashabiki mnahisi hamuzipendi, acheni kwenda kuzingalia YouTube, acheni kwenda Spotify kuzisikiliza, acheni kuziomba kwenye maredio na hata acheni kuwaambia Madj wazipige mkiwa club.