Snura akiri kuunga kwa mume wa mtu

Muktasari:
- Haikushangaza Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) walivyodata na kuifungia mara moja. Haikushangaza Youtube walivyoichomoa mara moja. Haijawahi kutokea video kama ile Bongo, labda kwenye vigodoro.
VIDEO nyingi za Bongo Fleva zimetoka, lakini ile ya Chura ya Snura Mushi ilikuwa ni balaa. Ni gumzo mpaka kesho. Ni video moja ya kikatili iliyofanywa na wendazimu fulani hivi.
Haikushangaza Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) walivyodata na kuifungia mara moja. Haikushangaza Youtube walivyoichomoa mara moja. Haijawahi kutokea video kama ile Bongo, labda kwenye vigodoro.
Huyo ni Snura, ni balaa. Anaimba kama vile dunia inakwisha kesho, halafu anayakata mauno kama vile hana mifupa.
Nyimbo zake, yeye ndiye stelingi halafu ana wadada wake wawili hivi wanacheza kinoma.
Alianzia kwenye filamu za Kibongo, akaona hakuna ishu. Ghafla akili yake ikahamia kwenye muziki. Ameishika Bongo Fleva. Ametengeneza muziki wa aina yake, pamoja na Zuwena Mohamed, Shilole ‘Shishi baby’.
Sasa wiki hii Mwanaspoti lilipata fursa ya kupiga stori mbili tatu na Snura. Amefunguka kinoma.
MUZIKI WAKE
Snura ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Vumbi la Mguu’ anasema tangu aanze muziki amebahatika kutoa albamu moja iliyompatia mafanikio makubwa kwani nyimbo zake zimependwa na mashabiki na kusababisha kufanya vizuri sokoni.
Albamu hiyo Snura ameitaja kuwa inaitwa Chura yenye nyimbo; Majanga, Debe la Vanga, Nimevurugwa, Ushaharibu na Uko Nyuma Sana.
UVUMILIVU WAMTOA
Snura anasema ameweza kuzishinda shida alizozipitia kutokana na uvumilivu, vinginevyo asingefika alipo.
Anasema wakati alipoamua kutoka nyumbani kwa wazazi wake na kwenda kuanza maisha yake, ilifikia kipindi alikuwa anashinda njaa na wakati mwingine kushindia ugali kwa mbilimbi, lakini hakujali.
“Nilishalala njaa sana tu, wakati natoka kwa wazazi na kuanza maisha yangu binafsi ya kujitegemea, nilikuwa na wakati mgumu, nakumbuka nilikuwa nashindia ugali na mbilimbi na nilikuwa jeuri kwa sababu maisha hayo hayakufanya nimtegemee mwanaume,” alisema.
“Nilikuwa jeuri sana japo nilikuwa na shida zangu, ila kati ya vyote suala la kodi lilikuwa linaniumiza kichwa vibaya mno, mawazo yalikuwa yanaongezeka mara mia kila nikifikiria kodi ya baba mwenye nyumba na kipindi hicho nakumbuka kodi ilikuwa Sh20,000 kwa mwezi ila ilikuwa mbinde kuipata,” anasema mwanadada huyo mwenye bonge la ‘Chura’.
APIGA TAARABU
Kama ulikuwa hufahamu, Snura kumbe kipaji chake kilianzia kwenye muziki kabla ya kuigiza na alikuwa ni mwimbaji wa taarabu na Kundi la ‘New Best Star’ mwaka 2004.
Baada ya hapo alianzisha kundi lake la muziki aliloliita ‘Chanya na Hasi’ pamoja na vijana wawili mmojawapo akiwa marehemu Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’ kabla hajajiunga rasmi na sanaa ya maigizo.
Kipaji cha Snura kiligunduliwa na mtu aliyefahamika kwa jina la Siasa, ambaye ndiye aliyemfuata na kumshauri kuigiza baada ya kuvutiwa na uzuri na umbo lake ndipo alipomshawishi kuwa angeweza kufanya vizuri kama angejiingiza katika sanaa, hiyo ilikuwa ni mwaka 2006.
Anasema bahati nzuri kwake mwaka huo alipata nafasi ya kuigiza kwenye Filamu ya Mfalme Seuta iliyoongozwa na Gumbo Kihorota. Baadaye alicheza filamu za Zinduna na Hitimisho.
Snura anasema alianza kujipatia umaarufu kupitia Filamu ya ITUNYAMA, na pia kupitia igizo la Jumba la Dhahabu akiwa chini ya Mwongozaji, Tuesday Kihangala ‘Mr Chuzi’.
AZUNGUMZIA NDOA
Kimtazamo Snura Mushi ukimuangalia kwa haraka unaweza kudhani kuwa ameolewa lakini mwenye anafunguka hapa.
“Unajua mimi si kama sitaki ndoa, ila huwa najifikiria sana, kuwa na mume si kitu cha mchezo mchezo, hivyo ni vyema kujipanga na kutokukurupuka,” anasema.
Siwezi kukubali kirahisi eti kwa sababu tu nimetajiwa ndoa. Yaani ni lazima nimjue kwanza mtu ni wa aina gani kwani hayo ni maisha yangu.
“Najua nikiingia kichwa kichwa, mwisho wa siku nitaumia na nitakuwa na historia nyingine kabisa kwani sitavumilia.”
KUIBA MUME
Snura kwa sasa ana skendo ya kumchukua mpenzi wa msanii mwenzake, Salma Jabu ‘Nisha’ aitwaye Minu.
“Huyo Minu si mpenzi wangu ila kwa kuwa watu wanasema hivyo na mimi nimeamua kuunganisha tu, maana kila nikiwaambia watu hawaelewi. Minu nimefahamiana naye baada ya kuandika wimbo ambao aliona nafaa kuuimba, na aliponiletea nikaona ni mzuri na ndipo tulipoanza kuzoeana na haikupita siku chache ikawa ni Siku ya Kuzaliwa kwake ndio nikamtakia heri ya kuzaliwa, hapo ndio ikawa kosa,” anaeleza.
KITU ANACHOJUTIA
Snura amesema kitu ambacho anajutia katika maisha ni kipindi cha nyuma alipokuwa anavaa nguo za nusu uchi, hadi hapo alipogundua ni makosa.
Snura anadai awali alikuwa akivaa mavazi ya nusu uchi au nguo za kumbana, lakini kwa sasa amejirekebisha na anatambua nguo zinazompendeza ili kutokuleta sintofahamu kwa mashabiki wake.
“Kwa kweli nashukuru ushauri wa watu katika suala la mavazi. Nimeshajirekebisha. Najuta hadi leo, nilikuwa nawakosea mashabiki wangu,” anamalizia.