Rayvanny almasi inayotoweka migodi ya WCB-1

Rayvanny almasi inayotoweka migodi ya WCB-1

MIMI ni Almasi mchangani sema tu sijashtukiwa, mgodi unaotembea wajinga wanashindwa kuelewa!. Ni miongoni mwa mistari kutoka kwenye wimbo wa Mwana FA, Binamu.
Hiyo ni sawa na mwimbaji wa Bongofleva, Raymond Shaban Mwakyusa ‘Rayvanny’ ambaye ni mfano wa Almasi iliyochimbwa na Diamond Platnumz katika mgodi wake, WCB Wasafi miaka saba iliyopita.
Sasa Almasi hii inayong’aa vilivyo inatajwa ipo katika mchakato wa kundoka katika migodi ya WCB baada ya thamani yake kupanda mara dufu katika soko.
Je, ni wapi msanii huyu ametoka?, yeye ni nani?, amefanikiwa vipi kimuziki? kwanini anatajwa kuondoka WCB?, na akiondoka itakuwaje?. Huu ni mfululizo wa makala unaoenda kuangazia hilo kwa mapana yake;  
Mwaka 2012 Rayvanny alijiunga na kundi la Tip Top Connection ambalo linasimamiwa na Babu Tale, kundi hili limekuza na kutengeneza wasanii wenye majina wakubwa katika Bongofleva kama MB Dogg, Madee, Keysha, Spack, Tundaman, Kassim Mganga, Z Anto, Dogo Janja na wengineo.
Hata hivyo, safari haikuwa rahisi, alichoka na kukata tamaa na muziki na ndipo alipomfuata Babu Tale na kumueleza muda anazidi kwenda na haoni dalili ya kutoka, lakini Madee akamshauri awe umvumilivu.
Alifanikiwa kutoa wimbo mmoja akiwa Tip Top uitwao ‘Upo Mwenyewe’ ambao haukufanya vizuri kwa kile alichoeleza wakati anauachia hakuwa kwenye maelewano mazuri na Babu Tale ambaye ndiye aliyemleta kwenye kundi hilo.
Uwezo wake wa kuandika nyimbo umlimfanya kuaminika ndani ya Tip Top alipokaa kwa miaka mitatu, mathalani alishiriki kuandika wimbo wa Dogo Janja, My Life uliomrejesha kwenye muziki baada ya kurudi katika kundi hilo akitokea Mtanashati Entertainment.
Wakati Dogo Janja anaenda na Madee studio za MJ Records kurekodi wimbo huo chini ya Prodyuza Marco Chali, ndipo Rayvanny alikuwa anashuti video ya wimbo wake kwanza chini ya WCB Wasafi na uliomtoa kimuziki, Kwetu.
Rayvanny alijiunga na WCB mwaka 2015 akiwa ni msanii wa pili wa lebo hiyo baada ya Harmonize, tayari Rayvanny alikuwa ameshaana na muziki wa Rap na kujikita katika uimbaji.
Ikumbukwe mwanzoni alikuwa akifanya muziki wa Rap kabla ya kuanza kuimba ambapo mwaka 2011 aliibuka mshindi katika mashindano ya Free Style pale Coco Beach, Dar es Salaam. Hata ukisikiliza ngoma zaka Sugu na Pochi Nene, unaweza kuona ni kwa jinsi gani ana uwezo mzuri wa kuchana.
Huyu alikuwa Rapa wa pili ndani ya WCB baada ya Diamond ambaye naye aliamua kuachana na aina hiyo ya muziki kwa madai hakuona uwekano wa kutoka kimuziki. Diamond ameonyesha uwezo wa kuchana kwenye ngoma kama Mtoto wa Mama alioshirikiana na Godzilla, pia kuna Fresh Remix wake Fid Q.
Alipojiunga WCB, Rayvanny amechangia melody kwenye wimbo wa Diamond, Make Me Sing aliomshirikisha AKA wa Afrika Kusini, Zigo Remix wake AY ambao Diamond ameshirikishwa.
Mbosso ana mchango mkubwa kwa Rayvanny kujiunga WCB kwani ndiye aliyempigia simu na kumwambia aende studio ambapo ndipo alipokutana na Diamond hadi kuona uwezo wake. Ni kipindi ambacho Mbosso (Maromboso) alikuwa chini ya Menejimenti ya Mkubwa na Wanae yake Mkubwa Fella.
Ilimchukua Rayvanny hadi Aprili 2016 ndipo akaachia wimbo wake kwanza, Kwetu ambao ndio ulimtoa na kubadilisha historia ya muziki wake hadi upande wa familia na kuanza kuitwa Baba.
Hadi sasa Kwetu ndio wimbo pekee ambao Rayvanny kafanya pekee yake (Solo) ambao video yake imetazamwa zaidi YouTube, ndani ya miaka sita imefikisha views milioni 30. Zenye views zaidi ya hiyo ni Tetema ft. Diamond (mil 66), Number ft. Zuchu (mil 63), Mwanza ft. Diamond (mil 56), Teamo ft. Messias Maricoa (mil 40) na Mmmh ft. Willy Paul (31).
Katika video ya Kwetu ambayo ilishika namba sita kati ya video zilitazamwa zaidi Tanzania mwaka 2016, ndipo Rayvanny alipokutana na mpenzi wake na mzazi mwenziye, Fahyma maarufu kama Fahyvanny ambaye wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume, Jaydan aliyezaliwa Aprili 2017.
Baadaye Fahyvanny akaja kuonekana kwenye video nyingine za Rayvanny kama Natafuta Kiki (2016) na Safari (2017). Na huyu ndiye mrembo pekee duniani aliyefanya video nyingi na Rayvanny.
Wimbo wake wa pili, Natafuta Kiki uliotoka Mei 2016 ulifanya vizuri hadi kuchaguliwa kuwani tuzo za Afrika Entertainment Awards, USA (AEAUSA) kama Best New Artist na Best New Talent, pia aliwania MTV MAMA 2016 katika kipengele cha Best Breakthrough Act ingawa hakufanikiwa hakuhinda.
Ushindi ulienda kwa msanii wa Nigeria, Tekno, na ni mwaka ambao hata wasanii wengine wa Tanzania waliowania tuzo hizo kama Alikiba, Diamond Platnumz, Yamoto Band, Navy Kenzo na Vanessa Mdee, hawakuweza kushinda.
Na katika ngoma hiyo, ndipo kwa mara ya kwanza aligusia kwamba kuna siku ataachana na lebo hiyo na kwenda kujiunga na nyingine. Je, ni ipi?, kwa namna gani?, hilo linasadifu vipi ukweli wa mambo kwa sasa?, katika toleo lijalo tutaangazia hilo. Usikose.