Mzee Chillo : Asema waandaaji filamu wanapenda uvaaji wa vichupi

Muktasari:
- Mbali ya hilo, Mzee Chillo, anapasua bomu jingine kwa kukiri kuwa katika sanaa hiyo kuna rushwa ya ngono.
MWIGIZAJI mkongwe wa Bongo, Mzee Chillo, amesema waandaji wa filamu wanafurahia vichupi kwa wasanii wa kike ili kuuza kazi zao licha ya kuwa vazi hilo lipo kinyume na maadili ya Kiafrika.
Msanii huyo amedai kuwa hali hiyo inawadhalilisha mabinti hao ingawa baadhi yao hawatambui.
“Waandaji wa filamu wamekuwa si wakali wa kuhimiza wasanii wa kike wavae mavazi yanayoendana na utamaduni wa Kiafrika, badala yake wanafurahia hali hii bila kufahamu kuwa wanawashushia hadhi na kuwafanya jamii iwadharau,” alisema.
“Wasichana wenyewe wamekuwa si watu wa kujiheshimu, hawana mwamko wa kuvaa nguo zinazoendana na jamii zao, badala yake wanavaa zisizo na heshima.”
Mbali ya hilo, Mzee Chillo, anapasua bomu jingine kwa kukiri kuwa katika sanaa hiyo kuna rushwa ya ngono.
Anasema: “Hakuna jambo nisilolipenda katika maisha kama rushwa ya ngono. Utakuta msanii wa kike anakuja ana kipaji anataka kuigiza, anakutana na msanii mwenye jina kubwa na anamwambia kuwa asijali atamsaidia, lakini hapo hapo anapewa sharti kuwa mpaka wakalale wote.
“Baada ya mpango huo kukamilika msanii huyo anaenda kwa prodyuza kumwambia kuwa kuna msanii mzuri inabidi ampangwe kwenye nafasi fulani ya filamu mpya... Huu ni udhalilishaji kwa dada zetu.
“Udhalilishaji huu haupaswi kuvumiliwa na unaleta picha mbaya katika jamii.”
Mzee Chillo anaongeza kuwa umoja wa wasanii usio imara, rasilimali zisizotosheleza na wananchi kutokuwa na ushirikiano wa kununua kazi halisi ni kikwazo kwa maendeleo yao kwenye filamu.
“Umoja wetu wa wasanii umekuwa si imara, wanachama wamekuwa hawana nguvu kushirikiana kwenye jambo fulani ili lipatiwe mwafaka, kinachotakiwa ni kuwa na sauti moja tukikubaliana kufanya jambo basi liwe kwa vitendo na si kwa mdomo.
“Rasilimali nazo zimekuwa ni kikwazo sasa hivi tumeshindwa hata kutoa filamu zetu wenyewe na kuzisambaza, lakini imekuwa tofauti kwenye filamu tunasimamiwa hadi kwenye suala la usambazaji.
“Wananchi nao wamekuwa wakiturudisha nyuma kwa namana moja au nyingine. Wamekuwa mstari wa mbele kununua nakala zisizo halisi ambazo zimekuwa zikiuzwa bei nafuu tofauti na zile halisi.”
Pia anawaasa wasanii kuhusu elimu akisema kwa kuwa tasnia hiyo inavuka mipaka, inawapasa wasanii kujiendeleza kielimu. Mzee chillo ameigiza filamu nyingi, lakini ameweka zaidi katika filamu za ‘Huba’ na ‘Ray Of Hope’ .
“Hakuna msanii ninayevutiwa na kazi zake kama, Steven Kanumba (marehemu). Nilifanya kazi naye na niliuona uwezo wake, alikuwa mtu tofauti na alijituma,” alisema.
“Jambo jingine kubwa ni kuwa hakukata tamaa, ndiyo tofauti kati yake na wasanii wengine. Kanumba alikuwa asiyeridhika kwani kila siku alikuwa mtu wa kubuni mbinu mpya ili tasnia hii iweze kupiga hatua.
“Hii ni tofauti na wasanii wengine ambao wameridhika na pale walipofikia.”
Anaongeza: “Kwa upande wa msanii wa kike ninayevutiwa na kazi zake ni Hidaya Njaidi, huyu anaubeba uhalisia na utamaduni wa nchi kiukweli, pia ni mtu anayejiheshimu kuliko kawaida.
“Kwa upande wa Nigeria ninawapenda Mercy Jonson, Nkriu na Emmanuel Francis hawa wote nimewahi kufanya nao kazi na ninajua uwezo wao.”
Kwa upande wake anasema sekta ya filamu imemsaidia kujikwamua kimaisha licha ya kumpa umaarufu mkubwa hadi kumpa mikataba ya biashara.
“Ninaendesha maisha ya familia yangu vizuri,” anasema Mzee Chillo ambaye kitaaluma ni Mwalimu wa elimu ya Sekondari.